HEADER AD

HEADER AD

CCM SIMIYU YARIDHISHWA UTEKELEZAJI MIRADI YA MAJI

 



Na Samwel Mwanga, Bariadi

KAMATI ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi(CCM)mkoa wa Simiyu imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya Maji inayofanywa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Simiyu.

Miradi hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 inayoelekeza ifikapo mwaka 2025 huduma ya upatikanaji wa maji vijijini kufikia asilimia 85.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed amesema hayo Novemba 25 mwaka huu baada ya kutembelea miradi ya maji ya Kijiji cha Lukale wilaya ya Meatu, mradi wa utafiti wa maji chini ya ardhi katika Kijiji cha Mwaswale wilaya ya Itilima na mradi wa Uchimbaji Bwawa na Kisima katika kijiji cha Lukale wilaya ya Meatu.

    Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed

Amesema RUWASA mkoa wa Simiyu imekuwa ikifanya kazi kubwa sana ya kusambaza maji kwa wananchi katika maeneo ya vijijini na miradi hiyo waliyoitembelea inatafsiri dhamira ya dhati ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.

Amesema kuwa miradi ya maji ni muhimu sana kwa wananchi hivyo inapaswa kukamilika kwa wakati ili iwanufaishe wananchi kwa kuzingatia ya kuwa maji hayana mbadala lakini changamoto zilizopo zinatokana na wakandarasi wanaopewa kazi ya kutekeleza miradi hiyo.

    Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsa Mohamed (kulia)akizungumza baada ya kukagua Mradi wa Maji katika Kijiji Cha Matongo wilaya ya Bariadi

“RUWASA mkoa wa Simiyu mnafanya vizuri sana katika miradi yenu na katika miradi hii tuliyoitembelea sisi wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM mkoa wa Simiyu tumerishwa nayo, Rais Dkt Samia Suluhu analeta fedha nyingi katika miradi ya miradi ya maji tunachotaka maji yafike kwa wananchi katika baadhi ya miradi tumeona Ruwasa mnaangushwa na hawa Wakandarasi.

“Wasimamieni hawa Wakandarasi na nikuagize Mkuu wa mkoa wa Simiyu Kaka yangu Dkt Yahaya Nawanda wale wakandarasi wanaotusumbua katika miradi yetu tunayowapa ndani ya mkoa ni kutowapatia kazi nyingine tena kwenye mkoa wetu maana wamekuwa wanatukwamisha kutokana na kutokamilika kwa miradi kwa wakati,”amesema.

Pia ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt Samia Suluhu kwa kuendelea kuleta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maeneo katika mkoa huo ikiwemo miradi ya maji.

       Tenki la kuhifadhi Maji katika Kijiji Cha Byuna wilaya ya Bariadi lililojengwa na Ruwasa

Aidha amewaomba wananchi ambao kwenye maeneo yao kuna miradi ya maji iliyojengwa na serikali au wadau wengine wa maendeleo kuinza na wasiihujumu  miundombinu yake kwani ni kwa ajili ya manufaa yao na wakumbuke maji hayana mbadala na pia miradi hiyo imekuwa ikitumia fedha nyingi katika kuijenga.

Wajumbe wa kamati ya siasa walipata taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo kwa nyakati tofauti tofauti kutoka kwa wasimamizi wa miradi hiyo ya maji ambao ni Mameneja wa Ruwasa wa wilaya.

Meneja wa Ruwasa wilaya ya Meatu, Mhandisi David Kaijage amesema kuwa utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa Bwawa na Kisima katika kijiji cha Lukale kilichoko Kata ya Bukundi umekamilika na utawanufaisha wakazi 2125 wa kijiji hicho.

       Meneja wa Ruwasa wilaya ya Meatu,Mhandisi David Kaijage(kushoto) akisoma taarifa ya Mradi wa Maji wa Kijiji Cha Lukale wilaya ya Meatu.

“Bwawa tulilochimba lina ujazo wa lita  4,200,000 ambalo litawezesha eneo la kisima kuwa na maji yasiyo na chumvi nay a kutosha na kisima kilichochimbwa kina urefu wa mita 20 za kufungwa pampu ya mkono,”amesema.

