HEADER AD

HEADER AD

UJENZI DARAJA MTO RUAHA KUCHANGIA MAENDELEO MIKOA YA NYANDA ZA JUU KUSINI


Na Mwandishi Wetu Kilombero

IMEELEZWA kuwa Ujenzi wa Daraja  mto Ruaha Mkuu barabara ya Kidatu – Ifakara lenye urefu wa mita 133 mkoani Morogoro, utakapokamilika utakuza uchumi wa wananchi.

Akizungumza hivi karibuni Kaimu Mhandisi Mkazi wa Mradi huo Marcel Kiimu amesema daraja hilo litaunganisha mkoa huo na mikoa mingine ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Lindi,  Mtwara.

Amesema mradi huo unakwenda sambamba na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 66.9.

Amesema katika daraja hilo magari yatapita mawili, moja kila upande , tofauti na awali ambapo lilikuwa likipitisha gari  moja pekee kutokana na ufinyu wa daraja uliosababisha msongamano wa magari.

Amesema pia kwenye barabara hiyo kumejengwa madaraja mengine ya kawaida manne ambayo ni Ikela, Msolwa, Sumbugulu na Kisawasawa, makalavati makubwa 45 yenye urefu wa mita 584 kwa kila moja na makalvati ya kawaida 249, ambayo yote yatasaidia kupitisha maji kwa haraka.

Mradi huo wa kimkakati ni sehemu ya mkakati wa Taifa wa kuwasaidia wakulima wadogo wanaolima mazao ya chakula na biashara kupitia Programu ya uendelezaji Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), waliopo katika Bonde la Mto Kilombero, Ulanga, Mlimba na Malinyi.

Amesema barabara hiyo itakuwa na upana wa mita 9.5 ikiwa na njia ya magari yenye upana wa mita 6.5 yenye lami nzito (asphalt concrete) na mabega ya barabara yenye upana wa mita 1.5 kwa kila upande wa maeneo yasiyokuwa na miji na upana wa mita 2.0 kila upande wenye miji, mitaro ya kupitisha maji na vivuko vya watembea kwa miguu.

Mhadisi Kiimu ameongeza kuwa  mradi huo wa ujenzi ya barabara ya Kidatu – Ifakara unaotarajiwa kukamilika Machi 2024  unasimamiwa na Kitengo cha TECU cha Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS).

Amesema mradi utatumia gharama ya zaidi ya Tsh. Bilioni 128.15, una wafanyakazi 792 kati yao wazawa ni 779 na 13 ni wageni, miongoni mwao wanaume ni 703 na wanawake ni 89. Pia kuna wahandisi wahitimu wa vyuo vikuu watano na wanafunzi toka vyuo vikuu saba.



No comments