WATOTO 110,891 KUPATIWA CHANJO YA SURUA,RUBELLA WILAYANI MASWA
Na Samwel Mwanga, Maswa
HALMASHAURI ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu inatarajia kuwapatia chanjo ya ugonjwa wa Surua na Rubella watoto wapatao 110,891 wenye umri chini ya miaka mitano ili kuweza kujikinga na magonjwa hayo.
Hayo yamesemwa Febuari 15 mwaka huu na Mkuu wa Divisheni wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Dk Hadija Zegega wakati akizindua chanjo hiyo katika hospitali ya wilaya ya Maswa.
Amesema mpango wa halmashauri ya wilaya kupitia divisheni hiyo imepanga kuwafikia watoto hao ili kuhakikisha kila mmoja anapatiwa chanjo hiyo ambayo ni muhimu sana kwa ajili ya kuwalinda ili wasiweze kupata magonjwa hayo.
“Mpango wa halmashauri ya wilaya ya Maswa ni kuwafikia Watoto110891 kwa kipindi cha siku nne kuanzia leo februari 15 hadi februari 18 mwaka huu na tukiwachanja wote hao tutakuwa tumefikia lengo letu la kuwachanja watoto kwa asilimia 100 waliopo katika wilaya ya Maswa,”amesema.
Dk Zegega amesema ili kuweze kufikia malengo hayo ni vizuri Wakinamama wenye watoto wenye umri huo kuwapeleka watoto wao katika vituo vya kutolewa chanjo ili waweze kupaya chanjo hiyo ili kuwakinga na ugonjwa wa surua ambao unaweza kumsababishia mtoto upofu na madhara kwenye mapafu.
“Napaenda kutoa rai kwa akinama wenye watoto wenye umri wa miezi tisa hadi miezi 59 kuwapeleka watoto wao katika vituo vya kutolea chanjo ili waweze kupata chanjo hii ya surua na rubella kwani ugonjwa wa surua ni hatari kwa watoto unaweza kumsababishia upofu pamoja na madhara kwenye mapafu,”amesema.
Awali Mratibu wa Chanjo wilaya ya Maswa, Abel Machibya amesema kuwa Hospitali ya wilaya hiyo ni miongoni mwa vituo 102 ambavyo vitatoa chanjo hiyo ili kuhakikisha watoto wote waliowekwa kwenye lengo la kuchanjwa wanafikiwa.
Amesema kuwa chanjo hiyo ni bora na salama kwa afya za watoto hivyo ni vizuri wananchi wote wakajitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto wenye umri huo katika vituo vya huduma na huduma ya mkoba kwa ajili ya kupata chanjo hiyo muhimu kwa afya ya watoto wao.
Mtoto akipatiwa chanjo ya surua na Rubella katika Hospitali ya wilaya ya Maswa“Tutakuwa na vituo 102 kwa ajili ya kutolea chanjo hii ya Surua na Rubella na kituo cha hospitali ya wilaya ya Maswa ni miongoni kati ya vituo hivyo ninawakaribisha wakinamaa wenye watoto wenye umri huo wawalete watoto wao ili wapate chanjo hiyo ambayo ni salama,”amesema.
Pia, amewaasa watumishi wa kada ya afya kutoa huduma kwa kufuata misingi ya viapo vyao na kwa uadilifu na uaminifu ili wananchi wa Maswa washuhudie ubora wa huduma lakini pia thamani ya wanaotoa huduma hizo.
Post a Comment