Amesema kuwa kwa wilaya hiyo hali ya upatikanaji wa maji maeneo ya vijijini ni asilimia 60.1 hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu na kwa sasa wanafanya kazi ya uboreshaji wa vyanzo vya maji katika maeneo ya Mwangwila, Mwabuzo, Mwabalebi, Mwamanimba na Isengwa na miradi mipya ya visima vimechimbwa katika kijiji cha Bulyashi na Mwamangongu na jumla ya tsh. Milioni 500 zinatarajia kutumika kazi miradi yote hiyo.

Naye Meneja wa RUWASA wilaya ya Itlima, Mhandisi Hussein Yahaya  amesema kuwa Mradi wa utafiti maji chini ya ardhi na uchimbaji wa kisima kirefu katika kijiji cha Mwaswale chenye urefu wa mita 100 umekamilika.
      Meneja wa Ruwasa wilaya ya Itilima, Mhandisi Hussein Yahaya(aliye kati)akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Mradi wa utafiti Maji chini ya Ardhi na Uchimbaji wa kisima kirefu katika Kijiji Cha Mwaswale kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM mkoa wa Simiyu.

Amesema lengo la mradi huo ni mpango wa muda mfupi ni kujenga mradi mdogo utakaotumia nishati ya jua na utakuwa na kituo kimoja cha kuchotea maji chenye jumla ya koki 10 na katika mwaka ujao wa fedha 2024/2025 watajenga mradi mkubwa wa maji ambao utahudumia vijiji vinne vya Mwaswale,Nkuyu,Ndolelezi na Gambasingu kwa gharama ya Sh milioni 100 .

Mhandisi Hussein amesema mradi huo utakapokamilika utawasaidia wananchi kupata maji safi na salama na kupunguza magonjwa yatokanayo na kutumia maji yasiyo salama na kupunguza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta maji badala yake kupata muda wa shughuli zingine za uzalishaji mali.

Meneja wa Ruwasa wilaya ya Bariadi, Mhandisi, Emmanuel Luswetula amesema kuwa mradi wa maji wa kijiji cha Matongo utagharimu kiasi cha Tsh. Milioni 528 na utawanufaisha wakazi 3200 wa kijiji hicho na ulipaswa kukamilika tangu Okotoba 30 mwaka huu lakini mkandarasi amechelewa hivyo utakamilika Mwishoni mwa mwezi Desemba.

        Meneja wa Ruwasa wilaya ya Bariadi,Mhandisi Emanuel Luswetura(wa kwanza kulia)akitoa taarifa ya Utekelezaji wa mradi wa Maji wa Kijiji Cha Byuna kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM mkoa wa Simiyu.

Pia amesema kuwa mradi wa maji wa Mwadobana katika kijiji cha Byuna utagharimu kiasi cha Sh Milioni 586 na tayari umeshaanza kutumika na wananchi wa eneo hilo wanapata maji safi na salama.

Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Dkt Yahaya Nawanda amemhakikishia Mwenyekiti wa CCM mkoa huo kuwa atasimamia fedha zote zinazoletwa na serikali kwenye mkoa huo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya maji ili ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa kwa manufaa ya wananchi.

“Nikuhakikishie Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, mimi mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt Yahaya Nawanda ndiye msimamizi mkuu wa miradi yote ya serikali ya mkoa huu najitolea kwa nguvu zangu zote kuhakikisha fedha yote inayoletwa na serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo inafanya kazi iliyokusudiwa,”amesema.

      Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Dkt Yahaya Nawanda(mwenye miwani) akizungumza kwenye Mradi wa Maji wa Matongo katika wilaya ya Bariadi na aliyeko kushoto ni Meneja wa Ruwasa wilaya ya Bariadi,Mhandisi Emmanuel Luswetura

        Tenki la kuhifadhi Maji katika Kijiji Cha Matongo wilaya ya Bariadi lililojengwa na Ruwasa

No comments