TIBA YA KIFUA KIKUU INAVYO WACHANGANYA WANANCHI
>> Wengine waamini tiba ya kifua kikuu uhakika wa kupona ni hospitali pekee
>>Wengine wasema tiba ya kifua kikuu suluhisho ni kupata tiba kwa waganga wa Jadi
>>Wataalam wa afya wasema hakuna utafiti uliothibitisha kisayansi kuwa waganga wa tiba za Jadi wanaweza kutibu ugonjwa wa TB
>> Waganga wa Jadi wataka tiba zao zisibezwe wakisema kuna magonjwa mengi wanasaidia baada ya hospitali kushindwa
Na Daniel Limbe, Geita
MJADALA wa tiba ipi inafaa kutumika kutibu ugonjwa wa kifua kikuu kwa jamii, umeendelea kusumbua vichwa vya baadhi ya wadau wa masuala ya afya,wagonjwa,wananchi na hata waganga wa tiba asili.
Hadi sasa,Tanzania haijawa na lugha moja katika matibabu ya kifua kikuu(TB) hasa kwa wananchi waishio vijijini kutokana na baadhi ya wagonjwa kutibiwa kwenye vituo rasmi vya kutolea huduma za afya na baadhi yao kwenda kwa waganga wa jadi.
Mkanganyiko huu umekuwa ukiwapa shida wadau wengi wa masuala ya afya kutokana na kukosekana kwa kauli moja yenye uhakika wa matibabu sahihi ya ugonjwa huo.
Baadhi yao wanasema umefika wakati wa serikali kuja na kauli moja ya matibabu sahihi ya kifua kikuu, na kuweka mkazo mkubwa ili kuhakikisha inapambana kikamilifu kuondoa tatizo la ugonjwa huo kwenye jamii kwa kuwa inawezekana.
Kwa kuachwa matibabu ya aina mbili yaendelee kutumika,wagonjwa na familia zao ndiyo wenye kuathirika zaidi kutokana na kutumia raslimali nyingi ili kunusuru maisha ya wagonjwa pasipo mafanikio,jambo linalosababisha kufirisika na kubaki maskini wa kutupwa.
Baadhi ya dawa za waganga wa tiba asili zikiwa zimeandaliwa kwaajili ya tiba kwa wagonjwa.
Baadhi ya familia zimetumia muda mwingi kuuguza wagonjwa kuliko kutumia muda huo katika uzalishaji mali, ambapo baadhi yao huanza kuwachukia wagonjwa na kuwanyanyapaa badala ya kuwajali, kuwapenda na kuwathamini.
Kwa sababu hiyo,wadau wa masuala ya afya wanasema nusura pekee ya TB nchini ni serikali kuja na mkakati kabambe wa kuwaonya waganga wa tiba asili kutojihusisha na matibabu ya ugonjwa huo, badala yake wagonjwa wote waelekezwe kwenye hospitali ili kupata matibabu sahihi.
Kutotibiwa kwa usahihi, husababisha kukomaa kwa ugonjwa (Usugu) jambo ambalo wagonjwa hulazimika kupata matibabu ya takribani miaka miwili badala ya miezi sita.
Uamuzi wa matibabu hayo kufanywa na serikali pekee utasaidia kujua ukubwa halisi wa tatizo hilo,kuweka mpango mkakati ulio bora kwa kushirikiana na wadau wengine wa afya ikiwa ni pamoja na kuongeza jitihada za ufuatiliaji, vipimo na tiba kwenye makundi hatarishi.
Shuhuda wa Ugonjwa wa TB
Makala hii imejikita zaidi kuangazia mgongano wa tiba sahihi ya ugonjwa wa kifua kikuu kwenye wilaya ya Chato mkoani Geita kutokana na baadhi ya waganga wa Jadi kuaminisha wagonjwa kuwa wanayo tiba ya ugonjwa huo.
