HEADER AD

HEADER AD

WENYEVITI , DIWANI KIBASUKA WAFUNGUKA UKOSEFU DARAJA MTO TIGHITE


Na Dinna Maningo, Tarime

UKOSEFU wa Daraja Mto Tighite umewaibua baadhi ya viongozi ngazi ya vijiji na Kata ya Kibasuka na Matongo-Nyamongo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara na kusema kwamba daraja likijengwa litarahisisha shughuli za wananchi za kijamii na kiuchumi.

Wakizungumza na DIMA Online kwa nyakati tofauti viongozi hao wanaunga mkono malalamiko ya wananchi toka katika kata hizo wakilalamika adha zinazowapata kutokana na ukosefu wa daraja mto Tighite unaotenganisha Kata ya Matongo na Kata ya Kibasuka huku wakiiomba Serikali iwajengee daraja .

        Mwananchi mkazi wa Kata ya Kibasuka akivuka mto Tighite

Siku ya Jumatatu, Januari, 08, 2024 katika chombo hiki cha cha habari cha DIMA Online iliripotiwa Makala yenye kichwa cha habari kisemacho 'UKOSEFU DARAJA MTO TIGHITE MKUKI UNAOWACHOMA WANANCHI, MIFUGO NYAMONGO - KIBASUKA'.

Ni baada ya Mwandishi wa DIMA Online hivi karibuni kufika kwenye mnada wa Ng'ombe na bidhaa mbalimbali na mifugo uliopo Kitongoji cha Nyabibago, Kijiji cha Matongo- Nyamongo unaofanyika Jumatatu ya kila wiki.

          Nguo zikiuzwa mnadani

Mwandishi allifika ili kufahamu kwa namna gani wananchi wa Kata ya Matongo na Kata ya Kibasuka wanavyopata adha kuvuka mto Tighite lakini pia kufahamu namna mifugo inavyopata shida kuvuka mto pindi inapopelekwa malishoni na kuuzwa mnadani.

Wananchi na wafugaji wakaeleza namna mto Tighite unavyowapa kero ikiwemo vifo, kusombwa na maji, mifugo kushindwa kuvuka mto huku wakilipa sh. 1000 kuvuka katika daraja la miti lililotengenezwa na mwananchi kwa lengo la kuwapunguzia adha ya ukosefu wa kivuko na wasio na fedha hulazimika kuogelea na kutembea majini kuvuka mto.

          Wananchi wakivuka daraja la miti,gharama ili uvuke darajani ni sh. 1,000.

Viongozi wazungumza

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyabibago, Kijiji cha Matongo, Charles Ryoba anasema daraja likijengwa mapato katika mnada wa Matongo yataongezeka na wenye mashamba watazalisha zaidi mazao.

"Huu mnada umedolola sana kwasababu ya huu mto Tighite, ukijaa watu wanashindwa kuvuka kuja mnadani, wanashindwa kuvusha mazao kwakuwa hakuna daraja, na lililopo la miti halikidhi mahitaji. Daraja likijengwa mapato yanayopatikana katika mnada huu yataongezeka.

      Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyabibago, Kijiji cha Matongo, Charles Ryoba.

"Wapo watu wanahitaji kuleta  ng'ombe, mazao na biashara mbalimbali mnadani,  lakini wanashindwa kwa sababu ya mto, daraja likijengwa litashawishi mnada kukua kwa haraka" anasema.

Mwenyekiti huyo anasema ukosefu wa daraja unawaathiri kiuchumi wakulima " kuna watu hapa Matongo wana mashamba ng'ambo ya mto, maji yakiwa mengi hawaendi shambani kulima au kupalilia, matokeo yake mazao yanadumaa na uzalishaji kuwa mdogo.

Anasema kwamba yeye ni mzaliwa katika kijiji cha Matongo na shida ya mto anaifahamu na ameshawahi kupeleka kero hiyo ya ukosefu wa daraja katika mamlaka ya Serikali.

        Ng'ombe wakivuka mto Tighite

" Hii shida ya mto Tighite naijua na watu wawili naowakumbuka walishakufa wakivuka mto na wengine wasio na idadi walisombwa na maji na kuokolewa wakati wakivuka mto.

" Nilichaguliwa 2019 kama Mwenyekiti wa Kitongoji, hii shida niliiona nikapeleka Serikali ya Kijiji cha Matongo, sisi kama Kitongoji tuliungana tukatengeneza daraja la mti ambalo baadae lilisombwa na maji miti ilioza likaharibika.

Anaongeza " Mwananchi mmoja aliona changamoto hiyo akaitumia kama fursa alijitolea na kutengeneza daraja la miti ambalo watu huvuka kwa sh. 1000 ambalo limesaidia sana watu.

                Daraja la Miti Mto Tighite lililotengenezwa na mwananchi

"Tunamshukuru sana kwa hilo sema bado halijakidhi hitaji, kwanza ni hatarishi limetengenezwa kwa miti ambalo huwezi kujua huimara wake. Wazee wanaogopa kupita kwenda mnadani kwasababu ya hali yenyewe" anasema Mwenyekiti.

