HEADER AD

HEADER AD

MJUMBE KAMATI YA SIASA AGAWA VYAKULA MFUNGO WA RAMADHANI PWANI



Na Gustafu Haule, Pwani

MJUMBE wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Pwani alhaji Musa Mansour amegawa sadaka ya vyakula vya aina mbalimbali kwa zaidi ya wananchi 1500 waliopo katika Halmashauri ya Mji Kibaha.

Mansour amegawa vyakula hivyo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani ulioanza leo Machi 11, 2024 hafla ambayo imefanyika nyumbani kwake Kongowe Kibaha.

      Mjumbe kamati ya Siasa Mkoa wa Pwani alhaji Musa Mansour (kushoto) akikabidhi sadaka ya vyakula Kwa mmoja wa wazee walioshiriki Dua iliyofanyika nyumbani kwake Kongowe Kibaha Mkoani Pwani.

Akizungumza baada ya kumaliza kugawa vyakula hivyo kwa wananchi hao Mansour amesema kuwa amefanya hivyo ili kuwasaidia wale wote wanaokwenda kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani wapate chakuanzia kufuturu siku za mwanzoni.

 Amesema sio Waislamu tu lakini pia amewajumuisha waumini wa kikristo ambao wamefunga Kwaresma kwasababu ya Sikukuu ya Pasaka na wao wamepata vyakula hivyo kwa ajili ya kumalizia siku za mfungo wanapoelekea mwishoni.

Miongoni mwa makundi yanayopewa kipaumbele ni wazee wasiojiweza, wajane, walemavu , watoto wanaoishi katika mazingira magumu na makundi mengine bila kuangalia dini wala ukabila.

       Mtoto wa Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Pwani Tanisah Mansour (kushoto) akigawa sadaka ya vyakula kwa mwananchi wa Kibaha katika hafla iliyofanyika Kongowe Kibaha Machi 10 ikiwa sehemu ya maandalizi ya kuingia katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mansour amesema kuwa utaratibu wa kugawa sadaka kwake sio mpya kwani ameanza tangu miaka saba iliyopita na amekuwa akifanya hivyo kwa wananchi wa mkoa wa Pwani na Dar es salaam .

"Kila mwaka huwa nafanya Maulid na kusoma Dua mara mbili kwa ajili ya  kuwakumbuka wazee wangu waliotangulia mbele ya haki lakini nafanya kwa utaratibu wa kuandaa vyakula na kugawa kwa makundi mbalimbali ya jamii ,"amesema Mansour

Mansour amesema anaamini katika kutoa kwakuwa ndio njia pekee ya kujiwekea hazina Mbinguni huku akiwashauri watu wengine kufanya hivyo kupitia imani na sio kwa ajili ya kupata kitu.

Shekh Mkuu wa Mkoa wa Pwani Hamis Mtupa, amemshukuru alhaji Mansour kwa kufanya tendo la imani la kutoa sadaka kwa wananchi hao huku akisema watu ambao wanafanya matendo ya imani wanapaswa kufanyiwa Dua.

     Shekh Mkuu wa Mkoa wa Pwani Hamis Mtupa, akiongoza ibada ya Dua katika Maulid iliyoandaliw a jana na Mjumbe wa Kamati ya Siasa Alhaji Musa Mansour nyumbani kwake Kongowe Kibaha Pwani.

Mtupa ambaye ameongoza Dua kabla ya kuanza zoezi la kugawa sadaka hiyo amewaasa wananchi waliokusanyika katika Dua hiyo kuendeleza upendo na kujenga  ushirikiano mzuri baina yao ili kuleta amani.

Wananchi waliopokea sadaka hiyo akiwemo Salum Hamis na Mwanaidi Juma, wamemshukuru Mansour kwa kutoa sadaka hiyo kwakuwa inaenda kuwasaidia katika hatua ya awali ya mfungo wa mwezi wa Ramadhani.

Wananchi Kibaha Mjini wakiwa katika foleni ya kupokea sadaka ya vyakula iliyokuwa ikitolewa jana na Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Pwani Alhaji Musa Mansour hafla iliyofanyika nyumbani kwake Kongowe Kibaha ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

"Tunamshukuru Mansour kwa kutoa sadaka hii maana amekuwa mtu wa mfano kwani kila mwaka tumekuwa tukifika hapa kupata sadaka kabla ya kuanza mfungo wa mwezi Mtukufu na hata katikati ya Ramadhani," amesema.

Hatahivyo, wamemuomba Mansour kuendelea na utaratibu huo kwani unamsaada mkubwa kwa jamii huku wakiomba watu wengine wenye uwezo kujitokeza kusaidia jamii inayoishi katika mazingira magumu.

        Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Pwani Alhaji Musa Mansour akigawa sadaka ya vyakula kwa  mmoja wa wazee wa aliyeshiriki Dua ya Maulid iliyofanyika Machi 10 nyumbani kwake Kongowe Kibaha Mkoani Pwani

No comments