HEADER AD

HEADER AD

DC, WANANCHI WAFANYA USAFI HOSPITALI MASWA MAADHIMISHO MIAKA 62 YA UHURU


Na Samwel Mwanga, Maswa

MKUU wa wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu, Aswege Kaminyoge amewaongoza wakazi wa wilaya hiyo katika zoezi la upandaji wa miti na kufanya usafi katika eneo la Hospitali ya wilaya hiyo ikiwa ni maadhimisho ya sherehe za miaka 62 za Uhuru wa Tanzania Bara.

Akiwa katika zoezi la upandaji miti lililofanyika Desemba 9 mwaka huu amewataka wananchi  wa wilaya hiyo kudumisha umoja, upendo na mshikamano na  kuendelea kumuomba mwenyezi Mungu ili aendelee kuilinda amani tuliyonayo na kuishi kwa upendo tulionao kama waasisi walivyotuachia amani ya kweli katika nchi yetu.

      Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge akifanya usafi kwa kufyeka nyasi katika eneo la hospitali ya wilaya ya Maswa.

Amesema kuwa anaipongeza kamati ya maadalizi ya maadhimisho hiyo ya wilaya hiyo iliyoongozwa na Katibu Tawala wa wilaya ya Maswa,Athuman Kalaghe kwa kupanga kufanya shughuli hizo ambazo zina umuhimu mkubwa kwa wilaya hiyo na taifa kwa ujumla.

Dc Kaminyoge amesema kuwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anasisitiza suala la utunzaji wa mazingira na upandaji wa miti ili kurudisha Uoto wa asili ambao umetoweka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

      Baadhi ya Watumishi wa serikali katika wilaya ya Maswa waliojitokeza kufanya usafi na kupanda miti katika hospitali ya wilaya ya Maswa.

“Shughuli mojawapo ambayo leo tunaifanya hapa ya kupanda miti katika eneo hili la Hospitali ya wilaya ya Maswa ni kuunga mkono juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu la kuhakikisha tunapanda miti kwa wingi katika maeneo mbalimbali ili kuweza kuhifadhi mazingira  na kurudisha Uoto wa asili na wananchi waige na wawe na utamaduni wa kupanda miti,”amesema.

Akizungumzia suala la usafi amesema kuwa wameamua kufanya usafi kwenye hospitali hiyo na wananchi wengine kufanya usafi kwenye maeneo yao hasa kwa kuondoa takataka kwenye mitaro iliyoko kwenye makazi yao ili kuhakikisha katika kipindi hiki ambacho tumetahadharishwa kuwepo na mvua kubwa ili kuruhusu maji ya mvua kutozingira makazi ya watu.

       Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge (aliye mbele)akizungumza na watumishi wa serikali na wananchi waliojitokeza katika shughuli ya kufanya usafi na kupanda miti katika hospitali ya wilaya ya Maswa.

“Wananchi wa mji wa Maswa ambao kumejengwa barabara zilizo na mitaro ni vizuri tukafanya usafi wa mara kwa mara kwenye hiyo mitaro ili iweze kusafirisha maji ya mvua ambazo zinaendelea kunyesha ili tuweze kuzilinda nyumba zetu zisiweze kupatwa na mafuriko ya maji kwa tayari Mamlaka ya hali ya hewa imeshatoa tahadhari ya kuwepo kwa mvua nyingi katika baadhi ya mikoa na mkoa wa Simiyu ukiwemo,”amesema.

Aidha ameiagiza Wakala wa Barabara nchini(TANROAD)mkoa wa Simiyu na Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini(Tarura)wilaya ya Maswa kuhakikisha mitaro yote ambayo wanaijenga kwa sasa katika mji huo inakamilika haraka ili kuruhusu maji ya mvua yaliyokusanywa yanaelekea mahali ambapo yamekusudiwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa amewasisitiza watumishi wa halmashauri hiyo kufanya kazi kwa umoja, ushirikiano na nidhamu ya hali ya juu ili kufikia malengo yaliyowekwa na serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi.

        Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa,Maisha Mtipa akizungumza na watumishi wa serikali na wananchi waliojitokeza katika shughuli ya kufanya usafi na kupanda miti katika hospitali ya wilaya ya Maswa.

Amesema kuwa ni vizuri wanapopewa wito kujitokeza ili kufanukisha mipango ya serikali kama walivyojitokeza katika maadhimisho hayo na kufanya shughuli za usafi pamoja na kupanda miti katika eneo hilo la hospitali ya wilaya.

Aidha ametumia fursa hiyo kuwakumbusha kupanda miti katika maeneo yao kwa lengo la kutunza mazingira kwa kuzingatia halmashauri hiyo imekwisha kuanza kupanda miti kwenye taasisi za serikali zikiwemo shule za Msingi, shule za sekondari, Zahanati na Vituo vya afya.

“Nawashukuru wote ambao mmejitokeza katika zoezi hili la kufanya usafi na kupanda miti katika hospitali yetu ya wilaya na sisi tukapande miti kwenye maeneo yetu na tuwahamasishe wananchi wapande miti,sisi halmashauri tumekwisha kuanza kupanda miti katika taasisi zetu za serikali zikiwemo Shule za Msingi,Shule za Sekondari,Zahanati na Vituo vya Afya,”amesema.

    Watumishi wa serikali katika wilaya ya Maswa wakifanya usafi katika eneo la Hospitali ya Wilaya ya Maswa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru mwaka huu.

       Katibu Tawala wa Wilaya ya Maswa,Athuman Kalaghe akipanda mti katika eneo la hospitali ya wilaya ya Maswa.
 

    Watumishi wa serikali na wananchi wa wilaya ya Maswa wakilimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge(hayupo pichani)wakati wa shughuli ya upandaji wa miti na kufanya usafi katika hospitali ya wilaya ya Maswa.

      Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge akifanya usafi kwa kufyeka nyasi katika eneo la hospitali ya wilaya ya Maswa.

No comments