HEADER AD

HEADER AD

JOKATE MWEGELO : POPOTE NITAKAPOITWA NA WANAWAKE WA TANZANIA AWE MMOJA NITAKWENDA

>>Asema yeye ni Katibu wa Wanawake Nchini

>>Asema Mwanamke yeyote atakayemuita haijarishi idadi, awe mmoja, wawili, watatu, atakwenda

Na Dinna Maningo, Nyamongo

" Nasimama kama Katibu Mkuu wa Wanawake wote nchini Tanzania, popote nitakapoitwa na Wanawake wa Tanzania , awe mmoja mmoja, wawili wawili, watatu watatu, watano watano haijarishi idadi nitakwenda" Jokate Mwegelo.

Jokate ambaye ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) ameyasema hayo wakati akiongea na wananchi katika viwanja vya shule ya sekondari Ingwe, Kata ya Kemambo alipowasili kama mgeni rasmi katika maadhimisho ya wiki ya wanawake Dunia.

Mkurugenzi na mwanzilishi wa Shirika la Health & Safe Delivery Baby Foundation (HSF) lililopo Nyamongo Wilayani Tarime linalojihusisha na maswala ya mama na mtoto, Emmyliana Julius Range kwa kushirikiana na Mkurugenzi na mwanzilishi wa Shirika la Power Life Health & Wealth linalojihusisha na masuala ya kuelimisha afya na uchumi kwa wanawake na vijana, Mariam Selemani walimwalika Jokate kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.

Jokate amesema kuwa popote alipo mwanamke katibu mkuu atakuwepo kwa ajili ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwa ajili ya umoja wa wanawake Chama cha Mapinduzi na kwaajili ya viongozi wakuu.

    Wananchi wakiwa na msafara wakielekea eneo la mkutano

" Kwakweli leo nimefika Nyamongo, kwa mara ya kwanza na nimefurahi kukanyaga ardhi ya Nyamongo, nimefika kwenye tukio kubwa, Twende Mara Oyeeee nawashukuru sana walioandaa hii shughuli .

"Siyo mchezo mnaweza kwakweli kwa mtu yeyote anayeandaa shughuli unaelewa presha ambayo unaipata wakati wa shughuli yako inafanyika. Na mimi nimesema nasimama hapa kama katibu mkuu wa wanawake popote nitakapoitwa nitakwenda" amesema Jokate.

Jokate amesema amepokea changamoto za wanawake likiwamo suala la mikopo huku akifurahishwa  akina mama kurejesha mikopo kwa wakati.

         Katibu wa UWT Jokati Mwegelo akikagua banda la maonesho

"Kitu kikubwa kwa akina mama ni uadilifu hatuna longolongo tumenyooka niwapongezs sana. Mnastahili kupewa mikopo, nikirudi nitaenda kushinikiza Waziri wa TAMISEMI Ofisi ya Rais arejeshe mikopo kwa vikundi mbalimbali.

"Akina mama wanahitaji mikopo wanajitahidi kukopesheka wakikopeshwa wanalipa kwa wakati. Nimewasisitizia CRDC pamoja na taasisi za Kibenki fursa ambazo wanazo za kukopesha wanawake tena ile waliyoniambia bidhaa ya kukopesha bila riba" amesema.

Amezihimiza Taasisi za kibenk kuwawezesha akina mama fursa kwakuwa wapo tayari na kwamba akina mama wa Tarime wanapenda kazi hivyo wasaidiwe wajiinue kiuchumi.

Jokate auagiza Mgodi wa Barrick

Pia ameuagiza Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara kuvipatia zabuni vikundi vidogovidogo vya wanawake kama juhudi za kuunga biashara ndogondogo zinazozalishwa Nyamongo.

      Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Joketi Mwegelo akizungumza na wanawake Nyamongo

"Nimemwita dada yangu kutoka Barrick Safarani nikamuuliza kwenye huu mradi wenu wa kuunga mkono biashara ndogondogo zinazozalishwa hapahapa Nyamongo imekaaje? akaniambia makundi ya wanawake wanayo mawili tu.

"Nimemwagiza tupate makundi mengi ya akina mama, kuna mama ameniomba anatengeneza bidhaa za kusafisha chooni, sabuni n.k anaomba afanye biashara mgodini. Mgodi upo hapa tuwasaidie akina mama wanao uwezo mkubwa tuwaunge mkono tuwaoneshe njia.

