DC CHACHA ANUSURIKA KATIKA AJALI
Na Samwel Mwanga, Maswa
MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Simon Chacha amenusurika kifo baada ya gari lake binafsi lenye namba za usajili T 911 BRZ aina ya Prado kuacha njia na eneo la jiwe la Hatari kijiji cha Sayusayu wilaya ya Maswa mkoani Simiyu kwenye Barabara kuu ya Shinyanga-Maswa.
DC Chacha alikuwa akitokea wilayani Sikonge mkoa wa Tabora kwenda Musoma mkoani Mara kupeleka mizigo yake nyumbani kwao.
Ajali hiyo ambayo imetokea Machi 19 mwaka huu majira ya saa 4:40 asubuhi akitokea Sikonge kwenda nyumbani kwao Tarime.
Dc Chacha alikuwa akiendesha gari hilo na alikuwa pekee yake kwenye gari iliyokuwa imebeba vitu vyake vya nyumbani.
Watu walioshuhudia tukio hilo wamesema kuwa waliiona gari hiyo ikiwa inayumba na kupoteza mwelekeo na kutoka barabarani na kugonga mawe na kupinduka na mara baada ya ajali hiyo hiyo DC huyo alikimbizwa katika Hospitali ya wilaya ya Maswa kwa ajili ya matibabu.
Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge ambaye alifika Hospitali ya wilaya ya Maswa na baadaye kwenye eneo la tukio akiambatana na Wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo amesema kuwa hali ya Dc Chacha inaendelea vizuri na amepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi.
Dc wa TUNDURU,Simon Chacha akiingizwa kwenye gari la wagonjwa katika Hospitali ya wilaya ya Maswa ili aweze kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando mara baada ya kupata ajali wilayani MaswaAmesema kuwa mara baada ya ajali hiyo Dc Chacha alifikishwa katika jengo la wagonjwa wa dharula katika hospitali hiyo na kuanza kupatiwa matibabu na amepata majeraha katika mkono wake wa kulia pamoja na maeneo ya kichwani.
DIMA Online imefika katika Hospitali ya wilaya ya Maswa na kushuhudia Dc Chacha akiondolewa katika jengo la wagonjwa wa dharula na kuingizwa kwenye gari la wagonjwa lenye namba za usajili STM 8149 kwa ajili ya kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza.
Hivi karibuni Rais Dkt. Samia Suluhu alifanya mabadiliko madogo kwa baadhi ya viongozi na kumhamisha kituo cha kazi wilaya ya Sikonge na kumpeleka wilaya ya Tunduru.
Post a Comment