HEADER AD

HEADER AD

UGUMU WA MAISHA UNAVYOMTESA CHARLES OWINO OGADA


Na Dinna Maningo, Rorya

" Natamani kuwa na mke, natamani kuwa na watoto, natamani tendo la ndoa, natamani kulala kwenye kitanda kizuri, natamani kula nyama ya kuku, natamani kula samaki, natamani kunywa soda" anasema Charles Owino Ogada.

Charles Owino Ogada amezaliwa mwaka 1964, ni mlemavu wa viungo asiyeweza kutembea, mkazi wa kitongoji cha Begi katika Kijiji cha Majengo, Kata ya Koryo, wilaya ya Rorya mkoani Mara, anayetamani kuwa na ndoa na maisha bora.

             Charles Owino Ogada akiwa ndani ya nyumba yake katika Kitongoji cha Begi Kijiji cha Majengo

Unapomtazama Charles ni dhahiri utajawa na huruma, na wakati mwingine machozi yatakudondoka kutokana na hali yake ya kimwili na ugumu wa maisha alionao, ama kweli wahenga wanasema hujafa hujaumbika.

Charles anatunzwa na kaka yake Mussa Daniel Ogada. Ndani ya nyumba ya Charles yenye chumba kimoja katika kitongoji hicho cha Begi kuna kipande kidogo cha godoro kilichozeeka kilichowekwa juu ya jamvi .

Anakitumia kipande hicho cha godoro kulala nyakati za mchana na usiku kinachompa maumivu katika mwili wake na kumyima usingizi kwakuwa hana uwezo wa kumudu kuwa na kitanda kizuri na godoro la kisasa.

            Charles Owino Ogada akiwa amekaa mbele yake kinaonekana kipande cha kodoro anachokitumia kulala

Mlemavu huyo wa viungo anajifunika shuka iliyozeeka huku akilalia godoro ambalo halijatandikwa shuka, ndani ya nyumba yake zinaonekana nguo chache zikiwa zimetundikwa juu ya kamba.

Akizungumza na DIMA Online, Charles anaeleza hali ya maisha yake huku matamanio yake makubwa ni kuwa na ndoa, malazi mazuri na mlo kamili.

Anasema kuwa alizaliwa akiwa na ulemavu wa viungo, wazazi wake wote walishafariki mwaka 2002, anaishi na kaka yake mwenye wake wawili na watoto wanne wanaomtegemea.

" Mimi na kaka yangu tunaishi kwenye ardhi tuliyoachiwa na wazazi wetu, kaka yangu ana wake wawili, mke mmoja anaishi hapa kijijini ambaye ananihudumia mimi.

"Kaka anaishi Mwanza na mke mwingine , alienda huko kutafuta maisha, akipata nafasi anakuja kijijini kwa siku kadhaa alafu anarudi Mwanza" anasema Charles.

Anasema kuwa shemeji yake Jenifa Mussa anamtunza kadri uwezo unavyopatikana ila ugumu wa maisha wa familia unamtesa kwani wakati mwingine anatamani kula kuku, samaki, kunywa soda lakini hana uwezo kwakuwa familia haina kipato kizuri.

" Natamani kula kuku, napenda ninywe soda, natamani kula samaki lakini nakosa kwasababu sina pesa ya kununua, sina kazi sitembei zaidi ya kujiburuza kwa makalio, nimechoka kula ugali na dagaa.

" Nalala chini kwenye kipande hiki cha godoro kama unavyokiona, huwa naumia viungo vya mwili, natamani na mimi nilale kwenye kitanda kizuri chenye godoro zuri.

"Mwambie Rais Samia anisaidie na mimi nipate maisha mazuri kama walemavu wengine, nateseka na ugumu wa maisha aninunulie Kiti mwendo ( wheelchair) " anasema Charles.

Anasema shemeji yake anapokuwa ameondoka kwenda kufanya biashara zake ndogondogo huteseka peke yake nyumbani.

"Shemeji yangu ndio ananipikia chakula , ananiogesha, anapokuwa ameenda kwenye shughuli zake nabaki peke yangu.

"Wakati mwingine nachelewa kula kwasababu lazima na yeye atafute pesa ili tuweze kuishi hawezi kukaa tu kumtegemea mme wake" anasema Charles.

Ndoa ni muungano wa hiari kati ya mwanaume na mwanamke kuishi pamoja kama mume na mke kwa muda wote wa maisha yao.

Kwa umri wa charles anapaswa kuwa na ndoa kwa maana ya mke na ikiwezekana kuwa na watoto, lakini hajafanikiwa kwa kile anachoeleza ni umaskini wa kipato ndio umemkosesha mke, kwani angekuwa na maisha mazuri au angezaliwa katika familia ya kitajiri angekuwa na ndoa.

"Kutokuwa na ndoa sio kwamba ni kwasababu ya ulemavu, wapo walemavu kama mimi lakini wana ndoa wana wake na watoto kwasababu wana vipato na wengine wanatoka familia za kitajiri zenye pesa, ukiwa na pesa utampaka mwanamke yeyote umtakaye.

" Natamani sana kuwa na ndoa natamani kufanya tendo la ndoa lakini sijawahi kupata mwanamke. Nina uwezo wa kushiriki tendo la ndoa.

"Nikipata mwanamke ntamudu maana jogoo wangu anapanda mtungi vizuri hajalala, nina nguvu na ninaweza, huwa nikizidiwa sina namna nalala " anasema huku akicheka.

Charles anasema kuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa ngozi kama anavyoonekana katika picha ambao umekuwa ukimtesa, anasumbuliwa na tumbo la mara kwa mara pamoja na kichwa.

