HEADER AD

HEADER AD

DC SERENGETI, WANANCHI WASEMA UJENZI WA BARABARA YA LAMI UTARAHISISHA MAWASILIANO


Na Dinna Maningo, Serengeti

MKUU wa wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Dkt. Vincent Mashinji, Diwani wa Kata ya Nyansurura, Josephat Ryoba na wananchi wameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha fedha kujenga barabara ya Tarime- Mugumu kwa kiwango cha lami.

Mkuu huyo wa Wilaya ametoa pongezi hizo wakati Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania ( TANROADS) mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe  alipofika kijiji cha Nyansurura  kumkabidhi mkandarasi kampuni ya STECOL Corporation  ya China kujenga barabara ya Tarime - Mugumu kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 61.

     Mkuu wa wilaya ya Serengeti Dkt. Vincent Mashinji (kushoto) akizungumza wakati wa makabidhiano ya ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami itakayojengwa na kampuni ya China.

Serikali imetoa fedha Tsh. Bilioni 81.146  kwa ajili ya ujenzi huo itakayojengwa kwa kipindi cha miaka miwili ambapo kipande cha kutoka Jembe la Nyundo Tarime mjini hadi Mogabiri kina urefu wa (km 9.3) na kutoka Kwinogo - Nyamongo hadi Mugumu Serengeti ni (km 51.75).

Kipande kingine cha ujenzi wa barabara kutoka Mogabiri hadi Nyamongo chenye urefu wa (km) 25  kinachogharimu zaidi ya Tsh. Bilioni 34.6 ujenzi wake unaendelea, barabara inayojengwa na Kampuni ya ujenzi ya Nyanza Road Works Limited ya hapa nchini.

                       Barabara itakayojengwa kwa kiwango cha lami

DC Mashinji amesema " Wilaya zote zinatakiwa ziunganishwe kwa barabara za lami, serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu imejitahidi sana katika miradi kutoka Bunda kuna barabara ya lami inaajengwa kutoka Sanzate - Nata ujenzi unaendelea.

"Tulikuwa tumebaki kuungana na Tarime na Tayali serikali imeshampata mkandarasi kampuni ya kichina, TANROADS wamekuja kumkabidhi barabara ili aanze ujenzi kwa kiwango cha Lami, najua mtauliza vipi barabara ya Serengeti Ngorongoro?.

"Kwasababu kuna hifadhi ya Taifa kuna taratibu zake lakini mimi nachojua barabaraba yetu kutoka Natta - Tabora B na yenyewe iko kwenye mpango inafanyiwa upembuzi yakinifu, barabara yetu kutoka Rung'abure - Sirori simba kushikana na wilaya ya Butiama inafanyiwa upembuzi yakinifu.

" Kwahiyo wilaya yetu inaenda kuunganishiwa na barabara za lami, leo hii nafurahi sana namshukuru Rais Samia ametuheshimisha sana watu wa Serengeti sasa hata gari ndogo tutaanza kununua, barabara yetu inajengwa kwa kiwango cha lami.

Dkt. Vincent ameongeza kusema"  waliniambia tuunganishe kambi ya pamoja kule Tarime nikawauliza kwani barabara ni ya Tarime tu? si inajengwa hadi Serengeti? kwahiyo na Serengeti iwekwe kambi kwaajili ya mkandarasi na tunaomba ianzie kujengwa kuanzia Serengeti kwenda Tarime siyo Tarime -Serengeti" amesema.


Mkuu huyo wa wilaya amepiga marufuku mifugo kutembea barabarani pindi barabara ya lami itakapojengwa huku akiwasisitiza wananchi kulinda mali zote zitakazotumika katika ujenzi wa barabara.

"Barabara itakapojengwa sitaki kuona ng' ombe zinatembea barabarani, lengo la kujenga barabara ya lami ni kufanya Mawasiliano yawe ya haraka na vyombo vyetu vya moto vidumu.

