HEADER AD

HEADER AD

JELA MIAKA 30 KWA KUBAKA MWANAFUNZI

 

Na Samwel Mwanga, Itilima

MAHAKAMA ya Wilaya ya Itilima katika mkoa wa Simiyu imemhukumu Jegi Msalenge(20) kwenda jela miaka 30 na kulipa fidia ya Sh 300,000 kwa Mhanga baada ya kupatikana na hatia ya Kubaka.

Akitoa hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Robert Kaanwa amesema kuwa ameridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka hivyo anamtia hatia mshtakiwa kwa kutenda kosa hilo na kumapatia adhabu hiyo.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya Taifa ya Mashtaka wilaya ya Itilima,Mkaguzi msaidizi wa Polisi,Vedastus wajanga kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Juni 15 na 28 mwaka huu katika kijiji cha Sagata.

Mwendesha Mashtaka huyo alizidi kuieleza mahakama hiyo kuwa katika siku hizo mshtakiwa akiwa katika kijiji hicho akichunga ng’ombe kwa ndugu yake alimbaka mhanga(jina linahifadhiwa)mwenye umri wa miaka 16 ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari na kumsababishia maumivu pamoja na ujauzito.

Amesema kuwa kwa kosa la kubaka ni  kinyume na kifungu cha 130(1)(2)e na 131(1) vya sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022. 

Amesema kuwa taarifa hizo zilifika katika kituo cha polisi wilaya ya Itilima Septemba 4 mwaka huu na Septemba 18 mwaka huu Mshtakiwa alifikishwa na kusomewa kosa lake na jumla ya mashahidi wane na kielelezo kimoja kilitolewa na upande wa mashtaka ili kuthibitisha kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.

Mara baada ya ushahidi huo kutolewa Mshtakiwa alijitetea mwenyewe lakini mahakama hiyo hiyo ilimtia hatia na hivyo upande wa mashitaka uliomba apewe adhabu kali ili liwe funzo kwake na jamii kwani matukio kama haya huacha kumbukumbu mbaya isiyo futika kirahisi katika maisha ya mhanga na maambukizi ya magonjwa ya zinaa na mhanga anaujauzito na mtoto anazaa na mtoto mwenzake.

Mshitakiwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwani ni mkosaji wa mara ya kwanza lakini Mahakama hiyo hiyo ilimtia hatia kutumikia adhabu kwa kosa la kubaka.


No comments