MAMLAKA YA MJI MDOGO WA MASWA YAVUNJWA
Na Samwel Mwanga, Mwanga
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu kwa kauli moja limepitisha azimio la kuivunja Mamlaka ya mji mdogo wa Maswa iliyoko kwenye halmashauri hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa imeshindwa kujiendesha tangu kuanzishwa kwake Machi 26 mwaka 2010.
Pia baraza hilo limepitisha azimio la kuanzishwa kwa halmashauri mbili katika wilaya hiyo ambazo ni Halmashauri ya Maswa Mashariki na Halmashauri ya Maswa Magharibi.
Madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Maswa wakiwa katika kikao.Maamuzi hayo yamefanyika Februari 16 mwaka huu katika kikao cha baraza hilo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa akiwasilisha azimio hilo mbele ya wajumbe wa baraza hilo amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo miaka 13 iliyopita imeshindwa kufikia malengo ambayo yaliwekwa ya kufikia hadhi ya halmashauri ya Mji.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Maswa,Maisha Mtipa akitoa ufafanuzi wa jambo katika kikao cha baraza la Madiwani.Amesema kuwa kwa Mamlaka hiyo imeshindwa kusimamia shughuli za maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii tangu ilipoanzishwa na kupewa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ambaye alikuwa na jukumu kubwa la kutekeleza mambo hayo pamoja na kusimamia vyanzo vya mapato na matokeo yake imekuwa ikiibebesha mzigo wa gharama Halmashauri ya wilaya.
“Ukusanyaji wa Mapato, Mamlaka ya mji mdogo pamoja na kuwa ilipewa baadhi ya vyanzo vya mapato imeshindwa kusimamia vyanzo hivyo na matokeo yake imeendelea kuwa mzigo kwa halmashauri ya wilaya kwa kugharamia shughuli za Mamlaka hiyo kama vile posho za wajumbe wa Baraza la mji mdogo.
“Wameshindwa kusimamia usafi wa Mji tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo ukiachilia mbali miji mingine midogomidogo. Mji wa Maswa wenyewe umeendelea kuwa mchafu na hata kupelekea mlipuko wa kipindupindu katika maeneo kadha ya mji huo huku wakiendelea kuajiri watumishi wa muda(vibarua)ambao ni wazee sana na hivyo kushindwa kabisa kumudu shughuli za usafi katika mji huo,”amesema.
Mtipa ameendelea kueleza kuwa kumekuwa hakuna mahusiano mazuri kati ya Mamlaka hiyo pamoja na Halmashauri hiyo na kinachoshuhudiwa ni kulaumiana na hasa kwa Mamlaka ya mji mdogo kuihukumu halmashauri kwa kila kitu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa (aliyesimama) akitoa ufafanuzi katika kikao Cha Baraza la Madiwani“Kitendo cha Wajumbe wa Baraza la Mamlaka kuzivamia ofisi za fedha za halmashauri kwa kile walichodai kuwa wanatetea posho zao za vikao ni kielelezo tosha kuwa Mamlaka hiyo haiheshimu halmashauri mama na kudhorotesha uhusiano katika na mamlaka hizo mbili,”amesema.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Maswa,Paul Maige amesema kuwa pamoja na kuendelea kuilea Mamlaka hiyo ili ifikie malengo ambayo yalikuwa yamekusudiwa na wananchi wa wilaya hiyo kuwa na Halmashauri ya Mji lakini imeshindwa kwa kipindi cha miaka 13.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Paul Maige (aliyesimama) akifungua kikao Cha madiwani.“Mamlaka ya mji mdogo ni kipindi cha mpito kuelekea hadhi ya halmashauri ya mji ambao wananchi wa wilaya ya Maswa walitamani kufikia malengo hayo lakini hawa tuliowakabidhi jukumu hilo wameshindwa ndani ya miaka 13 hivyo hatuna budi kuivunja kwa kujibu wa sheria,”amesema.
Amesema kuwa baada ya azimio hilo kupitishwa na Madiwani wote wameridhia mpango wa kuanzishwa kwa halmashauri mbili katika wilaya hiyo ili waweze kusogeza huduma kwa wananchi kwa kuzingatia ya wilaya hiyo ni kubwa ina Kata 36 na ina majimbo wawili ya Uchaguzi la Maswa Mashariki na Maswa Magharibi.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM)wilaya ya Maswa ,Onesmo Makota amesema kuwa chama hicho kimeunga mkono maazimio yote mawili yaliyopishwa na baraza hilo kwa lengo la kusogeza huduma karibu na maendeleo kwa wananchi lakini pia kutapunguza mzigo kwa halmashauri ya wilaya ya Maswa katika kusimamia utekelezaji wa shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Maswa,Onesmo Makota akizungumza kwenye kikao Cha baraza la Madiwani.Akitoa salamu za Serikali katika kikao hicho, Katibu Tawala wa wilaya ya Maswa, Athuman Kalaghe amesema kuwa ni vizuri kwa madiwani hao kuwa msitari wa mbele kuhakikisha wanasimamia maamuzi ambayo wanayatoa kwenye vikao vyao vya kisheria.
Katibu tawala wa Wilaya ya Maswa,Athuman Kalaghe akitoa salamu za serikali katika kikao cha baraza la madiwaniAmewataka kushirikiana na watendaji wa halmashauri hiyo kusimamia mapato ya ndani kwenye maeneo yao.
Mamlaka ya Mji Mdogo wa Maswa ilianzishwa rasmi Machi 3 mwaka 2010 kupitia tangazo la serikali GN No.356 la Septemba 17 mwaka 2004, Mamlaka za Miji midogo huanzisha kwa mujibu wa kifungu 16 na 17 cha sheria ya serikali za Mitaa(Mamlaka za Wilaya)na kifungu cha 7 ya mwaka 1982.
Madiwani wakiwa katika kikao cha baraza la Madiwani mjini Maswa
Post a Comment