MWANASHERIA WA SERIKALI AWAFUNDA MAWAKILI, AWAPA MIONGOZO 10
Na Gustafu Haule, Pwani
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali Dkt. Eliezer Feleshi amewafunda mawakili kutoka ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kuwapa miongozo 10 inayotakiwa kuzingatiwa pindi wanapotekeleza majukumu yao.
Dkt.Feleshi ametoa miongozo hiyo Januari 17 wakati akifungua mafunzo ya Viongozi kwa menejimenti ya ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali yanayofanyika katika Chuo Cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani.
Dkt Feleshi ametaja miongozo hiyo kuwa ni pamoja na kuhakikisha mawakili wote wa Serikali wanajifunza maarifa na stadi mpya za kazi bila kukoma ili kuendana na ulimwengu unavyobadilika.
Amesema moja ya miongozo hiyo ni kuandaa dondoo na mawasilisho ya kazi na mrejesho wa kazi wanazofanya na tatu ni kuwai eneo la kazi walau nusu saa kabla ya kuanza,huku muongozo wanne ni kuwa na mawasiliano na mahusiano mazuri na wafanyakazi wenzao pamoja na wadau wengine.
Aidha, katika muongozo wa tano Dkt.Feleshi amesema mawakili hawapaswi kutenda jambo lililo nje ya maelekezo waliyopewa kama wameelekezwa kufanya jambo fulani wakati muongozo wa sita ni kuwa muangalifu katika maneno na mawasiliano wanayofanya.
Kwa mujibu wa Dkt.Feleshi muongozo wa saba unawataka mawakili kujilinda na uovu na kuwa muaminifu muda wote na kama Kuna jambo baya wamefanya basi ni vyema wakatoa taarifa mapema.
Amesema, muongozo wa nane unamtaka Wakili wa Serikali kuwa tayari wakati wowote na kutoacha ombwe la uwakilishi na kwamba Wakili wa Serikali popote alipo anapaswa kujua ibara ya 6 ya Katiba.
Dkt.Feleshi ameongeza kuwa muongozo wa tisa ni kuhakikisha Mawakili wa Serikali wanawajengea uwezo wenzao kupitia TSW ikiwa na maana ya Tekeleza jukumu ulilopewa ,Saidia kufanyakazi na Wezesha huku muongozo wa 10 ni kufanya utafiti bila kukoma.
Mbali na hayo lakini pia Dkt.Feleshi amewataka Mawakili wa Serikali pamoja na viongozi wengine walioshiriki mafunzo hayo kuhakikisha wanafanyakazi zao kwa kuzingatia maadili katika utoaji wa huduma.
"Nimewapa miongozo 10 ya kutumia katika majukumu yenu lakini maadili ni muhimu kwani hatuwezi kuwa na watumishi wa umma wasio na maadili au wenye maadili hafifu katika utendaji wao wa kazi kwani hili ni takwa la kisheria lakini pia ni takwa la kijamii ambapo binadamu yeyote kuwa na maadili katika kuhusiana na binadamu mwenzie,"amesema.
Kwa upande wake Wakili Mkuu wa Serikali Dkt.Boniphace Luhende,katika kipindi cha miaka mitatu ofisi yake imekuwa na desturi ya kufanya mafunzo na kikao cha faragha kwa ajili ya menejimenti ya ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali pamoja na baadhi ya Viongozi pindi wanapoingia mwaka mpya wa kalenda.
Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende, akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika katika Chuo Cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha.Lengo la mafunzo hayo ni kujikumbusha wajibu na kupanga vipaumbele vya mwaka 2024 na kuweka mikakati ya utendaji kazi hususani katika kuelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika mwaka huu na uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Dkt.Luhende amesema pia mafunzo hayo yanalenga kuboresha ufanisi na kusaidia utatuzi wa ujumla wa changamoto mbalimbali ambazo zinajitokeza katika utendaji kazi wao.
Dkt.Luhende amesema mafunzo hayo yaliyoanza kufanyika Januari 16 mwaka huu yamejumuisha mawakili wafawidhi wa Serikali kutoka Mikoa mbalimbali ambapo siku tatu za mwanzo wanafundishwa kuhusu masuala ya Uwekezaji wa namna ya kujiongezea kipato.
Amesema mada nyingine ni afya ya akili na saikolojia, mfumo wa mpya wa usajili na uendeshaji mashauri huku siku mbili za mwisho kutakuwa na kikao cha faragha cha kufanya tathimini.
Amesema katika kipindi cha mwaka 2023 ofisi yake imepata mafanikio makubwa kwani hadi kufikia Septemba 2023 walifanikiwa kuendesha mashauri 7,393 ambapo kati ya hayo mashauri 7,256 ni ya madai na 137 ni ya usuluhishi.
Pia Luhende amesema wamefanikiwa kumaliza jumla ya mashauri 620 ambapo mashauri 579 yalimalizika kwa njia za Kimahakama na mashauri 42 yalimalizika kwa njia ya majadiliano nje ya mahakama.
Nae Kaimu Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Mark Mulwambo,amesema kuwa mafunzo hayo yamejumuisha wakuu wa idara ,wakuu wa vitengo, mawakili wa Serikali wafawidhi wa Mikoa,na ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
Kaimu Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Mark MulwamboHata hivyo, Mulwambo amesema kuwa washiriki hao wametoka katika Mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Dododma, Kigoma , Tanga, Ruvuma.
Mikoa mingine ni Rukwa ,Iringa, Mtwara, Kilimanjaro, Mwanza, Mbeya ,Kagera, Shinyanga, Morogoro,Mara na Manyara.
Post a Comment