Charles anaishukuru Serikali kupitia Mradi wa mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) ambao umekuwa ukimpatia fedha kama mnufaika wa kaya maskini kwani zimemwezesha kujenga nyumba anayoishi na pesa nyingine kuitumia katika mahitaji yake madogo madogo.

           Nyumba anayoishi  Charles Owino Ogada iliyopo Kitongoji cha Begi iliyojengwa kwa fedha za TASAF anazopokea kama mnufaika wa kaya masikini

" Nilianza kupokea fedha za TASAF tangu awamu ya kwanza ,huwa napokea sh. 20,000, zimenisaidia kaka yangu akanijengea nyumba nayoishi, pesa nyingine wananinunulia dawa na mahitaji mengine japo pesa hiyo ni kidogo haitoshelezi mahitaji yangu kama mlemavu" anasema Charles.

Mussa Daniel Ogada kaka wa Charles anasema katika familia yao wamezaliwa watoto wanne, anasema kuwa anapata chagamoto kumuhudumia mdogo wake kwakuwa ana wake wawili na watoto na kipato chake cha ufundi ujenzi hakitoshelezi kukidhi mahitaji.

             Mussa Daniel Ogada anayeishi na Charles akiwa nyumbani kwake Kitongoji cha Begi.

"Mimi ni fundi ujenzi wakati mwingine sipati kazi ya ujenzi, kipato changu hakitoshelezi. Mdogo wangu anapenda kuugua mara kwa mara hasa tatizo la upungufu wa damu.

" Mimi ndio nahangaika kuhakikisha anapata matibabu kwa pesa nazochakarika mwenyewe maana pesa ya TASAF ni ndogo haitoshi.

"Anapenda sana samaki, kuku na soda lakini kwa maisha yetu vinapatikana kwa nadra, kibaya zaidi akiugua ukimpatia dawa ni shida kumeza.

"Ili anywe dawa mpaka umsimamie na wakati mwingine anakwambia kameza kumbe kazibana mdomoni ukitoka anatema unazikuta chini" anasema.

Anasema mdogo wake amekuwa akisumbuliwa na maradhi jambo ambalo limemradhimu kumchukua na kuishi nae Mwanza kwa muda ili apate matibabu.

         Charles Owino akiwa katika hospitali ya Butimba jijini Mwanza hivi karibuni alipokuwa akipatiwa matibabu

" Niko nae Mwanza kwa muda tu kwa ajili ya kupata matibabu huwa nampeleka kupata matibabu katika hospitali ya Butimba na hospitali binafsi, hana bima na gharama ni zangu najikuta nalemewa na majukumu" anasema.

"Chakula anakula kwa shida, hanywi maji yaani kwa mwezi mzima anaweza kutumia lita mbili za maji tu na ukimlazimisha anazila kula chakula. Huwa tunambembeleza kula chakula wakati mwingine tunamwimbia wimbo ndio anakula.

Jenifer Mussa anasema shemeji yake anapata shida kwani analazimika kumwacha nyumbani peke yake ili kwenda kutafuta riziki na wakati mwingine huchelewa kwenda nyumbani.

Anasema watu wenye ulemavu wanaotoka katika familia duni wanakabiliwa na changamoto za matunzo hivyo ni vyema wakasaidiwa kuhakikisha nao wanaishi katika maisha bora.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Begi Christian Odundo Othiong'o anasema kuwa kutokana na hali ya mlemavu Charles aliingizwa kwenye mpango wa kaya masikini ambapo hupokea fedha ambazo zimekuwa zikisaidia katika mahitaji yake madogo madogo.

        Aliesimama mbele ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Begi Christian Odundo Othiong'o

Anawaomba wadau kumsaidia lakini pia apate tiba stahiki ya ugonjwa wa ngozi alionao pamoja na maradhi mengine yanayomsibu na kwamba makundi maalum yanahitaji kusaidiwa.

Ulemavu ni hali inayotokana na dosari ya kimwili au kiakili ya muda mfupi au ya kudumu ambayo inampunguzia mtu uwezo na fursa sawa katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali katika jamii.

Upungufu huo unaweza kuchochewa na mazingira na mtizamo wa jamii kuhusu ulemavu.

Sera ya Taifa kwa watu wenye Ulemavu

Kwa mujibu wa Sera Taifa ya maendeleo na huduma kwa watu wenye ulemavu ya mwaka 2004 inasema watu wenye ulemavu ni miongoni mwa watu maskini katika jamii.

Maisha yao yanaambatana na vikwazo ikiwa ni pamoja na kutengwa. Ushirikiano wao katika uzalishaji mali ni mdogo.

Madhumuni ya Sera hiyo ni kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu katika jamii kutekeleza yafuatayo ;

Kuchochea maendeleo ya watu wenye ulemavu, kuwezesha familia za watu wenye ulemavu kumudu makali yatokanayo na matunzo ya mtu mwenye ulemavu.

Kurekebisha sheria zisizolinda na kutoa haki kwa watu wenye ulemavu, kutoa huduma bora kwa watu wenye ulemavu, kutoa nafasi kwa watu wenye ulemavu kushiriki katika maamuzi na utekelezaji wa maswala muhimu ya kijamii.

Kuwezesha familia za watu wenye ulemavu na jamii kwa ujumla kushiriki katika maamuzi na utekelezaji wa maswala muhimu yanayowahusu watu wenye ulemavu.

Charles Owino anahitaji msaada wa matunzo na matibabu bora. Anayewiwa kumsaidia awasiliane na kaka yake Mussa Daniel anayeishi na kumuhudumia kwa kumpigia simu kwa namba +255767987809 au +255782948660.

No comments