HEADER AD

HEADER AD

CHADEMA KAGERA KUANDAMANA KUSHINIKIZA SERIKALI MAREKEBISHO YA KATIBA, TOZO


>> Chama chasema kuna mambo hayaendi sawa

Na Alodia Babara, Bukoba

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA mkoani Kagera kimesema kinaungana na viongozi wa chama hicho Taifa juu ya maandamano yatakayofanyika Januari 24 mwaka huu.

Lengo la maandamano hayo ni kushinikiza Serikali kufanya marekebisho ya Katiba pamoja na kuitaka Serikali kupunguza kodi na tozo mbalimbali kwenye bidhaa ili kuondoa hali ngumu ya maisha kwa wananchi.

Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Kagera Mechardi Rwizire akizungumza na waandishi wa habari Januari 20, 2023 katika ofisi za chama hicho mkoa, amesema licha ya serikali kudai kuwa imewekeza fedha nyingi katika miradi ya maendeleo bado kuna mambo hayaendi sawa.

    Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Kagera Mechardi Rwizire akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali mkoani humo.

Rwizire amesema wanachama wa CHADEMA mkoa wa Kagera wanaunga mkono viongozi wao wa kitaifa kuhusu kuandamana ili kushinikiza Serikali kufanyia marekebisho miswada mbalimbali ya sheria pamoja na kupunguza kodi na tozo kwenye bidhaa mbalimbali ambazo zimekuwa zikipanda bei kila wakati na hivyo kusababisha hali ngumu ya maisha kwa wananchi.  

Sababu nyingine alizozitaja Mwenyekiti huyo ambazo zinahusu mkoa wa Kagera ni pamoja na maendeleo duni kwa wakazi wa mkoa huo, elimu isiyokidhi mahitaji kwa vijana na zao la kahawa kurudishwa kwa wakulima ili wauze wenyewe na kuondokana na vyama vya ushirika.

 “Wakati tunapata uhuru mkoa wa Kagera ulikuwa ni miongoni mwa mikoa miwili ya kwanza yenye maendeleo Tanzania lakini kwa sasa ndio mkoa wa mwisho kwa maendeleo.

"Hivi huyo mtu aliyetuporomosha akatutoa namba moja sasa tuko wa mwisho anategemea tufanye nini, CHADEMA Kagera tunayo sababu ya kuandamana” amesema Rwizire.

Aidha amesema licha ya fedha zinazotajwa kuwekezwa kwenye elimu bado hakuna kiongozi mkubwa wa nchi ya Tanzania anayesomesha watoto wake katika shule za serikali badala yake wanawapeleka shule za binafsi na nje ya nchi.

Rwizire amesema kuwa wamepanga kuandamana kwa tarehe husika kwani nia yao ni kutaka baadhi ya vifungu katika katiba ambavyo havina manufaa kwa watanzania vifanyiwe marekebisho.


Amesema Serikali inatakiwa kufanya marekebisho sheria za uchaguzi ili uchaguzi uweze kuwa wa huru na haki na serikali iwajibike kwa wananchi na siyo wananchi kuwajibika kwa serikali.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake BAVICHA mkoa wa Kagera, Pendo Ngonyani ameunga mkono tamko la viongozi wake wa taifa la kuandamana na kusema naye anatarajia kushiriki katika maandamano hayo.

Mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la Bukoba mjini Chief Kalumuna amesema kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe alisema kuwa amegundua hakuna maridhiano kati ya CHADEMA na CCM pamoja na Serikali katika swala la utayari wa kubadirisha miswada na kufanya marekebisho kwenye sheria za uchaguzi hivyo CCM na Serikali hawana dhamira njema.

     Mwenyekiti wa chadema Bukoba mjini Chief Kalumuna akizumgumza katika mkutano na waandishi wa habari

“Kumbe sisi kama ni uvumilivu tumeonyesha kama ni busara tumeonyesha kama ni hekima tumeonyesha kama ni utayari tumeonyesha lakini wenzetu hawakujali” amesema Kalumuna.

Kalumuna amesema yeye ni mmoja kati ya watu ambao ni waumini wa kuhitaji yafanyike marekebisho ya kitaifa juu ya maswala ya kiuchaguzi.

Amesema katika uchaguzi mkuu wa 2020 yeye akiwa mgombea ubunge jimbo la Bukoba mjini kupitia chama hicho alishuhudia baadhi ya viongozi kama wakurugenzi wa wilaya, vyombo vya ulinzi na usalama na watendaji wa kata wakishinikizwa na viongozi wa ngazi za juu kushinikiza watu wanaowataka.


No comments