James Mojjo, mkazi wa kijiji cha Muungano ni miongoni mwa watu waliotibiwa ugonjwa wa kifua kikuu kwenye hospitali ya wilaya ya Chato na kupona, ambapo anatoa ushuhuda kuwa tiba sahihi ya ugonjwa huo ni hospitali pekee.
Anadai kabla ya kubaini tatizo hilo, alitumia fedha nyingi kupata tiba isiyo sahihi mpaka pale ndugu zake walipoamua kumfanyia vipimo kwenye hospitali kisha kugundulika kuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa TB.
"Mwili wangu ulidhoofika sana, kilo zilipungua mpaka baadhi ya watu wakahisi nina Ukimwi, nilikuwa nikikohoa sana kiasi kwamba hata majirani walitambua kuna mgonjwa maana kikohozi hakina siri.
"Lakini baada ya kuanza matibabu takribani wiki moja tu kikohozi kilikatika na nikaanza kupumua vizuri japo ilinichukua miezi sita mpaka kupona lakini ningepelekwa kwa waganga wa jadi huenda sasa ningekuwa marehemu" anasema Mojjo.
Susan Lutobeka (siyo jina halisi) anasema unyanyapaa kwa watu waliougua kifua kikuu ni mkubwa sana jambo linalochangia wagonjwa wengi kukata tamaa na wengine kutamani kujiua.
"Mimi kabla sijatambua kama ni mwathirika wa VVU niliteseka sana kwa kuamini kuwa nimelogwa na ndugu zangu waliamini hivyo, tulitumia pesa nyingi sana kwa waganga wa Jadi pasipo mafanikio baada ya kupelekwa hospitalini niligundulika kuwa nina maambukizi ya virusi vya Ukimwi pamoja na kifua kikuu.
"Kwa kipindi nilichokuwa bado mgonjwa hata majirani zangu walikuwa wakiogopa kuja kunisalimia kutokana na kikohozi kikavu nilichokuwa nakohoa mara kwa mara.
"Hata hivyo namshukuru sana Mungu baada ya matibabu ya miezi 6 mfululizo nilipona kabisa TB na sasa ninaendelea na dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi" anasema Lutobeka.
Grace William, mkazi wa kijiji cha Kibehe anasema amewahi kumhudumia mdogo wake aliyeugua kifua kikuu na kwamba jamii yake ilionekana kumnyanyapaa kwa kuamini anaishi na mtu mwenye VVU, lakini ilimbidi kukabiliana na hali hiyo mpaka nduguye alipotibiwa na kupona.
Licha ya nduguye kutibiwa hospitali, bado anaamini waganga wa Jadi wanaweza kutibu kwa kuwa hata magonjwa mengine hushindikana hospitali na suluhisho kupatikana kwenye tiba za asili.
"Ninachokiamini mimi ni kuwa kila ugonjwa una dawa yake, na mwenyezi Mungu anaamua dawa hiyo amfunulie nani haijarishi ni wataalamu wa hospitali au wale wa Jadi, ndiyo maana kuna magonjwa yanashindikana hospitali lakini yanapona kwenye tiba mbadala" anasema Grace.
Kauli za waganga wa Jadi
Cloud Ngelela (mtoa huduma tiba mbadala) anasema licha ya kwamba hospitali zinatibu kifua kikuu, bado huwezi kubeza tiba zinazotolewa na waganga wa jadi kwa kuwa kuna magonjwa mengi wanasaidia baada hospitali kushindwa.
"Mimi kifua kikuu ninatibu na wagonjwa wangu wanapona kabisa maana kila ugonjwa huwa una tiba yake na unapoupatia dawa sahihi lazima utakwisha, ila usipoupatia unaweza kusababisha usugu na hata kifo.
"Kwanza ni muhimu ujue kuwa hata hizo tiba zilizopo hospitalini nyingi zinatokana na miti au mimea ambapo pia waganga wa tiba asili tunatumia miti iliyotoa matokeo mazuri kwa wagonjwa mbalimbali" anasema Cloud.
