MAUWASA YAONDOA TOPE CHUJIO LA MAJI
Na Samwel Mwanga, Maswa
MAMLAKA ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (MAUWASA)iliyoko katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu imeanza kazi ya kuondoa tope katika mtambo wa kusafisha na kutibu maji ulioko katika bwawa la New Sola(Maarufu Bwawa la Zanzui)ambalo liko kwenye kijiji cha Zanzui wilayani humo.
Hayo yameelezwa Desemba 17 mwaka huu na Mkurugenzi Mtendaji wa MAUWASA ,Mhandisi Nandi Mathias katika kijiji cha Zanzui ulipo mtambo huo wakati wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kwa umoja wao wameshiriki kazi hiyo ya kuondoa tope.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa,Mhandisi Nandi Mathias akieleza kazi zinazofanyika za kuondoa tope katika mtambo wa kuchuja na kutibu maji ulioko katika Bwawa la New Sola.
Amesema kwa mujibu wa kanuni za Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji(EWURA)ambayo inawataka kufanya usafi wa mtambo kila baada ya miezi sita.
Amesema wanafanya usafi huo kutokana na maji yanayoingia kwenye bwawa hilo na kisha kuchunjwa kwenye mtambo huo kuwa na kiasi kikubwa cha tope.
Wafanyakazi wa Mauwasa wakiwa kwenye shehemu ya chujio la maji katika mtambo wa kutibu na kuchuja maji wakifanya usafi wa kuondoa tope
Mhandisi Nandi amesema kuwa kwa sasa baadhi ya wananchi wanafanya shughuli za kilimo ndani ya mita 60 ya mito inayoingiza maji kwenye bwawa hilo kinyume cha sheria jambo ambalo linafanya maji kusomba udongo na kuupeleka katika bwawa la New Sola na hivyo maji kutokuwa maangavu.
“Serikali ya wilaya ya Maswa kwa kushirikiana na Bonde la Ziwa Victoria wanalinda mito yote ambayo inaingiza maji kwenye bwawa la New Sola hivyo ilishapiga marufuku kwa wananchi kufanya shughuli za kibinadamu zikiwemo za kilimo ndani ya mita 60 ya mito hiyo lakini bado baadhi ya wananchi kwa musimu huu wamelima kwenye maeneo yaliyokatazwa.
“Kwa sasa kipindi hiki cha sasa mvua ni nyingi sana hivyo sehemu kubwa ya udongo kwenye mashamba hayo unasombwa na maji na kupelekwa moja kwa moja kwenye bwawa na hapo husababisha tope kujaa kwenye mtambo wa kuchuja na kutibu maji.
Baadhi ya wafanyakazi wa Mauwasa walifanya Usafi katika chujio la maji lililoko katika Bwawa la New Sola
"Tunaposukuma kwa wateja wetu yanakuwa si maangavu tena kutokana na kuwepo kwa tope jingi ndiyo maana tumeona tufanye usafi huu kwa muda wa siku mbili,”amesema.
Amesema kuwa katika kipindi hicho ambacho wanafanya usafi huo hawatatoa huduma ya maji na kabla ya kuanza kwa kazi hiyo walishawajulisha wateja wao siku mbili kabla ili waweze kuchota maji ya kutosha yatakayowawezesha kuyatumia kwa kipindi hicho cha siku mbili.
Baadhi ya wafanyakazi wa Mauwasa walifanya Usafi katika chujio la maji lililoko katika Bwawa la New Sola
“Nitumie fursa hii kuwaomba radhi wateja wetu kwa kipindi hiki cha siku mbili tunachofanya usafi wa mtambo huu kuwa hatutatoa huduma ya maji ila kazi tunayoifanya usiku na mchana tutahakikisha tunarejesha huduma ya maji, lengo letu tuwapatie huduma ya maji safi na salama na maji yetu ni lazima yawe maangavu,”amesema.
Aidha amesema kuwa baada ya kukamilika kwa usafi wa mtambo huo baada ya mwezi mmoja kupita wataelekeza nguvu kufanya usafi katika tenki la maji ambalo limejengwa chini ya ardhi (Clear water tank)ili wananchi wapate maji yenye Uangavu zaidi ya sasa.
Naye Fundi Sanifu Ubora wa Maji wa MAUWASA, Mary Maiko ameeleza kuwa moja ya faida ya usafishaji wa chujio hilo ni pamoja na kuliwezesha liweze kufanya kazi kwa ubora zaidi kwani likijaa tope uwezo wake unapungua na hivyo kusababisha maji kutokuwa maangavu na kuwa na kiasi cha tope jamboi ambalo si zuri kwa watumiaji wa maji.
Fundi Sanifu Ubora wa Maji wa Mauwasa,Mary Maiko akielezea faida za kufanya usafi kwenye mtambo wa kuchuja na kutibu maji.
Esther John mkazi wa kitongoji cha Majebele mjini Maswa amesema hatua ya MAUWASA kuamua kufanya usafi wa mtambo wa kuchuja na kutibu maji ni jambo la muhimu sana kwani kwa sasa walianza kupata maji yakiwa na kiwango kidogo cha tope tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma kabla ya mvua kunyesha.
“Maji kwa sasa si meupe kama ilivyokuwa siku za nyuma kabla ya mvua kunyesha hivyo kwa hatua ya Mamlaka kuliona jambo hilo na kuamua kufanya usafi wa hilo chujio la maji wanaonyesha ni jinsi gani wamejipanga kutuhudumia sisi wateja wao,”amesema.
Michael Jisena mkazi wa kitongoji wa Mwangui mjini Maswa ameuomba uongozi wa serikali wa wilaya ya Maswa kuhakikisha watu wote ambao bado wanaendelea na kufanya shughuli za kilimo katika vyanzo vya maji, ukiwemo mto Sola unaopeleka maji katika bwawa la New Sola wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria, kwani hao ndicho cha tope kujaa kwenye bwawa na kwenye mtambo wa kutibu na kuchuja maji.
Mtambo wa kutibu na kuchuja maji ulijengwa na serikali kwa gharama ya zaidi ya Tsh. Bilioni tatu ili kuhakikisha kuwa wananchi wa mji wa Maswa na vijiji vipatavyo 12 vinavyopata huduma ya maji kupitia chanzo hicho wanapata maji safi na salama na ya uhakika.
Tope linaloonekana kwenye moja ya vizimba vya kuchujia maji katika mtambo wa kuchuja na kusafisha maji ulioko katika bwawa la New Sola wilayani Maswa mkoa wa Simiyu ulioko chini ya Mauwasa.
Post a Comment