HEADER AD

HEADER AD

MFUMO WA UTOAJI HAKI JINAI ULIVYO MUHIMU KATIKA USTAWI WA TAIFA

Na Dinna Maningo, Tarime

KILA mwaka Mahakama ya Tanzania huadhimisha siku ya sheria nchini ambayo ni kiashiria cha kuanza kwa mwaka mpya wa kimahakama.

Siku ya sheria hutanguliwa na wiki ya sheria ambayo madhumuni yake ni kutoa elimu kwa wananchi pamoja na wadau mbalimbali katika wilaya husika.

Kwa mwaka huu wiki ya sheria ilianza Januari, 24, 2024, na uzinduzi rasmi ulifanyika Januari, 27,2024 ambapo kilele chake hufanyika kila mwezi wa Februari, 01, ya kila mwaka.

      Watendaji wa Mahakama ya wilaya ya Tarime na Mahakama za Mwanzo katika wilaya hiyo wakiwa wameketi wakati wa kilele cha maadhimisho siku ya sheria nchini

Kwa mwaka huu wa 2024 kauli mbiu ilikuwa ni " Umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa jamii wa Taifa ; Nafasi ya mahakama na wadau katika kuboresha mfumo jumuishi wa haki jinai.

Wilayani Tarime mkoani Mara, maadhimisho ya kilele cha siku ya sheria yalifanyika katika viunga vya Mahakama ya wilaya ya Tarime.

Watenda kazi wa serikali wakiwemo wa mahakama za mwanzo, mahakama ya wilaya, wanasheria ,viongozi wa dini, polisi na wananchi walijumuika pamoja kuadhimisha siku hiyo.

Veronica Selemani ni Hakimu Mkazi Mfawidhi katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime, anasema kwa tafsiri ya kamusi ya kisheria neno haki ni kile mtu anachostahili kuwa nacho au kile kinachoruhusiwa kufanywa, au kile anachostahili kupokea kutoka kwa wengine kwa mujibu wa sheria.

        Veronica Selemani ni Hakimu Mkazi Mfawidhi katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime, Veronica Selemani akihutumia hadhara katika viunga vya Mahakama ya wilaya hiyo wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria nchini ambayo kiwilaya ilifanyika katika mahakama ya wilaya ya Tarime.

"Haki ni maslahi ya mtu ambayo yanatambuliwa na kulindwa na sheria. Kwa mujibu wa ibara ya 107 A ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mahakama ndio chombo pekee chenye mamlaka ya kutoa haki nchini."anasema Hakimu Veronica.

Anasema mfumo jumuishi wa haki jinai, unamaanisha mnyororo mzima, tangu kubainika kwa uhalifu, utolewaji wa taarifa katika kituo cha polisi, kukamatwa kwa mtuhumiwa, kufanyika kwa uchunguzi wa kosa lenyewe.

Pia uandaaji wa hati ya mashtaka, shauri kupelekwa mahakamani, uendeshaji wa shauri mahakamani, utoaji wa hukumu, mfungwa kupelekwa gerezani hadi anapomaliza kifungo chake na kurudi uraiani.


"Ili shauri la jinai liweze kufika mahakamani kwa ajili ya haki kupatikana hupitia kwa wadau wengine wa haki jinai ili kukamilisha hatua mbalimbali " anasema.

Anasema Mahakama imekuwa ikifanya maboresho kwenye huduma zake ili kutoa huduma bora zinazomlenga mwananchi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya maendeleo ya Taifa 2025.

Hakimu huyo anasema kuwa maendeleo na ustawi wa Taifa yanategemea uwepo wa amani, usalama na utulivu.

Anasema ili kuhakikisha hilo, maboresho ya kimkakati katika tasnia ya utoaji haki yanatakiwa kuwa jumuishi katika kuboresha sera na kanuni kwenye sekta ya sheria na mfumo wa makosa ya jinai nchini .

       Wadau wa Sheria wakiwa katika maandamano wakati wa siku ya sheria

"Katika utoaji na upatikanaji wa haki kunatakiwa kuwa na mifumo imara na jumuishi ya taasisi hususani kwenye eneo la vitendea kazi vya kisasa vya TEHAMA na uwepo wa miundombinu wezeshi baina ya taasisi za haki jinai.