Anasema tofauti ya wataalam wa afya na wale wa asili (kienyeji) ni elimu ya darasani ambayo hutolewa kuwajengea uwezo wa kutambua magonjwa na tiba zinazoweza kusaidia binadamu kwa kutumia dawa zilizotengenezwa kitaalam ukilinganisha na wao ambao baadhi yao hupata maelekezo ya tiba kutoka kwenye mizimu ya mababu zao kupitia ndoto.
"Kwanza tuelewane kuwa sisi elimu yetu ni ya asili tunasikiliza historia ya mgonjwa pamoja na dalili anazokuja nazo kisha tunampatia dawa zetu ambazo tumechimba na kuziandaa sisi wenyewe kulingana na uzoefu wa magonjwa na wakati mwingine tunavyopewa maelekezo na mababu zetu waliotangulia mbele za haki kitambo kupitia ndoto (Mizimu)" anasema Cloud .
Masunga Kisena (Mganga wa Jadi) anasema hakuna ugonjwa usiotibika kwenye tiba za jadi, isipokuwa baadhi ya viongozi wa umma wamekuwa na tabia ya kubeza tiba za Jadi na kuendekeza za kizungu kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa kwenye vituo vya kutolea tiba.
"Ukweli ni kwamba sisi kwenye Jadi tunatibu magonjwa karibu yote isipokuwa tumekuwa na tabia ya kutubezwa tu na baadhi ya viongozi wenye kujipatia maslahi yao binafsi kutoka kwenye tiba za kizungu, kwanini usijiulize mwenyewe kuwa magonjwa yanayowashinda wao wakija kwetu wagonjwa wanapona?" anahoji Masunga.
Hata hivyo anasema serikali inapaswa kushirikiana na viongozi wa vyama vya waganga wa Jadi ili kuwabaini waganga wasio na sifa ambao huwarubuni wagonjwa kwa tamaa ya fedha wakati wakijua wazi kuwa hawana tiba za magonjwa husika badala ya kuwajumuisha waganga wote.
Kaimu Mwenyekiti Waganga wa Jadi wilaya ya Chato, Juma Masanja, anapingana vikali na tiba inayotolewa na baadhi ya waganga hao kuhusiana na ugonjwa wa TB, na kwamba wanachoweza kutibu ni kifua cha kubana (Pumu).
"Ni kweli wapo baadhi ya waganga wa Jadi wanaodanganya kutibu kifua kikuu, ugonjwa huo hautibiki kwa Jadi isipokuwa hospitalini pekee nitumie fursa hii kuwasihi waganga wenzangu kujiepusha na tamaa ya fedha toka kwa wagonjwa ili kusaidia jitihada za serikali kutokomeza ugonjwa huo".
"Changamoto ninayoiona kwa waganga wenzangu ni kushindwa kutofautisha ugonjwa wa Pumu na kifua kikuu naamini baadhi ya waganga wa tiba asili wana uwezo mzuri wa kutibu ugonjwa wa Pumu lakini siyo kifua kikuu" anasema Juma.
Kwa mantiki hiyo, ipo haja ya kuendelea kutolewa elimu kwa waganga wa tiba za asili katika mkakati wa kutokomeza kifua kikuu nchini na kwamba ili kufikia malengo tarajiwa makundi hayo yanapaswa kunena lugha moja ya tiba sahihi ya ugonjwa huo.
Mpango mkakati wa Halmashauri
Kutokana na hali hiyo, Mganga mkuu wa wilaya ya Chato Dkt. Eugen Rutaisire, anaelezea mikakati waliyonayo kukabiliana na tatizo la ugonjwa wa kifua Kikuu wilayani humo kuwa ni kwenda maeneo ya migodi na mikusanyiko ya watu ili kutoa elimu na upimaji.
Anasema mikakati mingine ni kuzifuatilia kwa ukaribu familia zilizogundulika kuwa na mgonjwa wa TB ili kujiridhisha kama hawajaambukizwa na ambao tayari wana vimelea wanaanzishiwa matibabu haraka.
