HEADER AD

HEADER AD

WANANCHI SIMIYU WATAKA HABARI ZA KUFICHUA MAOVU


Na Samwel Mwanga, Simiyu

WADAU wa Habari wamewataka Waandishi wa habari wa DIMA ONLINE kutumia vyema taaluma yao na kujikita katika habari za uchunguzi ili kufichua maovu katika jamii hali ambayo itasaidia serikali kufanya maamuzi sahihi.

Hayo yameelezwa kwa nyakati tofauti na maeneo mbalimbali  walipokuwa wakitoa Maoni yao juu ya habari zinazochapishwa na mtandao huo.

Wamesema kuwa licha ya mtandao huu kuripoti habari za matukio yanayotokea kila siku lakini bado kuripoti habari za uchunguzi hali ambayo imewafanya watu wengine kuanza kupoteza hamu ya kusoma .

Wamesema kuwa kwa sasa watu wanapenda kusoma habari ambazo zina uchambuzi wa kina kwani kwa sasa taarifa nyingi zinazoandikwa ni zile tayari zimeshaonekana kwenye mitandao ya mingine ya kijamii.

"Siku hizi mitandao ya kijamii ni mingi sana na inatoa taarifa au habari nyingi unaweza ukuona habari DIMA ONLINE baadaye utaziona kwenye mitandao mingine hapa sasa cha kufanya ni kuandika habari za kina za uchunguzi,"amesema Robert Urassa.

Wamesema kuna haja vyombo vya habari ikiwemo DIMA ONLINE sasa kuwekeza katika uandishi wa uchunguzi kwa kuwawezesha waandishi wa habari kusafiri mbali kwenda kuchokonoa mambo na kuja na habari zenye tija. 

“DIMA ONLINE ikitaka kufanya vizuri ni vizuri iwekeze kwenye habari za uchunguzi ni vizuri Waandishi waende maeneo mbalimbali wasafiri kwenda kufuatilia habari kwa kina hasa maeneo ya vijijini,"amesema Mhandisi Nandi Mathias.

Naye  Abel Mange Mkazi wa mjini Maswa anasema kuwa Kuna jambo haliko sawa na linalisababisha  kukosekana kwa habari za uchunguzi ni ukosefu wa ari kwa mwandishi wa habari.

“Zamani mwandishi wa habari za uchunguzi alikuwa anajivunia na hata ukimuona ana hadhi fulani. Lakini sasa hivi si kuandika hata anayetangaza, unaweza kuulizwa swali hadi wakati mwingine wewe unayeulizwa inabidi umsaidie kuuliza ili apate stori,” amesema.

Wameongeza kusema kuwa ni dhahiri kuwa kwa sasa watu wengi wanalalamika wakihoji ziko wapi habari za kiuchunguzi hata DIMA ONLINE hatuzioni isipokuwa tunakutana na habari za matukio ya kila siku tena ya maagizo ya viongozi tu.

"Tunahoji kwa DIMA ONLINE ziko wapi habari zenye mtiririko ambazo zimefanyiwa utafiti ili kesho unatafuta ili uendelee ilipoishia"amesema Lydia John ambaye ni Mwandishi wa habari.

Wamesema kuwa mkoa wa Simiyu unalima zao la pamba na kuna Wakulima unakuta mtu anapata fedha hadi karibu Milioni 20 akini utashangaa inapofika msimu wa kuandaa shamba hana hela ya kusafisha wala kuandalia sasa hebu tuchimbue tujue hawa hela wanapeleka wapi?

Imeelezwa kuwa habari za uchunguzi zikitafutwa nchini zipo na kwamba endapo waandishi wa habari wa DIMA ONLINE wakijikita zaidi kwenye habari za uchunguzi wataisaidia serikali kufanya maamuzi sahihi na chombo hicho kitaaminiwa na jamii na kupata matangazo ya biashara.

Mkurugenzi  Mtendaji wa DIMA ONLINE Rose Joseph Kimaro ameshukuru maoni yaliyotolewa na wananchi wa mkoa wa Simiyu na kusema kuwa yanasaidia kuijenga DIMA ONLINE.

" Tumejaribu kukusanya maoni kutoka kwa wananchi kupitia baadhi ya Waandishi wetu wa habari, lengo ilikuwa kujua wananchi wanahitaji vitu gani vya kihabari kupitia chombo hiki.

" Tumegundua kwamba wananchi wanatamani kuona stori za kufichua maovu hususani habari za uchunguzi. Tumepokea maoni yao na uongozi utayafanyia kazi kuhakikisha wananchi wanapata habari ambazo ni matamanio yao.

Amesema kuwa DIMA ONLINE ni chombo kimpya cha habari kilichoanzishwa Septemba 21,2022 hivyo bado hakijakuwa kiuchumi na hakijapata matangazo ambayo yatakiwezesha kujipatia fedha.

Amesema kuwa mkakati uliopo ni kutafuta vyanzo vya mapato ili ofisi iweze kujiendesha vyema ikiwa ni pamoja na kuwawezesha gharama za usafiri Waandishi wa habari kufika vijijini kuibua habari zilizofichika zikiwemo za kufichua maovu, za kuelimisha na kuburudisha.

No comments