HEADER AD

HEADER AD

MWENYEKITI MAWASILIANO ASHAURI DORIA ZIFANYIKE KUKABILIANA NA WIZI WA TAA ZA BARABARANI

Na Dinna Maningo, Tarime 

MWENYEKITI wa Mtaa wa Mawasiliano Kata ya Bomani Mjini Tarime, mkoani Mara, Chacha Balozi amewaomba Wenyeviti wa Mitaa ambao Taa za Barabarani zimepita kwenye mitaa yao washirikiane kwa pamoja kudhibiti wizi wa taa za barabarani.

Aidha amesema kuwa watakaobainika kuiba taa za barabarani katika mtaa anao uongoza atahakikisha wanasakwa na kuanikwa hadharani mbele ya wananchi kisha watawajibishwa kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza na DIMA Online amesema tangu kuwekwa taa za barabarani zimesaidia kuwepo mwanga wa kutosha ambao umesaidia kupunguza vitendo vya uhalifu lakini anasikitika kuona wizi wa taa umezuka kwa baadhi ya mitaa iliyopitiwa na taa za barabarani.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mawasiliano Kata ya Bomani Mjini Tarime, mkoani Mara, Chacha Balozi

"Wenyeviti wenzangu nawaomba tufanye doria za mara kwa mara mitaani kwetu. Mwanzoni kulikuwa na taa zalizowekwa na halmashauri baadhi ya taa zikaibwa na zingine zilikufa kwakuwa zilikuwa na uwezo mdogo wa mwanga.

"Serikali kupitia TANROADS ikatuletea taa zenye mwanga wa kutosha zikawekwa katika baadhi ya barabara hapa mjini na mtaa wangu umepitiwa na hizo taa.

" Nashangaa kusikia kwamba kumezuka wizi wa taa za barabarani, kule Buhemba wezi wameiba taa eneo ambalo lilikuwa hatarishi kwa vibaka kuvamia watu njiani, taa zilivyowekwa uhalifu ulipungua sasa utarejea tena" amesema.

Mwenyekiti huyo amesema kuna haja ya kufanya upekuzi kwenye gereji na maeneo yanayonunua vyuma chakavu na kwamba baadhi ya taa zinazoibwa huuzwa nchini Kenya.

            Mwenyekiti wa Mtaa wa Mawasiliano Chacha Balozi akionesha moja ya taa ya barabarani iliyotolewa betri.

"Nawaomba wananchi wangu mtaani kwangu tuwe walinzi kuhakikisha tunaisaidia serikali yetu, tusiachie serikali tu ndo iwe mlinzi wa taa za barabarani, likitokea mtaani kwangu tutawasaka na tutawataja hadharani ili washughulikiwe "amesema Chacha.

Ameongeza kusema " Inasemekana kuwa taa zikiibwa zinaenda kuuzwa Kenya, kwenye magereji na wanakonunua vyuma chakavu, naomba ukaguzi ufanywe kwenye maeneo hayo haiwezekani turudishwe kwenye giza tunajua madhara ya giza" amesema Mwenyekiti.

Wakala wa mabasi yaendayo mikoani kampuni ya Batco katika stendi kuu ya Mabasi mjini Tarime, Weboga Warioba amesema uwepo wa taa za barabarani zinasaidia usalama wa abiria wanapopita barabarani kuingia stendi.

           Wakala wa mabasi yaendayo mikoani kampuni ya Batco katika stendi kuu ya Mabasi mjini Tarime, Weboga Warioba

"Taa zikiwepo barabarani zinapunguza wizi kwa abiria wanaosafiri maana wakati wanatembea barabarani kwenda stendi barabara inakuwa na mwanga hivyo kibaka hawezi mvamia tofauti na miaka ya nyuma vibaka walivamia watu barabarani wakati wakiingia stendi kwakuwa hakukuwa na taa za barabarani" amesema Weboga.

Ameshauri kuanzishwa kwa vikundi vya ulinzi shirikishi vitakavyozunguka mitaani nyakati za usiku kwani vitasaidia kupunguza matukio ya wizi wa taa za barabarani.

            Taa iliyotolewa betri maeneo ya darajani mjini Tarime

Meneja Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) , Wilaya ya Tarime Mkoani Mara, Mhandisi Charles Marwa akizungumza na chombo hiki cha habari amewaomba wananchi kuwafichua wezi wa Taa za barabarani.

Amesema kuwa kumezuka wizi wa taa za barabarani lakini wananchi hawatoi taarifa dhidi ya wanaohujumu miundombinu ya barabara jambo ambalo linarudisha nyuma jitihada za serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi.

             Meneja Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) , Wilaya ya Tarime Mkoani Mara, Mhandisi Charles Marwa 


No comments