"Tunaendelea na mapambano ya kudhibiti ugonjwa huo, tunapompata mgonjwa wa kifua kikuu tunahakikisha tunafuatilia na ndugu anaoishi nao ili kujiridhisha iwapo amesha waambukiza au bado, wakiwa hawajaambukizwa tunawaelimisha namna ya kuishi na walioambukizwa.
" Vile vile kuwarejesha waliopotea kwenye matibabu, kusafirisha sampuli kutoka zahanati zisizo na huduma ya upimaji na kuzipeleka vituo vyenye huduma, sambamba na kutoa elimu kwenye makanisa, misikiti, vilabu vya pombe, misiba, mikutano ya kisiasa na kiserikali pamoja na vikao vya waganga wa tiba asili" anasema Dkt. Eugen.
Anasema mkakati huo unatekelezwa kwa kushirikiana na watoa huduma ngazi ya jamii ambao wamepewa mafunzo ya kugundua dalili za mtu mwenye kifua kikuu, na kwamba wana stadi bora za kuongea na wahisiwa ili kuwasogeza kwenye vituo vya kutolea huduma za uchunguzi na matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa za maambukizi ya ugonjwa wa TB mkoa wa Geita kwa mwaka 2022/23, wagonjwa 4,112 walibainiwa kati 4,225 waliotarajiwa kufikiwa.
Aidha wilaya ya Chato imeshika nafasi ya pili kwa idadi ya wagonjwa wa Kifua Kikuu (TB) baada ya kuwafikia walengwa 806 kati ya 922 waliotarajiwa huku wilaya ya Bukombe ikitajwa kuongoza kati ya wilaya tano za mkoa huo.
Wilaya hizo ni Bukombe,Chato,
Nyang'hwale,Mbongwe na Geita.
Ikumbukwe kuwa ugonjwa wa TB unashika nafasi ya tatu kwa kusababisha vifo kwa jamii ya kitanzania, ukitanguliwa na Malaria pamoja na Upungufu wa kinga mwilini (Ukimwi).
Mratibu wa Kifua kikuu na Ukoma mkoani mkoani Geita, Dkt. Michael Mashala, anasema hakuna utafiti uliothibitika kisayansi unaoonyesha kuwa waganga wa tiba za Jadi wanaweza kutibu ugonjwa wa TB na kwamba ugonjwa huo hutibiwa hospitali pekee.
"Changamoto kubwa iliyopo kwenye jamii yetu ni kuaminishwa kuwa mtu anayekohoa kwa muda mrefu na kupungua uzito haraka anakuwa amelogwa kwahiyo baadhi ya wagonjwa wa TB hukimbilia kwa waganga wa Jadi kupata huduma za afya wakiamini wamelogwa jambo linaloathiri jitihada za serikali kutokomeza ugonjwa huo" anasema Dkt Michael.
Kadhalika mazingira ya tiba za Jadi ni moja ya sababu zinazochangia kuenea kwa ugonjwa wa kifua kikuu kutokana na msongamano wa wagonjwa kwenye nyumba zisizokuwa na hewa ya kutosha ambapo mgonjwa mmoja wa TB anaweza kuambukiza watu zaidi ya 20 iwapo atakohoa katika msongamano huo.
Sababu zingine ni pamoja na shughuli mbalimbali za kijamii zinazoathili afya ya mapafu ikiwemo vumbi linalotokana na uchimbaji mdogo wa madini,uvutaji wa sigara,bangi,shinikizo la damu,kansa na Ukimwi.
Dkt. Michael anasema mbali na sababu hizo, ipo haja kubwa kwa waganga wa tiba za Jadi kuacha kuwarubuni wagonjwa wa kifua kikuu kwa lengo la kujipatia fedha, badala yake wanapaswa kuwaeleza ukweli kuwa ugonjwa huo hutibiwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya serikali.
