RC MARA AVUTIWA NA KAMPUNI YA RIN CO.LTD YA NYAMONGO KWA UTOAJI CSR
Na Dinna Maningo, Tarime
MKUU wa mkoa wa Mara Said Mtanda amevutiwa na kampuni ya ujenzi ya RIN CO. LTD ya Nyamongo, Wilayani Tarime mkoa wa Mara kwa kuchangia huduma mbalimbali za jamii.
RC Mtanda amempongeza Mfanyabiashara ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo ya RIN CO.LTD, Isack Charles Range kwamba amekuwa akipata zabuni katika Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara na kampuni yake imekuwa ikitekeleza uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR) na hivyo kuwa sehemu ya mchango mkubwa wa maendeleo kwa jamii wakiwemo wazawa.
Mkuu huyo wa mkoa ameyasema hayo Novemba,23, 2023 wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya uendeshaji biashara kwa wafanyabiashara wa mkoa wa Mara yaliyoandaliwa na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara yaliyotolewa na wawezeshaji kutoka Kampuni ya Impacten Afrika limited.
" Hizi semina ni muhimu sana zingatieni programu ya mafunzo itasaidia kupata uzoefu wa kufanya kazi na mgodi wa North Mara, itakusaidia kufanya kazi na wawekezaji wa nje. Tatizo sisi watanzania hatupendi mambo ya elimu tunapenda shotikati, tunapenda mambo ya harakaharaka mambo ya konakona.
" Nakupongeza RIN unatoaga CSR kule Nyamongo wewe unafanya kazi na mgodi kampuni yako inapata kazi mgodini lakini bado na kampuni yako inatoa CSR, pamoja na kwamba mgodi unatoa CSR na wewe kampuni yako inatoa CSR kazi nzuri" amesema Mtanda.
Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya ujenzi ya RIN CO. LTD amesema kwa mwaka 2022/2023 ametoa Tsh. Milioni 30 kama uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR) huku akiupongeza Mgodi wa North Mara kuendelea kumpa zabuni ambazo zimesaidia kampuni yake kuchangia maendeleo ndani ya jamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ujenzi ya RIN CO.LTD Isack Charles Range (katikati) akiwa ameketi na wafanyakazi wake wakati wakipata mafunzo ya uendeshaji biashara.
"Nina kampuni mbili ya ujenzi na ya usafirishaji, sisi wafanyabiashara tunafanya kazi na Mgodi, mnyonge mnyongeni haki yake mpeni kiukweli Mgodi wa North Mara umefanya mambo mengi sana, sisi wazawa tunaotoka mgodi wa North Mara ambao tunafanya kazi na mgodi tupo wengi na kampuni ni nyingi.
" Mgodi wa North Mara unatuwezesha makampuni kupitia kazi mbalimbali tunazofanya nao na sisi tunaajiri vijana ili wasiweze kwenda kuvamia mgodi, tunaajiri wazawa na wasio wazawa" amesema Range.
Ameongeza " Binafsi mimi lazima nisaidie jamii kwa sababu mimi ni kati ya waliosomeshwa na mgodi umenisomesha kutoka sekondari hadi chuo. Nimefanya kazi kwa miaka kumi sasa niliajiriwa na sasa nimejiajiri mwenyewe.
" Mkuu wa mkoa binafsi mgodi usingekuwepo sijui ningekuwa wapi kwasababu nategemea mgodi kwa asilimia 100 Mungu awabariki viongozi na mgodi, kwasababu wanapotupatia kazi makampuni na sisi tunasaidia ndugu zetu, niwaombe vijana wenzangu niwaambie CSR ni jambo la muhimu ukipata kidogo isaidie jamii " amesema Range.
Wakati huohuo, Range amemshukuru Mkuu wa mkoa wa Mara, wilaya na Mgodi kwa ushirikiano kuhakikisha wafanyabiashara wanapata elimu ya biashara.
" Nampongeza mkuu wa mkoa na serikali yake, mkuu wa wilaya na Mgodi kutuwezesha programu hii ya mafunzo ya kukuza biashara tumeifurahia lakini pia imetusaidia kutukutanisha pamoja kushirikiana na tumetambuana kuna watu walikuwa hawafahamu RIN ni nani leo mmenifahamu" amesema.
Mkurugenzi huyo amewashauri wafanyabisha ambao ndio wanaanza biashara kutafuta watu ambao wameshaendelea kibiashara wawashauri namna ya kufanya biashara zao huku akiwakaribisha ofisini kwakwe Nyangoto kwa ushauri.
Amemuhakikishia mkuu wa mkoa wa Mara kwamba ataendelea kuisaidia jamii na kutoa CSR pamoja na kufanyia kazi mafunzo waliyoyapata ya kukuza biashara yaliyotolewa na wakufunzi.
Post a Comment