HEADER AD

HEADER AD

BoT : NI MARUFUKU KUFANYA BIASHARA YA KUBADILISHA FEDHA ZA KIGENI BILA KUWA NA LESENI


>>Watakaokiuka Sheria na Kanuni kukiona

>> Hairuhusiwi kuhamisha biashara kwenda eneo lingine bila idhini ya Benki Kuu.

>>Hairuhusiwi kugawa miamala kwa nia ya kuepuka kutoa risiti na nyaraka

Kabla ya kuanza kuchukua hatua BoT yawapa elimu ya sheria ya fedha za kigeni wafanyabiashara wa mpakani 


Na Dinna Maningo, Tarime

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia Meneja Msaidizi Kitengo cha Huduma za Kifedha kwa Taasisi Maalum, Omary Msuya imetoa elimu ya sheria ya fedha za kigeni  ya mwaka 1992 kwa wafanyabiashara wa Sirari wanaofanya biashara mpakani mwa nchi ya Tanzania na Kenya.

Pia Benki hiyo imepiga marufuku Wafanyabiashara wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni kufanya biashara hiyo bila kuwa na leseni iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania pamoja na ukiukaji mwingine kinyume cha sheria na kanuni zilizowekwa.

Hayo yameelezwa na Meneja Msaidizi Kitengo cha Huduma za Kifedha kwa Taasisi Maalum kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Omary Msuya wakati akitoa elimu ya sheria ya fedha za kigeni kwa wafanyabiashara katika Kata ya Sirari iliyopo nchini mpakani mwa Tanzania na nchi jirani ya Kenya.

   
   Meneja Msaidizi Kitengo cha Huduma za Kifedha kwa Taasisi Maalum, Omary Msuya.

Elimu hiyo ya sheria ya fedha za kigeni ilitolewa Oktoba, 01,2023 katika ukumbi wa kituo cha Forodha Sirari ambapo baadhi ya wafanyabiashara na maafisa wa serikali wakiwamo wa Jeshi la Polisi wameshiriki na kupata mafunzo hayo.

Meneja Omary akielezea sheria hiyo pamoja na kanuni amesema kuwa biashara ya kubadili fedha za kigeni inahusisha kuuza na kununua fedha za kigeni na kupeleka  fedha nje kwa niaba ya wateja.

Omary akatoa mada ya utoaji wa Leseni na matakwa ya mtaji, matakwa ya utoaji wa Leseni ya Duka la kubadilisha fedha za kigeni lililoanzishwa na hoteli, usimamizi wa Duka la kubadili fedha za kigeni, uendeshaji wa Duka la kubadilisha fedha za kigeni pamoja na Taarifa za fedha na ukaguzi masharti ya jumla.

Wafanyabiashra wa mpakani Sirari na viongozi wa Serikali wakimsikiliza Meneja wa BoT wakati wakipatiwa elimu ya Sheria ya fedha za kigeni katika ukumbi wa forodha- Sirari.

" Biashara ya kubadilisha fedha za kigeni inahusisha fedha za kigeni, inahusisha kuuza na kununua fedha za kigeni na kupeleka fedha nje kwa niaba ya wateja.

" Biashara hii husimamiwa kutokana na yafuatayo; Ni sehemu nyeti katika sekta ya fedha, kuwezesha udhibiti wa fedha za kigeni, usitumiwe vibaya na wahalifu, kwa ajili ya Takwimu, kuhakikisha huduma za fedha za kigeni zinapatikana" Amesema Omary Msuya.

Isemavyo sheria ya fedha za kigeni 

Meneja huyo amesema biashara ya kubadilisha fedha za kigeni husimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania kwa mujibu wa sheria ya fedha za kigeni ya mwaka 1992.
             Omary Msuya

Amesema pamoja na mambo mengine, sheria imeipa benki kuu mamlaka ya kutunga kanuni za kusimamia biashara hiyo.

" Kifungua cha 5 (a) cha sheria ya fedha za kigeni ya 1992 inasema kwamba, Benki inaweza kuidhinisha uanzishaji wa Duka la kubadilisha fedha za kigeni kwa ajili ya kufanya biashara ya kununua na kuuza fedha za kigeni.

" Kifungua cha 6 cha sheria ya fedha za kigeni ya 1992 kinasema, Benki itakuwa na mamlaka ya kufanya kazi zote zinazohusiana na udhibiti wa usimamizi wa mambo yote ya fedha za kigeni" amesema.