"Licha ya uwepo makundi mbalimbali ambayo huchochea maambukizi ya TB mkoani hapa, kundi la waganga wa tiba asili bado linaonekana kikwazo katika mpango mkakati wa serikali kukabiliana na ugonjwa huo.
"Katika harakati zetu kufuatilia wagonjwa wa TB mkoani hapa tulibaini mmoja wa waganga wa tiba asili (jina limehifadhiwa) akiwa ameambukizwa kifua kikuu sugu yeye na wake zake wawili, wakati wakiendelea kumtibu mgonjwa wao pasipo kujua" anasema Dk. Michael.
Aidha anaitaka jamii kujiepusha na misongamano isiyokuwa ya lazima kwa sababu ugonjwa huo huambukizwa kwa njia ya hewa,na kwamba wanaendelea kuishauri serikali kuboresha mazingira ya magereza na mahabusu za polisi ili kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa mkoani humo.
"Mpango mkakati wetu kama mkoa ni kuhakikisha watu wote wanaohofiwa kuwa na kifua kikuu tunawafuatilia na kuwapima ili ikithibitika tuwaanzishie matibabu haraka, njia hii imetusaidia sana kuendelea kuwabaini na kuwahudumia wagonjwa hao" anasema.
Anaongeza kusema kwamba, wanaendelea kuwaelimisha waganga wa tiba asili, kuacha kuwarubuni watu kwa magonjwa wasiyoweza kuyatibu badala yake wawahimize kuja hospitalini kwaajili ya matibabu yenye uhakika ili kupunguza vifo visivyokuwa vya lazima.
"Niwatake wananchi wote kuungana na serikali katika kudhibiti maambukizi mapya ya TB waache kuwaficha wagonjwa bali wachukue hatua za haraka kuwapeleka hospitali maana tiba zetu ni zenye uhakika na salama zaidi" anasema Michael.
Ripoti ya Mwaka 2018
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, kupitia mpango wa Taifa wa kudhibiti Kifua kikuu na Ukoma, toleo la mwaka 2018, Kabla ya julai 2016 tiba ya kifua kikuu ilikuwa inatolewa katika hospitali ya Kibong'oto iliyopo Siha mkoani Kilimanjaro inaeleza kuwa;
Mgonjwa alitakiwa kulazwa kwa kipindi cha miezi sita hadi nane kwa matibabu ya awali na baadaye kuruhusiwa kuendelea na matibabu ya mwendelezo kwenye kituo kilicho karibu na nyumbani kwake kwa miezi 12.
Hata hivyo, kwa kutambua umuhimu wa kusogeza huduma za matibabu karibu na jamii, serikali iliamua kugatua huduma hizo kwenda kwenye hospitali za rufaa za kanda,Mikoa na nyinginezo ambazo zilikidhi vigezo baada ya kufanyiwa tathmini kwa lengo la kuhakikisha ugonjwa wa kifua kikuu sugu unatokomezwa nchini.
Kadhalika Shirika la afya duniani(WHO) lilitoa mapendekezo ya kutumika kwa tiba ya kifua kikuu sugu ya muda mfupi ambayo imeonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuponya ukilinganisha na awali.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa matibabu ya ugonjwa huo yamegawanyika awamu mbili yakiwemo ya awali ambayo huchukua miezi minne hadi sita na mwendelezo wake huchukua miezi mitano,huku muda wa matibabu yote ukitajwa kuwa miezi tisa hadi 11.
Pia ili mgonjwa apate tiba ya muda mfupi lazima asiwe na miongoni mwa viashiria vya kifua kikuu sugu zaidi ( XDR TB) ikiwa ni pamoja na usugu wa dawa za Quinolone au sindano ambazo ni dawa za kutibu kifua kikuu sugu.
Asiwe amewahi kutumia dawa za kifua kikuu sugu kwa kipindi cha mwezi mmoja au zaidi na asiwe na mzio au kushindwa kuvumilia dawa zinazotumika kwa tiba ya muda mfupi.
