HEADER AD

HEADER AD

RC SIMIYU AAGIZA WASIO NA VYOO WACHUKULIWE HATUA ZA KISHERIA

Na Samwel Mwanga, Maswa

MKUU wa mkoa wa Simiyu, Dkt. Yahaya Nawanda ameuagiza uongozi wa wilaya ya Maswa mkoani humo kuwachukulia hatua za kisheria watu wote ambao nyumba zao hazina vyoo.

Ametoa agizo hilo ikiwa ni moja ya mkakati wa kupambana na ugonjwa wa kuhara na kutapika uliozuka katika wilaya hiyo na kusababisha shughuli nyingine za kiuchumi kusimama.

Hayo yameelezwa Desemba ,9 mwaka mjini Maswa na mkuu huyo wa mkoa wakati akizungumza na Viongozi wa wilaya hiyo wakiwemo viongozi wa dini.

           Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Dkt Yahaya Nawanda akizungumza na Viongozi na Wadau mbalimbali wa wilaya ya Maswa (hawako pichani)juu ya kujikinga na ugonjwa wa kuhara na kutapika uliozuka katika wilaya hiyo.

Wengine ni wazee maarufu na Watendaji wa Kata na Vijiji katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo kwa lengo la kupambana na ugonjwa huo ambao umekuwa ukisambaa  kwenye wilaya hiyo na mkoa wa Simiyu kwa ujumla.

Amesema ugonjwa huo ni wa aibu pia ni wa kujitakia ambao unasababishwa na uchafu kutokana na baadhi ya watu kutokuwa na vyoo na hivyo kujisaidia kwenye vichaka na kusababisha kuenea kwa ugonjwa wa kuhara na kutapika.

          Mkuu wa mkoa Simiyu,Dkt Yahaya Nawanda(wa pili kushoto)akiongoza msafara wake kukagua Kaya zisizo na Vyoo mjini Maswa.

Rc Nawanda amesema kuwa amefika katika wilaya hiyo kwa ajili ya kuhamamisha watu kufanya usafi baada ya kuona kazi hizo hazifanyiki huku ugonjwa huo ukiendelea kuenea.

Amesema kila mmoja kwa nafasi yake ahamasishe suala la usafi kwenye maeneo yao na wale wasio na vyoo wasakwe na kuchukuliwa hatua za kisheria kwani kwa sheria za mazingira zinataka kila kaya kuwa na choo bora na siyo bora choo.

   Baadhi ya Wakuu wa Divisheni na  Vitengo katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa wakiwa kwenye kikao cha kuthibiti ugonjwa wa kuhara na kutapika  kilichoitishwa na Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Dkt Yahaya Nawanda,(hatuko pichani).

“Huu ugonjwa ni wa aibu katika familia na ni wa kujitakia kwa sababu hujengi choo na usipokuwa na choo utapata ugonjwa huu maana utakwenda kujisaidia vichakani na inzi watabeba vijidudu vya ugonjwa huo na kuvisambaza na hatimaye utavila kwenye chakula na ndipo utakapoanza kuhara na hatimaye kutapika sababu umekula uchafu yaani kinyesi chako mwenyewe tena kibichi.

“Niwaombe ndugu zangu kufuatia ugonjwa huu wa aibu nimefika kuhamasisha masuala ya usafi na leo nitatembelea baadhi ya Kaya kuona masuala ya usafi hasa vyoo maana nimeona kwa wilaya hii kazi haifanyiki ndiyo maana ugonjwa huu umeenea maeneo mbalimbali,”amesema.

Amesema hana mzaha na hivyo kuwataka viongozi wa wilaya hiyo wakiwemo Maafisa watendaji wa Kata na Maafisa Watendaji wa Vijiji kuhakikisha wanazingatia maagizo hayo ambayo ameyatoa ili kuhakikisha ndani ya juma moja ugonjwa huo unatoweka kwenye wilaya hiyo.

Aidha katika kupambana na ugonjwa huo Mkuu huyo wa mkoa ametoa maagizo katika wilaya hiyo ambayo ni pamoja na kupiga marufuku vyakula kwenye maeneo ya mikusanyiko kama vile kwenye misiba,kupiga marufuku uuzaji wa vyakula katika shule zote, Migahawa yote inayofanya biashara.

     Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Dkt Yahaya Nawanda (kulia)akimpatia maelezo ya Usafi wa Mazingira mjasiliamali (kushoto)aliyemkuta akikaanga samaki maeneo ya Stendi mpya mjini Maswa wakati waukaguzi wa vyoo kwa kila Kaya wilayani humo.

Ameagiza watu kuwa na maji tiririka ya moto ya kunawa mikono kabla na baada ya kula na amepiga marufuku biashara ya mahindi ya kuchemshwa, biashara ya pombe za kienyeji kwenye maeneo yasiyo na vyoo huku akiwataka wakulima wanaokwenda kulima kwa umoja wao kwenda shambani na maji ya kunywa yaliyochemshwa na siyo kunywa maji ya madimbwi.

Awali Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge amesema kuwa ugonjwa huo uligundulika kuwepo katika wilaya hiyo tangu Desemba 27 mwaka jana hivyo kwa kushirikiana na Wataalamu wa Afya,Viongozi wa dini,Watendaji wa Kata na vijiji Madiwani na Wadau mbalimbali wa maendeleo walikutana na kuweka mikakati ya kupambana na ugonjwa huo.

      Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Aswege Kaminyoge akitoa taarifa  ya hali halisi ya wilaya hiyo juu ya ugonjwa wa kuhara na kutapika katika kikao kilichooitishwa na Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Dkt Yahaya Nawanda,(hayuko pichani).

Amesema kuwa waliunda timu za ufuatiliaji ambazo zilipita katika maeneo kuhamasisha suala la usafi wa mazingira na ujenzi wa vyoo kwa watu ambao hawana vyoo kwa kutoa elimu ya kanuni za afya  na kwa wale ambao ni wakaidi aliagiza wachukuliwe hatua za kisheria.

“Tangu ugonjwa huu ulipoingia katika wilaya yetu Desemba 27 mwaka jana tulianza kuchukua hatua mbalimbali ili kukabiliana nao tulikutana viongozi wa wilaya pamoja na wataalamu wa afya na wadau mbalimbali tukaanza kutoa elimu ya kanuni za afya hasa usafi wa mazingira na wale watu ambao hawana vyoo tuliwahamasisha wajenge waliokiuka tumeanza kuwachukulia hatua.

“Kuna kiongozi mmoja ambaye ni Mwenyekiti wa kitongoji katika Kijiji cha Mwasayi  tumemkamata kufuatia kuwatorosha wananchi 10 katika eneo lake ambao hawana vyoo na kwa sasa yuko kituo cha polisi wilaya ya Maswa na atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zake zinazomkabili,”amesema.

DC Kaminiyoge amezitaja Kata ambazo zimeathirika na ugonjwa huo ni pamoja na Busilili, Masela, Mwamanenge, Nguliguli,Seng’wa, Lalago,Budekwa, Shanwa, Binza na Sola.

Naye Mganga Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dkt. Hadija Zegega amesema kuwa hadi sasa wilaya hiyo ina wagonjwa 8 ambao wamelazwa wakiendelea kupatiwa matibabu kwa ajili ya ugonjwa huo wa kuhara na kutapika.



 Amesema suala la watu kupuuza kujenga choo si jambo la kufumbia macho kwani kitendo hicho kinachangia idadi kubwa ya wagonjwa walioathirika na magonjwa ya mlipuko kama huo wa kuhara na kutapika haasa wakiwa watoto na watu wazima.

Nao baadhi ya wananchi ambao nyumba zao zilikaguliwa na Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Dkt Nawanda aliyeambatana na msafara wake katika eneo la Shanwa mjini Maswa walisema sababu ya kukosa vyoo inatokana na ardhi yao kutitia chini kila wanapoandaa choo.

Maelezo hayo yamepingwa na RC Nawanda na kusisitiza kukosa choo ni uzembe kisha akaweka mkazo na kusema sheria ndogo za halmashauri na za nchi zitatumika kuwatia hatiani watakaokaidi agizo la kujenga choo.


No comments