"Hii isipofanyika kutakuwa na madhara mbalimbali ikiwemo ucheleweshaji wa haki, wadau kuchukua muda mwingi na fedha katika kuendesha kesi mahakamani hivyo kukosa muda wa kutosha kujishughulisha na shughuli zao za maendeleo" anasema Veronica.

Hakimu huyo anasema kuwa, kauli mbiu ya mwaka 2024 ina malengo mahsusi ya kuhamasisha mahakama na wadau juu ya umuhimu wa kufungamanisha na kuboresha mfumo jumuishi wa haki jinai.

Mfumo unaosomana utakaosaidia katika kubadilishana taarifa kuanzia hatua ya uchunguzi /upelelezi, uendeshaji wa mashtaka na utoaji wa maamuzi.


"Hili litawezekana endapo mfumo jumuishi wa haki jinai utachukua hatua ikiwa ni pamoja na kufanya uwekezaji kwenye eneo la miundombinu ya TEHAMA na usimikaji wa mifumo ya kidigitali.

"Kuajili wataalam wa TEHAMA na kuwaendeleza kwa mafunzo ili waweze kusimamia na kutoa msaada wa kiufundu.

"Kuwapa vifaa vya kisasa vya TEHAMA ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuongeza ushieikiano kwaa wadau wa haki jinai ili kuharakisha huduma ya utoaji haki " anasema Hakimu.

Anasema mfumo jumuishi wa haki jinai una umuhimu mkubwa katika Taifa kwakuwa utasaidia upatikanaji wa taarifa kwa wakati muafaka.

      Watendaji wa mahakama , polisi, wanasheria wakiwa katika maandamano wakielekea viunga vya mahakama ya wilaya kuadhimisha kilele siku ya sheria nchini.

Anasema utaondoa urasimu wa utendaji kazi katika hatua mbalimbali kwenye taasisi za utoaji haki jinai na kupelekea haki kutolewa kwa wakati kwa mstakabali wa ustawi wa taifa ambapo amani, utulivu, usalama na umoja wa kitaifa utatamalaki.

Anaeleza kuwa mahakama ya Tanzania imekuwa ikishirikiana na wadau wengine wa haki jinai katika kutekeleza utoaji haki kwa wakati na kwa wadau wote na imeendelea kutekeleza kwa vitendo katika utoaji haki kwa wakati.

"Mahakama imeboresha mfumo mpya wa kuratibu mashauri kwa njia za ki-elektroniki unaowezesha; kusjili mashauri kwa njia ya mtandai,upangaji wa mashauri kwa Majaji na mahakimu, uandishi wa hukumu na mienendo ya mashauri moja kwa moja kwenye mfumo.

"Pia mfumo wa kuweka nyaraka katika mfumo digiri kwenye masjala , mfumo wa unukuzi wa tafsiri , mfumo huu unavyohusu unukuzi na kutafsiri mienendo ya mahakama na kuharakisha utayarishaju wa kumbukumbu, hivyo kuepuka utayarishaji wa kumbukumbu kwa mkoni uliokuwa na hatari ya makoa" anasema Veronica.

Anasema mfumo mwingine ni wa Tanzi 11. Mfumo huu unawezesha wadau wa mahakama kupata nyaraka mbalimbali kama vile hukumu, maamuzi mbalimbali ya mahakama na sheria kwa njia ya kielektroniki.


Hakimu huyo anasema mfumo mwingine ni wa usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya mtandao kupitia runinga, ambapo kupitia mfumo huo mahakama inao uwezo wa kuchukua ushahidi wa mahabusu au mfungwa aliyeko gerezani bila ya kufika mahakamani.

Changamoto

Hakimu Veronica anasema mnyororo wa haki jinai unakumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ile ya mifumo katika taasisi kutosomana na hivyo kusababisha ucheleweshwaji wa utoaji haki na kwamba mfumo wa haki jinai unaweza kuboreshwa kwa taasisi hizi;

Taasisi za upelelezi wa makosa ya jinai kama vile jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mamlaka ya mkemia mkuu wa serikali.