Mwenyekiti huyo anasema tayari changamoto hiyo ilishajadiliwa kwenye vikao vya serikali ya kijiji na kwamba Meneja Wakala wa barabara za Vijijini na Mjini ( TARURA) wilaya ya Tarime Mhandisi Charles Marwa alishafika katika mto huo na kushuhudia daraja la miti.

"Tunaomba Serikali itujengee daraja kwasababu nilishalipeleka hilo serikali ya kijiji na  ikapeleka kwenye vikao vya WDC na Diwani analijua, hata Meneja TARURA alishakuja nikampeleka mpaka pale kwenye barabara inayotoka Nyarwana.

" Taarifa hiyo anaijua na kila siku anatuahidi daraja litatengenezwa lakini bado hatujaona matokeo, tunaomba chombo hiki cha habari kitupazie sauti ili wakubwa na wanaoweza kutusaidia watusaidie" anasema Charles.

Daraja likijengwa litakomesha mapigano

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwara Masero Marwa Mnanka anasema kuwa  wakati mwingine kumekuwa kukizuka mapigano ya koo Jamii ya kabila la wakurya wa Kitongoji cha Nyabibago koo ya Wanyamongo na koo ya Wanyabasi Kitongoji cha Mwara wakigombania ardhi, hivyo daraja lilijengwa litachochea mahusiano mema kwa koo hizo.

      Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwara, Masero Marwa Mnanka

" Daraja likijengwa itakuwa mwisho wa mapigano ya koo kwasababu litakuwa na muingiliano wa watu mbalimbali zikiwemo koo hizo, makabila tofauti tofauti watapita darajani kwenda Nyamongo na Tarime kupitia mto Tighite -barabara ya  Nyarwana -Mogabiri hadi Tarime.

" Itakuwa rahisi askari Polisi kufika pindi yatokeapo matukio ya uhalifu na uvunjifu wa amani maana hata yalipotokea mapigano polisi walipata shida kufika eneo la tukio kutokana na ukosefu wa daraja uliosababisha gari kushindwa kupita na pikipiki kushindwa kuvuka "anasema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyarwana Naftari Mgesi anasema kwamba waumini ambao ni wakazi wa Kitongoji cha Mwara wanaabudu katika makanisa na kupata huduma ya afya ng'ambo ya mto katika kijiji cha Matongo.

       Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyarwana Naftari Mgesi.

"Wakazi wangu wa Kijiji cha Nyarwana hususani Kitongoji cha Mwara wanapata huduma zao Kijiji cha Matongo, na mto Tighite ndio umetenganisha kata hizo, akina mama wanapata huduma ya afya Zahanati ya Matongo, maji yakiwa mengi wanashindwa kuvuka wakati wa kwenda kujifungua na kujikuta wakijifungulia njiani.

"Pia litarahisisha shughuli za wakulima watapitisha mazao yao kwa amani pindi wanapotoka kuvuna shambani na uchumi wa mkulima utakuwa kwakuwa atakuwa na uhakika wa kufanya shughuli za kilimo kwa wakati wote atakaotaka yeye" anasema Naftari.

Daraja litapunguza umbali 

Diwani wa Kata ya Kibasuka Thomas Nyagoryo anasema daraja likijengwa wananchi wa kijiji cha Nyarwana hawatahangaika kutembea umbali mrefu kwenda kupata huduma ya Afya Hospitali ya Halmashauri iliyopo Kata ya Nyamwaga km 20 na badala yake watatembea mwendo wa km.6 kwenda Nyamongo kupata huduma ya afya.

      Diwani wa Kata ya Kibasuka Thomas Nyagoryo.

"Tunateseka pia vifaa vya ujenzi kuna vingine havipo senta ya Nyarwana mpaka usafiri umbali wa km 50 kupitia Komaswa kufuata vifaa Tarime mjini au  ukizungukia Nyamwaga ni km 47. 

"Ili uende mnada wa Matongo kuuza mazao mpaka uzunguke uwanja wa ndege kwenda Nyamongo kwa gharama ya zaidi ya sh. 10,000 ambapo ungepitia mto Tighite ungetumia usafiri wa sh. 2,000-3,000"anasema Diwani.

Anasema mto Tighite umekuwa kero kwa wananchi " Huu mto ulishaua watu wengi kama 10 , waliosombwa na maji hawana idadi, Serikali ituone ituondolee hii changamoto maana inarudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

Anaongeza kuwa changamoto hiyo ilishajadiliwa kwenye vikao vya baraza la Madiwani na kwamba TARURA iliwaeleza kuwa tayali swala hilo la daraja limeshapelekwa serikalini na endapo itatoa fedha daraja litajengwa. Nini Kauli ya TARURA ?

 ........Itaendelea....

            Ng'ombe wakivuka mto




No comments