         Wananchi wa Kijiji cha Nyansurura wakimsikiliza DC Dkt. Mashinji

" Kwahiyo hatutegemei kuona barabara inakuwa kijiwe matokeo yake zinatokea ajali tunaanza kuweka matuta, kwa wenzetu kule tulikozunguka barabara kubwa kama hii haiwekewi matuta, lakini kwenye nchi yetu tunalazimika  kuweka matuta kwasababu hatujui matumizi bora ya barabara" amesema.

Ameitaka kmpuni inayojenga barabara kutoa ajira kwa wakazi wa Serengeti " Hatutegemei mkandarasi atuletee vibarua kutoka mbali vibarua wote wawe wa hapahapa tunajua hakuna mkurya mvivu " amesema Dk. Mashinji.

               Wajenzi kutoka kampuni ya STECOL Corporation  ya China itakayojenga barabara ya lami Tarime- Mugumu

DC Mashinji amewataka wananchi kulinda mali za Serikali zilizopo karibu na makazi yao kwa kile alichosema kuwa miradi inayojengwa ni fedha za kodi za qananchi hivyo kitendo cha kuiba vifaa vya miradi ni kujiibia wao wenyewe na kurudisha nyuma maendelo yao.

Diwani wa Kata ya Nyansurura Joseph at Ryoba Seronga ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami huku akiwataka vijana kujitokeza pindi mkandarasi atakapohitaji vijana wa kufanya kazi.

         Diwani wa Kata ya Nyansurura Joseph at Ryoba Seronga

Joseph Chacha amesema kuwa barabara ya lami ni muhimu kwakuwa inatumiwa pia na watalii wanaokwenda kutalii Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Ameongeza kuwa barabara hiyo itasaidia kuchochea Utalii kwakuwa haitawachosha wasafiri ikilinganishwa na barabara iliyopo kwa sasa yenye vumbi ambayo wakati wa msimu wa mvua inaharibika na kuleta usumbufu kwa watumiaji wa barabara.

Mkazi wa Kijiji cha Nyansurura Feth Ogutu Naftari amesema barabara ikijengwa kwa lami itasaidia wananchi wakiwemo wafanyabiashara wanaopeleka mkaa, mahindi, limao, kukuu kuuza Nyamongo.

         Mkazi wa Kijiji cha Nyansurura Feth Ogutu Naftari.

" Nyamongo tunaenda kwa nauli ya sh. 4000-5000 ikijengwa kwa lami tuna hakika nauli itapungua, na tutaondokana na matope wakati wa mvua barabara inaukuwa mbovu" amesema.

Akikabidhi Barabara kwa mkandarasi, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania ( TANROADS) mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe amesema;

     Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania ( TANROADS) mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus  Maribe (Katikati  aliyevaa miwani) akizungumza

"Leo tumekuja kumkabidhi mkandarasi barabara ajenge kwa kiwango cha lami itajegwa na Kampuni ya STECOL Corporation ya China, kwa hiyo Serikali imeanza kazi na ujenzi utagharimu Bilioni 81.146" amesema Meneja.

Ameongeza " Barabara itajengwa kwa viwango vya upana wa barabara itakuwa mita 9.5 ambapo mita 6.5 ni kwa ajili ya magari kupita na Mita 1.5 ni kwa ajili ya watembea kwa miguu. Itajengwa kwa makaravati, madaraja, itakuwa na viwango vya lami nyepesi" amesema Mhandisi Vedastus.

Ilani ya CCM 

Ibara ya 50 ya Ilani ya Uchaguzi ya 2020- 2025 ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inasema Chama kinatambua umuhimu wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara, uchukuzi, mawasiliano kwa lengo la kuwezesha ujenzi wa uchumi imara unaojitegemea.

             Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hasani akionesha Ilani ya Uchaguzi ya CCM 

Pia manufaa ya sekta hii ni pamoja na Kuboresha maisha ya watanzania kwa kuwawezesha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, kuongezeka kwa matumizi ya fursa za kijiografia na mapato nchini.

Ibara ya 55 ya Ilani hiyo inasema Chama cha Mapinduzi kitaielekeza Serikali kuendeleza shughuli za ujenzi wa miundombinu mbalimbali ili kuifanya sekta ya ujenzi ifikie malengo yake ya kuwezesha wananchi kuendelea na uzalishaji kwa ajili ya kuongeza kipato chao.





No comments