RC PWANI AWAAGIZA MA-DC, MA-DED KUFANYA UTAMBUZI MASHAMBA PORI
Na Gustafu Haule, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge,ametoa maagizo kwa Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanafanya utambuzi wa mashamba pori yasiyoendelezwa ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Kunenge, ametoa maagizo hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari uliowajumuisha Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya uliofanyika Mjini Kibaha kuhusu namna Serikali ilivyojipanga kukabiliana na migogoro ya ardhi.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya mkoa huo.Amesema kuwa mkoa wa Pwani bado kuna mashamba pori mengi na makubwa ambayo yametelekezwa na watu bila kuyafanyiakazi na hivyo kuathiri uzalishaji kwa watu wa Mkoa wa Pwani.
Amesema mbali na hilo wakati mwingine mashamba hayo yanatumika kama vichaka vya kufanyia matendo ya uhalifu jambo ambalo Serikali haiwezi kukubali hali hiyo iendelee.
Kunenge, ameongeza kuwa baada ya kufanya utambuzi huo hatua itakayofuata ni kuwaandikia barua wahusika wa mashamba hayo kwa ajili ya kujua kwanini wanamiliki mashamba bila ya kutumia.
Amesema baada ya hapo mwekezaji au mmiliki wa mashamba pori ambaye hatakuwa na sababu za msingi taarifa hizo zitawasilishwa kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ili aweze kufuta hati zao.
" Natoa agizo kwa Wakurugenzi,Wakuu wa Wilaya na watendaji wengine mliopo hapa kuhakikisha mnakwenda kufanya utambuzi kwa mashamba pori yasiyoendelezwa ili tuyapeleke kwa Rais kwa ajili ya kubatilishwa hatia zao ," amesema Kunenge.
Katika kikao hicho Kunenge amewaeleza waandishi wa habari kuwa Mkoa wa Pwani umekuwa na migogoro mingi ya ardhi lakini migogoro hiyo inasababishwa na watu kutokujua Sheria na wengine hufanya makusudi.
Amesema pamoja na kutokujua Sheria lakini haimaanishi hiwe sababu ya kuvamia mashamba ya watu na kwamba yeyote atakayebainika kuvamia maeneo ya watu atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha,katika mkutano huo Kunenge amesema kuwa pamoja na kufanya utambuzi wa mashamba pori lakini bado mkoa unaendelea na oparesheni ya kuwakamata madalali na matapeli wa ardhi kwakuwa ndio wanaosababisha migogoro hiyo.
Amesema,katika oparesheni iliyokuwa ikifanyika kwa muda mrefu tayari Serikali imewatia nguvuni watu 24 kwa ajili ya kuhojiwa huku akisema majukumu mengine yanafanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa ajili ya kupata taarifa sahihi za watu hao.
" Serikali ipo katika oparesheni ya kukamata madalali na matapeli wa ardhi na mpaka sasa tayari watu 24 wametiwa nguvuni na wengine tumewakabidhi Takukuru wanawafanyiakazi,kwahiyo Serikali ipo kazini na wale wote wanaohusika na utapeli huo watakamatwa,"amesema Kunenge.
Amewataka wale wote waliovamia maeneo ya watu au Serikali kinyume na utaratibu waondoke haraka kwakuwa hakutakuwa na huruma kwa mtu yeyote zaidi ya kufuata Sheria katika utatuzi wa migogoro hiyo.
Hatahivyo, Kunenge ametumia mkutano huo kuwaomba Waandishi wa habari kutumia taaluma yao kuwaelimisha wananchi na jamii kiujumla juu ya kuacha kuvamia mashamba yao watu na kwamba kwa kufanya hivyo anaamini migogoro hiyo itamalizika haraka.
Post a Comment