HEADER AD

HEADER AD

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI SHIRIKA LA NDC


 Na Gustafu Haule , Kilimanjaro

KAMATI ya Kudumu ya Bunge  inayoshughulika na Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi imeridhishwa na utendaji kazi wa Shirika la  Taifa la Maendeleo (NDC) kwa namna ambavyo limeweza kusimamia uboreshwaji wa kiwanda cha kutengeneza vipuri na mashine mbalimbali(KMTC) kilichopo Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.

Kauli ya kamati hiyo imetolewa Machi 13 mwaka huu  kupitia mwenyekiti wake Deo Mwanyika baada  ya kutembelea kiwanda hicho na kukagua shughuli mbalimbali zinazofanyika kiwandani hapo ikiwemo ya utengenezaji wa vipuri.

Mwanyika ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Njombe kupitia Chama cha Mapinduzi ( CCM)amesema kiwanda cha KMTC kilianzishwa siku nyingi lakini kilishindwa kufanyakazi kutokana na changamoto mbalimbali.

Mwanyika amesema kuwa NDC wanastahili kupongezwa kwakuwa  wamefanya jitihada kubwa za kuhakikisha kiwanda hicho kinaboreshwa na kuendelea na uzalishaji wa vipuri pamoja na mashine mbalimbali kama ilivyokusudiwa wakati wa uanzishwaji wake.

Amesema KMTC ni kiwanda kikubwa kinachoweza kuzalisha viwanda vingine na kimekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa  huku akisema uzalishaji wake unategemea malighafi ya chuma yanayotumika kutengeneza  vipuri na mashine mbalimbali.



"



 Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulika na Viwanda, Biashara,Kilimo,Mifugo na Uvuvi wakiangalia namna ambavyo vipuri vinavyozalishwa katika kiwanda cha KMTC 

Nitumie fursa hii kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kufufua kiwanda hiki kwenye matumizi ya chuma na kuamua kutoa fedha nyingi za fidia kule Liganga ili chuma kile kitumike kiwandani hapa,"amesema Mwanyika .

Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt.Ashatu Kijaji amesema Wizara yenye dhamana ya kusimamia maendeleo ya viwanda hapa nchini imepata fahari kubwa kuona kazi ya kuyeyusha chuma imeanza kiwandani hapo .

Dkt. Kijaji amesema kuboreshwa kwa kiwanda hicho imesaidia kurejesha ajira za Watanzania zilizopotea muda mrefu  na kwamba ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha zilizofanikisha ujenzi wa Tanuru la kuyeyusha chuma pamoja na mtambo wa kutia utandu kwenye chuma.

"Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa na maono makubwa katika Taifa letu ndio maana amekuwa akitekeleza kwa vitendo na anathibitisha kuwa Taifa hili litajengwa kwa uchumi wa viwanda hasa viwanda mama kama hiki cha KMTC,"amesema Kijaji

Kijaji amewashauri  wafanyabiashara mbalimbali kununua bidhaa zinazozalishwa na kiwanda cha KMTC na kwamba wasihangaike kutafuta vipuri vya mitambo yao nje ya nchi kwani KMTC inauwezo kuchonga vipuri vyenye viwango vya juu.

    Mhandisi Adriano Nyaluke wa kiwanda cha kutengenezea Vipuri na mashine mbalimbali kilichopo Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro (KMTC) akiwaeleza wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi iliyotembelea kiwandani hapo jana Kwa ajili ya kukagua shughuli zinazofanyika .

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) Dkt.Nicolaus Shombe amesema kuwa bidhaa zinazozalishwa kiwandani hapo zinagusa sekta mbalimbali kama vile  Kilimo, Viwanda, Uchukuzi, Usafirishaji, Madini, Misitu na Ujenzi.

Hatahivyo Shombe amesema Serikali imeendelea kufanya juhudi  ili kuhakikisha kiwanda hicho kinaboreshwa na hatimaye kiweze kutoa mchango mkubwa wa maendeleo ya viwanda nchini na kuinua maisha ya Watanzania kupitia ajira

No comments