Ameongeza " Kifungua cha 7(a) cha sheria ya fedha za kigeni ya 1992 inampa haki Gavana kuweza kuweka kanuni, miongozo na maelekezo yanayohusiana na mamlaka ya fedha za kigeni.

" Kwahiyo kanuni za usimamizi wa maduka ya fedha za kigeni ya 2023 zimewekwa kwa mujibu wa kifungu 5 (a) na 7 cha sheria ya fedha za kigeni ya 1992" Meneja BoT.

Utoaji wa Leseni na matakwa ya mtaji

Meneja wa BoT anasema kwamba kifungu cha 4;-(1) kinasema mtu hataruhusiwa kufanya biashara ya Duka ma kubadilisha fedha za kigeni bila kuwa na Leseni iliyotolewa na Benki.

" Vigezi 5 vya kuomba Leseni (a) Kampuni iliyosajiliwa Tanzania Bara au Tanzania Zanzibar, (b) Hoteli ya Nyota 3 au zaidi iliyosajiliwa Tanzania Bara au Tanzania Zanzibar" Amesema Meneja.

Anataja aina za Leseni kuwa ni Leseni Daraja A, inahusisha umiliki wa wasio watanzania na umiliki wa wazawa, Daraja B na Daraja C

Anasema Daraja A inawataka wale wasio watanzania wawe na mtaji wa Tsh. Bilioni moja na wazawa wawe na mtaji wa Tsh.Milioni 500. Leseni za Daraja A zitaruhusiwa kufungua matawu na kutyma fedha za kigeni kupitia wakala.

" Leseni ya Daraja B mtu anatakiwa kuwa na mtaji wa Tsh. Milioni 200.Haitafungua matawi wala kutuma fedha, na Leseni Daraja C mtaji ni ule wa hoteli" amesema.

Maombi ya Leseni

Meneja anasema mtu yeyote anayetaka kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni anatakiwa kupeleka maombi kwa maandishi Benk kuu ikiwa na mahitaji yaliyoainishwa kama mtu anayetaka kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni anatakiwa awe na jina la biashara linaloishia na kubadilisha fedha za kigeni.

Anasema maombi ya Leseni yatashughulikiwa na Benki kuu ndani ya mwezi mmoja baada ya nyaraka zinazohitajika kukamilishwa na muombaji na Benki itatoa idhini ya muda au kukataa ombi la Leseni.

" Idhini ya muda (Provisional Approval) haitachukuliwa kama Leseni ya kuanza kufanya biashara ya fedha za kigeni. BDC haitaanza biashara mpaka pale eneo lake la biashara, mifumo yake itakapokaguliwa na kuidhinishwa na Benki" amesema.

Ada ya mwaka na umiliki Daraja A, B

Omary amesema ada ya mwaka ni Tsh. 500,000 kwa kila tawi linaloendesha biashara.

Mabadiliko ya umiliki

Meneja huyo amesema kuwa mabadiliko ya umiliki wa duka la kubadilisha fedha za kigeni yanahitaji kupata idhini ya benki kuu, kisha mabadiliko yasajiliwe kwa msajili wa kampuni.

Uongozi BDC 

Amesema biashara ya duka la kubadilisha fedha za kigeni (BDC) inatakiwa kuwa na Bodi ya Wakurugenzi wawili au zaidi, BDC haitakiwi kumteua mtu yeyote kwenye nafasi ya Mtendaji mkuu au mkuu wa tawi bila idhini ya Benki kuu, kwa daraja C bodi ni ile ya hoteli.

Uendeshaji wa BDC

Meneja amesema hairuhusiwi kumruhusu mtu mwingine kufanya biashara ya fedha za kigeni katika eneo lake. BDC hairuhusiwi kuhamisha biashara kwenda eneo lingine bila idhini ya Benki kuu. BDC inayokusudia kufanya Biashara yake kwa muda mfupi au mrefu yatakiwa kupata ruhusa toka Benki kuu.


Amesema BDC hairuhusiwi kugawa miamala kwa nia ya kuepuka kutoa risiti na nyaraka isipokuwa pale tu fedha za kigeni hazipo, BDC hairuhusiwi kukataa kumuuzia mteja fedha za kigeni.

"BDC itahakikisha taswira na nyendo ndani ya eneo zinarekodiwa na kutunzwa kwa kipindi cha miezi 3. BDC yatakiwa kuonesha katika eneo lake la biashara tangazo kwa mteja ana haki ya kupewa risiti.