Vile vile inashauriwa asiwe mjamzito,na asiwe na TB ya nje ya mapafu ambayo ni kali mfano ile ya ubongo na ya mifupa.
Hali kadhalika Dawa mpya za kifua kikuu sugu aina ya "Bedaquiline na Delamanid" zimetajwa kuwa na uwezo mkubwa zaidi ya kuponya kifua kikuu,na kifua kikuu sugu kwa kipindi cha miezi sita pekee licha ya wenye kifua kikuu sugu kushauriwa kuendelea kutumia dawa zingine kwa matibabu ya miezi 20 hadi 24 ili kupona kabisa.
Kauli ya Wizara ya Afya
Hivi karibuni kwenye mkutano mkuu wa 78 wa Umoja wa mataifa ulioketi hapa nchini, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alitoa rai kwa jumuiya za Kimataifa kushirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu kwa kuongeza nguvu zaidi katika kuutokomeza kabla ya mwaka 2030.
"Bado hakuna raslimali za kutosha kupambana na TB, tunaendelea kuhimiza wadau wa sekta ya afya kuunganisha nguvu za pamoja na kuwekeza zaidi kwenye raslimali, tafiti,teknolojia, vifaa na vifaa tiba".alisema Waziri Ummy.
Anasema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 duniani zenye watu wengi wenye maambukizi ya kifua kikuu ambapo takribani watu 70 hufariki dunia kila siku, hali inayoshusha nguvu kazi katika jamii pamoja na uchumi wa taifa kwa ujumla.
"Takwimu za mwaka 2021 zinaonyesha Kuwa Tanzania ilikuwa na watu 132,000 wanaougua ugonjwa wa kifua kikuu tumeweza kupunguza maambukizo mapya ya ugonjwa huo kwa aslimia 55 na serikali inaendelea na mapambano zaidi ili kuhakikisha tunautokomeza ifikapo mwaka 2030".
Waziri Ummy, anasema Tanzania imejitahidi sana kuwekeza nguvu kubwa kwenye utoaji wa tiba ya kifua kikuu pamoja na utoaji wa elimu ya afya ili jamii iweze kufahamu ugonjwa huo mapema kabla na baada ya kuugua sambamba na kupata matibabu sahihi.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa Mpango Mkakati Shirikishi wa Sekta ya Afya katika mapambano dhidi ya kifua kikuu uliozinduliwa mwezi machi 2023 utakaosaidia kuongoza katika jitihada za kuutokomeza ugonjwa huo nchini.
Nini kifanyike
Ili kuyafikia malengo ya serikali ya kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu nchini kabla ya mwaka 2030, serikali inashauriwa kuongeze jitihada za kuwafikia watu walio na maambukizi ya kifua kikuu hasa katika makundi yaliyopo hatarini zaidi.
Serikali itenge bajeti ya kutosha kuwawezesha wataalamu wa kifua kikuu nchini kutoa elimu sahihi ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Serikali ikutane na waganga wa tiba za asili kwa mashauriano na kujengeana uelewa mpana ili kuutekeleza kikamilifu mkakati madhubuti wa kutokomeza ugonjwa huo.
Viongozi wa dini na wale wa kisiasa watumie majukwaa yao kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi mapya ya ugonjwa wa TB badala ya kuiachia serikali pekee.
Vyombo vya habari na wanahabari walichukulie uzito unaopaswa suala la maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu kwa kuelimisha jamii namna bora ya kujilinda kabla na baada ya kuambukizwa.
Jamii ijiepushe na unyanyapaa pamoja na imani potofu za kuamini kulogwa (ushirikina) badala yake wagonjwa wapelekwe hospitali kwaajili ya vipimo na matibabu sahihi.
Jamii itambue kuwa ugonjwa wa kifua kikuu unatibika na kupona kabisa iwapo mgonjwa atafikishwa kwenye vituo vya kutolea tiba vilivyoidhinishwa na serikali.
Post a Comment