Taasisi zingine ni Kitengo cha kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya kuunganisha mifumo jumuishi ya upelelezi/ uchunguzi iliyopo sasa katika taasisi mbalimbali ili kuharakisha utoaji wa haki jinai.

Hakimu Veronica aniomba serikali kuwa, Polisi na taasisi zingine za uchunguzi kuanzisha mfumo wa jumuishi wa TEHAMA utakaosaidia kufuatilia mienendo ya vielelezo mahakamani.

    Mawakili wa kujitegemea na wageni waalikwa wakiwa katika kilele siku ya sheria nchini yaliyofanyika kiwilaya katika mahakama ya wilaya ya Tarime

Pia uondoshaji wa vielelezo hivyo, mathalani, kusomana kwa mfumo wa uchukuaji, upokeaji, uhifadhi, utoaji wa vielelezo mahakamani na uondishaji wake kati ya jeshi la polisi, ofisi ya Taifa ya mashtaka na mahakama.

Anasema pia kuna haja ya mawakili wa serikali na wa kujitegemea kujenga uhusiano ili kufikia malengo ya usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya mtandao.

Anasema ni vyema Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali kufanya jitihada za kuandaa miswada yenye kuakisi mabadiliko ya sheria yenye lengo la kuondoa vikwazo vya upatikanaji haki jumuishi.

Hakimu huyo analiomba bunge kufanya marekebisho ya sheria zinazozuia upatikanaji wa haki jumuishi pale miswada ya mabadiliko inapofika bungeni.

Vile vile Wizara ya fedha iziwezeshe taasisi za haki jinai kutimiza majukumu yake kwa kutenga bajeti inayotosheleza majukumu ya taasisi za haki jinai.

Afisa Elimu Halmashauri ya Mji Tarime, Mwl. Simbanilo Changila aliyekuwa mgeni wa heshima akimwakilisha mkuu wa wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele , anasema ili haki ya mtu itendeke mahakama itende kazi kwa uadilifu kuhakikisha mtu anayestahili kupata haki aipate kwa wakati.

     Afisa Elimu Halmashauri ya Mji Tarime, Mwl. Simbanilo Changila

Anasema Haki ikitendeka kwa wakati itasaidia kuondoa malalamiko kwa wananchi dhidi ya mahakama kutokana na kuwepo ucheleweshaji wa haki za watu.

Hakimu Mkazi Mahakama ya wilaya Tarime , Vincencia Balyaruha anawashukuru wananchi, wadau wa sheria, watumishi wa mahakama, viongozi wa Serikali na na Dini katika kufanikisha kilele cha maadhimisho siku ya sheria nchini.

        Hakimu Mkazi Mahakama ya wilaya Tarime , Vincencia Balyaruha akihutumia hadhara katika viunga vya Mahakama ya wilaya hiyo wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria nchini.

Wakili wa Serikali Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Tawabu Yahaya Issa, akisoma hotuba kwa niaba ya Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Mwanasheria wa Serikali anasema serikali imekuwa mstali wa mbele kuhakikisha changamoto zinazoukabili mfumo wa haki Jinai zinapungua au kuondolewa kabisa.

"Kama tunavyokumbuka Januari, 31, 2023 Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua Tume ya kuangalia jinsi ya kuboresha Taasisi za Haki Jinai nchini.

Tume hiyo pamoja na mambo mengine ilipewa jukumu la kutafuta kiini cha changamoto zinazoathiri haki jinai nchini na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuondoa changamoto katika mnyororo mzima wa mfumo wa haki jinai nchini zinazosababisha wananchi kutopata haki zao ipasavyo" anasema.

Anasema Tume hiyo imefanya mabadiliko mbalimbali ikiwemo kuangalia fikra za kiutendaji, mahusiano kati ya taasisi za haki jinai na raia na kuzitaka taasisi za haki jinai kuendesha na kusimamia haki jinai kwa kuzingatia misingi ya sheria, waledi, usawa, uadilifu pamoja na mila na desturi za watanzania.

Mkazi wa Mtaa wa Rebu Senta Julius Chacha anaiomba mahakama na wapelelezi wa kesi kushughulikia kesi kwa wakati kwani ucheleweshaji wa kesi unasababisha wananchi kukosa imani na mahakama.


No comments