" BDC inatakiwa kuweka rekodi za miamala yote iliyofanyika katika biashara na kuitunza kwa kipindi kisichopungua miaka 10. Kabla ya kufanya huduma ya Money Transfer ( uhamisho wa pesa), BDC inatakiwa ipate nyaraka za uthibitisho za chanzo cha fedha." amesema.

Omary ameongeza kusema " BDC hairuhusiwi kumuuzia fedha za kigeni mtu asiye mkazi isipokuwa pale tu ambapo fedha za huyo zitapatikana kwa kuuza fedha za kigeni au kwa kazi halali aliyoifanya nchini.

Kanuni za Jumla

Meneja amesema kifungu cha 36 kinasema kama Benki itaridhika kwamba duka la kubadilisha fedha za kigeni (BDC) limekiuka kanuni hizi, yaweza kusimamisha BDC isifanye biashara kwa kipindi kisichozidi mwaka mmoja, kufuta Leseni ya BDC.

Pia kuitoza faini isiyozidi Dolla za USD 3,000, Leseni ya BDC yaweza kufutwa pale tu itakapobainika kuwa inapata fedha za kigeni kwa njia isiyo halali.

Katika Semina hiyo baadhi ya wafanyabiashara na maafisa wa Serikali walichangia mjadala na kuuliza maswali na kutoa maoni yao akiwemo Joseph Nyabaturi, Werema Tingo, Yohana Ibaru, Deus Magarya, George Mang'era na Luttha Tibilikirwa.

Mfanyabiashara wa nafaka na Hoteli Joseph Nyabaturi aliuliza iwapo ni sahihi wananchi waishio mpakani kununua bidhaa upande wa Sirare- Kenya na wakenya kununua bidhaa Sirari- Tanzania kwa matumizi binafsi ya familia yasiyo ya kibiashara, ambapo Meneja huyo alisema sio kosa ni ujirani mwema.

   Mfanyabiashara wa nafaka na Hoteli Joseph Nyabaturi

Afisa Biashara halmashauri ya Wilaya ya Tarime Abdalla Yusuf amependekeza itungwe sheria ya kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wenye mtaji wa Tsh. Milioni 30 nao waweze kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni.

Kamishna Msaidizi wa Polisi mkoa wa Polisi Tarime Rorya Amme AAA Anange alisisitiza wafanyabiashara wa fedha za kigeni kuangalia maeneo mazuri yenye usalama kuweka maduka yao ya biashara za fedha za kigeni.

        Kamishna Msaidizi wa Polisi mkoa wa Polisi Tarime Rorya Amme AAA Anange

Meneja Msaidizi wa Forodha Sirari Onesmal Rutohora amesisitiza wafanyabiashara kutoa Taarifa za fedha walizonazo pindi wanapotaka kuvuka mpaka.

Amesema fedha zinazotakiwa kutolewa Taarifa Forodhani hapo ni kiasi cha kuanzia fedha yenye thamani sawa na Dolla 10,000 ambapo anatakiwa kufika na kujaza fomu huduma ambayo ni bure kwamba kufanya hivyo kutasaidia kuepuka kusumbuliwa wawapo safarini nchi husika.

      Meneja Msaidizi wa Forodha Sirari Onesmal Rutohora

Meneja huyo alisisitiza wanaovuka mpaka kuwa wanaruhusiwa kutembea umbali wa km 15 pekee kutoka mpakani japo watu utembea km 18 hadi Tarime mjini na Km 22 kwenda Migori nchini Kenya. 

Hata hivyo washiriki wa semina hiyo wameipongeza Benki ya Tanzania kutoa elimu ya sheria ya fedha za kigeni huku wakiomba elimu hiyo iwe endelevu kwani watu wanawajibu wa kuelimishwa na kukumbushwa maswala mbalimbali ya sheria kwakuwa wengi wao hufanya makosa kwa kutofahamu sheria.

            Afisa Biashara halmashauri ya Wilaya ya Tarime Abdalla Yusuf 

          Afisa wa Polisi  Lutha Tibilikirwa akichangia mada

             Deus Magarya akichangia mada

                   Yohana Ibaru akichangia hoja

                Mfanyabiashara George Mang'era akichangia mada
              Jengo la Forodha Sirari


             Mfanyabiashara Werema Tingo




No comments