DC KAMINYOGE ATAKA UHALISIA UTEKELEZAJI WA AFUA ZA LISHE MASWA
Na Samwel Mwanga,Maswa
MKUU wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aswege Kaminyoge amewaagiza Maafisa watendaji wa Kata katika wilaya hiyo kuhakikisha wanatekeleza kwa uhalisia afua za lishe katika maeneo yao ya kazi.
Dc Kaminyoge ametoa agizo hilo wakati wa kikao cha tathimini ya Mkataba wa Lishe ngazi ya Kata katika kipindi cha robo ya kwanza kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa wilaya na kuhudhuriwa na Maafisa Watendaji wa Kata 36 za wilaya hiyo pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya lishe ya Halmashauri ya wilaya ya Maswa.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge(aliyesimama)akifungua kikao Cha Kamati ya Tathimini ya Mkataba wa Lishe ngazi ya Kata katika Ukumbi wa Mkuu wa wilaya ya Maswa.Amesema kuwa Watendaji wote kuanzia ngazi ya juu ya serikali kwa maana ya Mawaziri,Wakuu wa Mikoa,Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri ,Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji wanapimwa katika utekelezaji wa afua za lishe kwa kuangalia matokeo halisi na si takwimu tu zilizoko kwenye makaratasi.
Amesema kuwa kila wanapokutana katika vikao hivyo vya tathimini kumekuwa na taarifa ambazo wanazipata juu ya utekelezaji wa Afua za lishe katika kila Kata lakini ni vizuri Watendaji hao wakajiridhisha kuliko kupokea hizo taarifa kutoka katika vijiji vilivyoko kwenye maeneo yao na kuziamini.
Baadhi ya Wajumbe wakiwa kikao Cha Tathimini ya Mkataba wa Lishe ngazi ya Kata katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu“Watendaji wa Kata fuatilieni taarifa mnazopewa kwenye maeneo yenu za Afua za lishe ambazo nanyi mmekuwa mkizileta wilayani ni vizuri mkajiridhisha na hizi takwimu zilizoko kwenye makaratasi iwe ni sehemu ya msingi ya kigezo au kiashiria cha utekelezaji lakini sisi watendaji tulio chini tufuatilie kilichoandikwa kama ni halisi.
“Tunatakiwa kuwa na matokeo yenye mashiko kwenye Afua za lishe hivyo ni lazima tumsaidie Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu kuhakikisha suala la lishe linatekelezeka kwa vitendo kwa kuona matokeo katika jamii,”Amesema.
Amesema ni lazima tujipime kwa kuangalia viashiria ambavyo ni pamoja na kuhakikisha Watoto chini ya miaka mitano wanapata vyakula vyenye virutubisho vinavyostahili, Wakinamama wajawazito wanapata virutubisho vinavyostahili vile madini joto pamoja na kuhudhuria kliniki.
Amesema kuwa ni lazima shule zote za Msingi na shule za Sekondari katika wilaya hiyo vinatoa chakula chenye virutubisho kwa wanafunzi kuanzia darasa la awali hadi sekondari huku akimpatia siku saba kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo,Maisha Mtipa kumpatia taarifa halisi ya utoaji wa chakula katika shule hizo.
Baadhi ya Wajumbe wakiwa kikao Cha Tathimini ya Mkataba wa Lishe ngazi ya Kata katika wilaya ya Maswa mkoa wa SimiyuNaye Shekhe wa wilaya ya Maswa,Issa Elias ambaye ni mjumbe wa kamati ya lishe katika halmashauri ya wilaya hiyo alisema ni vizuri mashamba ambayo yanamilikiwa na shule za msingi na sekondari katika wilaya ya Maswa yakalimwa mazao ya chakula kwa utaalamu kwa kuwatumia Maafisa Ugani ili shule ziweze kupata mazao ya kutosha ambayo yatatumika chakula kwa wanafunzi na hii itampunguzia mzigo mzazi kuchangia chakula cha wanafunzi shuleni.
“Haya mashamba ya shule yakilimwa kitaalam kwa kufuata kanuni bora za kilimo kwa kuelekezwa na maafisa ugani, nina amini shule zitapata mazao ya kutosha ya chakula ambayo yatatumika kumpatia chakula mwanafunzi awepo shule wakati wa masomo.
"Na hapo tutafanikiwa kutoa chakula kwa wanafunzi wote pia itampunguzia mzazi mzigo wa kuchangia chakula shuleni na hata kama atachangia mzigo mkubwa utakuwa umebebwa na shule,”amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa,Maisha Mtipa amesema kuwa suala la lishe ni agenda ya serikali tusipoisimamia vizuri itajenga jamii ambayo si nzuri katika ukuaji hivyo kwa kuwa tumesaini mikataba ya Afua za lishe ni vizuri kufanya vitu kwa uhalisia kwa kutoa takwimu sahihi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa(kulia)akufafanua jambo kwenye kikao Cha Tathimini ya Mkataba wa Lishe ngazi ya Kata na aliyeko upande wa kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge“Tutoe takwimu sahihi za afua za lishe na tufanye ufuatiliaji na kutoa taarifa zisizo sahihi ukumbuke vipo vyombo mbalimbali vya kufuatilia hizo taarifa ili kujua ukweli wake.
"Ukibainika umetoa taarifa ambazo si sahihi ni lazima tutakuchukulia hatua za kinidhamu,Mtendaji wa Kata ndiyo mkuu kwenye eneo lake hivyo taasisi zote zilizoko kwenye eneo la Kata ziko chini yake hivyo unapoletewa taarifa za lishe fuatilia ukajiridhishe na siyo kukaa ofisi tu,”amesema.
Awali Afisa Lishe wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa,Abel Gyunda amesema katika kipindi cha robo ya kwanza(Mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu) kadi alama bado inaonyesha rangi nyekundu kwa baadhi ya maeneo kwa Kata mbili za Busangi na Mwabaratulu katika shule zao ambazo zimekuwa hazitoi chakula kwa wanafunzi wanapokuwepo shuleni.
Post a Comment