HEADER AD

HEADER AD

KAMATI YA BUNGE YAKAGUA MITAMBO YA UZALISHAJI MAJI, RIDHIWANI KIKWETE ATIA NENO


Na Gustafu Haule, Pwani

KAMATI ya Bunge ya Uwekezaji na  Mitaji ya Umma pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge wamefanya ziara ya kutembelea na kukagua mitambo ya uzalishaji maji ya DAWASA iliyopo Wami  Chalinze Mkoani Pwani.

Katika ziara hiyo iliyofanyika Novemba 12 mwaka huu kamati hiyo iliambatana na viongozi wengine akiwemo Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete,Katibu Mkuu Wizara ya Maji Jamal Katundu ,Mkurugenzi Mkuu wa Dawasa Kiula Kingu,pamoja na baadhi ya watumishi wa Dawasa.

Wakiwa katika mitambo hiyo wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wao Deus Sangu ,walipokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa DAWASA Kiula Kingu na baadae kutembelea sehemu mbalimbali za uchakataji wa maji hayo.

       Mkurugenzi Mkuu wa DAWASA Kiula Kingu,akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji katika mtambo wa Wami uliopo Chalinze -Pwani kwa Kamati ya Bunge Uwekezaji na Mitaji ya Umma .

Kingu,amesema kuwa mradi wa maji Wami umetekelezwa kwa awamu tatu ambapo mpaka sasa umetumia zaidi ya bilioni 160 na kwamba tayari mpaka sasa wateja 7,687 wameunganishiwa maji huku kukiwa na vioski 800.

Kingu,amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kumetokana na juhudi za Serikali kutafuta fedha kutoka kwa wahisani mbalimbali na kwamba hali ya hupatikanaji maji kwasasa imekuwa na mafanikio makubwa.

Amesema,kwasasa DAWASA inaendelea na programu ya kutengeneza miundombinu ya Maji katika Jijini la Dar es Salaam ambapo tayari imetenga bilioni 55 na Chalinze imetengewa bilioni 1.5 kwa ajili ya usambazaji maji sehemu mbalimbali.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete ambaye pia mbunge wa Jimbo la Chalinze ameishukuru Serikali kwa namna ilivyojipanga kutekeleza mradi huo.


Kikwete ,amesema kuwa wakati anagombea ubunge katika Jimbo hilo mwaka 2014 mmoja wa wananchi alimletea  chupa ya maji machafu mezani na kwamba wananchi hao walisema watamchagua lakini kero yao kubwa ni maji.

Amesema kwasasa,anaishukuru kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwani ni moja ya sababu ambayo imefanya leo hii haulizwi suala la maji katika mikutano yake anayoifanya jimboni Chalinze kwakuwa changamoto hiyo imepatiwa majibu.

Aidha,Kikwete mbali na kuipongeza kamati hiyo lakini pia amesema anamshukuru Hayati Rais wa awamu ya tano John Pombe Magufuli kwa jitihada zake za kutoa pesa asilimia 30 sawa na Bilioni 7 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo lakini Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye aliyefanyakazi kubwa ya kutoa asilimia 70 ya fedha za kukamilisha mradi huo.

"Namshukuru Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan kwakufanyakazi kubwa ya kukamilisha mradi huu mkubwa wa maji kwani Chalinze sasa imetulia,Rais Samia ametoa asilimia 70 ya fedha zote za mradi huu na bado haitoshi akatoa agizo kwa Dawasa kutenga milioni 500 kwa ajili ya kusambaza maji katika nyumba za wananchi,hakika hiyo ni faraja kubwa,"amesema Kikwete.

Ameongeza kuwa,mafanikio ya Chalinze kupata maji ya kutosha imetokana na juhudi za DAWASA kwani wamefanyakazi kubwa ya kuokoa maisha ya watu wa Chalinze kwani mbali na Rais kuagiza kutoa milioni 500 lakini wao wakajiongeza na kutoa bilioni 1.3 za kusaidia kusambaza maji katika maeneo yote ya Chalinze na kwamba Chalinze kwasasa inapata maji kwa asilimia 88 .

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge,amesema Mkoa wa Pwani unahudumiwa na Ruwasa na Dawasa ambapo kwasasa Mkoa unapata maji kwa asilimia 86 na kwamba Dawasa wanafanyakazi nzuri  na yenye kuleta mfano wa taasisi nyingine.

Kunenge, amesema kuwa Dawasa wamepewa lengo la kuhakikisha maji yanapatikana kwa asilimia 85 na 95 ambapo ameomba Dawasa wapewe msaada zaidi ili waweze kufikia malengo kwakuwa idadi ya watu inaongezeka kila siku.

Kunenge,amesema kuwa Mkoa wa Pwani ni Mkoa wa Uwekezaji na huduma ya Maji ndio kipaumbele kikubwa na kwamba kwa juhudi anazoziona kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan changamoto ya maji Mkoa wa Pwani inakwenda kuisha na hivyo kuwapa fursa wawekezaji kuzalisha kwa wingi.

Kunenge,ameishauri kamati hiyo ya Bunge awasaidie Dawasa maana wanamipango mizuri ya kuboresha na kuimarisha mitambo ya maji na kwamba wanataka kuona mafanikio ya Dkt.Samia juu ya hupatikanaji wa maji Mkoa wa Pwani yanafikiwa kwa haraka zaidi.

Kwa upande Mwenyekiti wa kamati ya Bunge Uwekezaji na Mitaji ya Umma Deus Sangu,amesema lengo ya ziara hiyo ni kuona kama fedha zilizotolewa zimefanyakazi iliyokusudiwa lakini hatahivyo kamati imejiridhisha na kazi iliyofanyika.

    Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Uwekezaji na Mitaji ya Umma Deus Sangu

Sangu, ameishukuru Dawasa kwa kazi nzuri inayofanya na kwamba kati ya maazimio 14 ya kamati maazimio mawili yamelenga kuisaidia Dawasa ikiwemo pendekezo la kamati kutenga bilioni 48 ya deni kuwa mtaji pamoja na kuhakikisha taasisi zinazodaiwa na Dawasa zinalipa deni hilo haraka.

"Kamati imezielekeza taasisi zinazodaiwa na Dawasa kulipa madeni hayo kwa haraka kwani mpaka sasa bilioni 13 Dawasa inadai kutoka katika taasisi mbalimbali na kwamba kufanya hivyo itakuwa ni msaada mkubwa wa Dawasa kuweza kufanya shughuli zake bila vikwazo." amesema Sangu.

Hata hivyo,Sangu amepongeza juhudi za mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete kwa namna anavyotoa ushirikiano kwa taasisi ya Dawasa huku akisema kamati inajua umuhimu wa maji Mkoa wa Pwani kwani kuna viwanda zaidi ya 1500 na kwamba lazima kamati ihakikishe maji yanapatikana  kuimarisha Uwekezaji ndani ya mkoa.

Kamati ya Bunge Uwekezaji na Mitaji ya Umma ikikagua mitambo ya maji ya Wami iliyopo Chalinze Mkoani Pwani Novemba 12 mwaka huu.

No comments