Hata hivyo, Jokate amesema kuwa atafurahi kuona matokeo chanya baada ya ujio wake Nyamongo " Mimi sipendi kwenda sehemu nisione matokeo chanya.

"Rais wetu anataka kuona tunajikomboa kiuchumi sasa naomba nimetua mguu wangu hapa ninapoondoka nipate taarifa makundi mengi ya akina mama mmeyasaidia kuweza kupeleka bidhaa zao kule mgodini.

Jokate amesema kuwa lazima wazawa wapate faida na ndio sababu ya kuwepo tukio la wanawake " Hamjaja kusalimiana kunywa soda na kuondoka tumekuja hapa kubadilishana maisha yetu, kukuza mitaji ya kiuchumi.

"Lakini kuongeza watu ambao tutapanua wigo wa biashara, kufahamu watu wengine lakini mwisho wa siku yote yalete mafanikio chanya kwenye biashara zetu na shughuli zingine tunazozifanya za kiuchumi.

Wakati huohuo, Jokate amefurahishwa kuona elimu ya afya ikitolewa wakati akikagua mabanda ya maonesho ya bidha mbalimbali na kusema kuwa wanawake wanateseka sana na maswala ya afya.


"Siku hizi mara mambo ya uzazi, mara mambo ya UTI sugu, lakini watoto wetu wa kike wanateseka sana kujua mabadiliko yao ya kimwili. Kwenye hili tamasha nimefurahi mmetoa huduma ya bure ya afya nimewahamasisha afya ndio mtaji wa mambo yote kabla hujatafuta mkopo tafuta afya.

Katibu huyo wa UWT amesema kuwa bila afya njema mtu hawezi kufanya shughuli yoyote huku akiwaomba akina mama kujiunga na bima ya afya lakini pia kuzingatia  afya zao.

"Tusisubiri mpaka tunaumwa, tukisikia furs kama hizi  makongamano, warsha, matamasha na upimaji wa afya tujitokeze kwa wingi tujue afya zetu, afya ikiwa mbaya kwanza gharama zinakuwa juu za kujitibu, mtaji wetu wa kwanza ni afya bila afya njema hatuwezi kufanya shughuli zozote za kijamii na kiuchumi.

"Nimeipenda ile ngoma yetu hivi (Ritungu) huwezi kufanya hivi (kucheza) kichwa kinauma haiwezekani tumeelewana?" amesema Joketi.

Ameongeza kuwa Rais Samia apongezwe kwani serikali imejenga Zahanati, Vituo vya afya, hospitali ya wilaya nakwamba wananchi wazitumie huduma hizo.

Wanawake wa Nyamongo akiwemo Mwajuma Issa wamempongeza Jokate kuwaheshimisha Wanyamongo kushiriki  nao katika siku ya wanawake duniani.

"Hatukutegemea kama Jokate angekuja Nyamongo lakini kajitoa na kuja kutuona. Kama alivyosema yupo tayali kuitwa na mama yeyote Tanzania mmoja mmoja, vikundi nimefurahishwa sana  tunamshukuru sana "amesema Mwajuma.

Mkurugenzi wa Shirika la Health & Safe Delivery Baby Foundation (HSF) Emmyliana Julius Range amewashukuru wote walioshiriki katika maadhimisho hayo huki akimshukuru Jokate kwa kukubali ombi lao la kuwa mgeni rasmi na hatimaye kufika Nyamongo.

       Mkurugenzi wa Shirika la Health & Safe Delivery Baby Foundation (HSF) Emmyliana Julius Range

"Tumekuwa na wiki ya wanawake na kilele ni leo, nawashukuru wote mliofika , nakushukuru sana mgeni rasmi umetuheshimisha kufika hapa, tunakupenda sana mwenyezi Mungu akubariki tunakukaribisha tena Nyamongo" amesema Emmyliana.

Mkurugenzi wa Shirika la Power Life Health & Wealth Mariam Seleman amesema shirika lake limesajiliwa kisheria kwa malengo ya kuwajengea uwezo wanawake wa kike na wa kiume ili kujikuza kiuchumi.

   Mkurugenzi wa Shirika la Power Life Health & Wealth Mariam Seleman

 " Tunapinga vita vya ukatili vinavyowanyima haki mwawake kuimarisha mahusiano na uhusianonmzuri kwa jamii , tunawajengea uwezo wajasiliamali ili kuweza kuuza bidhaa zao" amesema Mariam.





No comments