UNESCO YAKUTANA NA WADAU KUJADILI NYENZO ZA KUKABILIANA NA VITENDO VYA KIKATILI
Na Andrew Chale, Dar es Salaam
SHIRIKA la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa mataifa (UNESCO) limekutana na Wadau Wataalam kutoka mashirika yasiyo ya Kiserikali, serikali na mashirika ya watu wenye ulemavu.
Lengo la mkutano huo ni kupitia na kutoa maoni nyenzo za kukabiliana na vitendo vya kikatili na kinyanyasaji kwa wanafunzi walemavu wanaosoma vyuo vya ufundi hapa nchini.
Mkutano huo wa siku mbili uliofanyika Novemba 14- 15, 2023 Tanzania, pia unafanyika sambamba katika nchi zingine tatu za Namibia, Msumbiji na Zimbabwe kwa pamoja wakijadiliana kupitia video kwa mtandao wa ZOOM.
Mkutano huo ni mpango unaotekelezwa na UNESCO na shirika la kazi Duniani (ILO)kupitia mradi unaofadhiliwa na United Nations Partnership on the Rights of Persons with Disabilities (UNPRPD) wenye lengo la kukomesha unyanyapaa na ubaguzi wa watu wenye ulemavu katika vyuo vya ufundi na kazini.
Katika majadiliano hayo, wadau wametoa maoni yao na namna bora ya hatua za kuchukuliwa ili kufikiwa malengo, huku pia wakijifunza kutoka kwa wenzao wanchi za Msumbiji, Zimbabwe na Namibia.
Mkurugenzi wa Elimu maalumu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Magreth Matonya ameshukuru shirika la kimataifa la UNESCO na ILO kwa mkutano huo wa wadau namna bora ya kukabiliana na vitendo vya kikatili ambavyo vinaendelea katika vyuo vya ufundi vya Tanzania.
Amesema mkutano huo ni muhimu kwani tayari kuna nyenzo zimeandaliwa ambazo zitasaidia kupata taarifa mbalimbali za vitendo vya kikatili na kinyanyasi kwa watoto walemavu ambavyo vinafanyika kwenye vyuo hivyo.
“Nyenzo hii imetumika kupata taarifa mbalimbali kwenye vyuo vya ufundi nchini. Tumeijadili na tumeona ni muhimu kwani imeandaliwa vizuri.
"Pia italeta chachu namna bora ya kubaini ni aina gani ya vitendo vya kikatili ambavyo vinafanyika, lakini ni nani ambaye ni msababishi mkuu wa hivyo vitendo vya kikatili katika vyuo vya ufundi vya Tanzania.’’ Amesema Dk. Magreth Matonya.
Ameongeza kuwa Serikali iendelea kuwasaidia vijana wote wenye ulemavu vyuo vya ufundi ambao wanatakiwa kusoma na kuepuka changamoto za ukatili.
‘’Vijana wenye ulemavu wanahitaji kusoma, wanapokutana na changamoto ya vitendo vya kikatili wanapata msongo wa mawazo kiasi kwamba hawawezi kusoma na kufanikiwa ili watimize ndoto zao.
"Lakini pia wanapata msongo wa mawazo kutoka kwenye jamii, kutoka kwenye familia, lakini upande wa mfumo wa vyuoni, wanapata msongo wa mawazo kutoka kwa Wanafunzi pamoja na Walimu kwani mpaka sasa wapo baadhi yao bado hawajawatambua wenye ulemavu, hivyo nyenzo hii inakuja kusaidia na muhimu zaidi.’’ Amesema Dk. Magreth Matonya.
Mshiriki kutoka (NACTVET) Taasisi ambayo inasimamia vyuo hapa nchini, Eligius Bwalya, ambaye ana ulemavu wa aina mbili unaohusisha viungo na macho.
Amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwani wameweza kubainisha vitu mbalimbali ilikuweza kuchukuliwa hatua za haraka katika kumsaidia kijana mwenye ulemavu yakiwemo masuala ya kuomba usajili wa vyuo ama kazi pamoja na matangazo mengi yanawabagua walemavu.
‘’Kuna shida katika masuala ya matangazo ama katika masuala ya kutuma maombi yawe ya kazi ama kujiunga na vyuo ama shule.
"Matangazo haya yanawatenga walemavu ikiwemo mfano kujiunga na vyuo muombaji anawez kushindwa kufanya vizuri katika kujaza maoni yake mtandaoni ipo mifumo ambayo sio rafiki hali ambayo inaweza muombaji kujaziwa uongo.
"Lakini pia mfano unakuta matangazo haya yanaweka masharti fulani fulani ambayo yanawatenga walemavu, ama unakuta baadhi ya matangazo hasa ya kwenye televisheni mwanzo limeanza vizuri muombaji awe na sifa hii na zile.
" lakini kule mwishoni linamalizia kwa maoni zaidi wasiliana na mawasiliano yanayopita chini’’ hii inatenga walemavu hasa wasioona nchini hivyo, ameomba namna ya kuona hatua za kuchukuliwa ilikuwa katika usawa pande zote.’’ Amesema Eligius Bwalya.
Aidha, Wadau hao kwa pamoja na wenzao kutoka nchi za Zimbabwe, Msumbiji, Namibia wameweza kutoa maoni yao kwa kila nchi kuona jinsi ya kupata hatua sahihi za kuwasaidia walemavu katika vyuo vya ufundi.
Post a Comment