DCPC YAICHAPA MABAO POLISI JAMII , BENK YA EXIM YATIA NENO
BENKI ya Exim imepongeza juhudi za pamoja baina ya Wanahabari na Jeshi la Polisi nchini hasa katika ushirikiano wa kijamii ikiwemo michezo.
Hayo yameelezwa na Mwakilishi wa Benki ya Exim, Chrispin Mwakibibi wakati wa Bonanza hilo lililoenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayosheherekewa kila mwaka Machi 8.
Chrispin amesema benki ya Exim imefadhili kwa heshima Bonanza hilo maalum la Polisi na Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Dar es Salaam (DCPC) lililolenga kusherehekea jitihada za kipekee zilizofanywa na wanawake katika jamii.
Bonanza hilo ni ishara ya kutambua mchango muhimu uliofanywa na wanawake, pamoja na jukumu la kuendeleza na kutetea haki za wanawake hapa Tanzania.
"Tunajivunia kuwa pamoja na wanawake katika jamii yetu na kuonyesha msaada wetu kwa kazi yao ngumu na ujitoaji kwao.
"Matukio kama Bonanza la Polisi si tu yanasherehekea mafanikio ya wanawake bali pia yanatukumbusha umuhimu wa kusimama kwa ajili ya usawa wa kijinsia na haki za wanawake." Amesema Mwakabibi.
Amesema jitihada ya pamoja kati ya Benki ya Exim na idara ya Polisi inaonyesha umuhimu wa kutambua na kuwainua wanawake katika jamii kupitia mipango kama Bonanza hilo, ambalo linaweza kuvutia vizazi vijavyo na kujenga mazingira yenye uwezeshaji na yenye kuunga mkono wanawake kufanikiwa.
"Huku tukitafakari mafanikio na maendeleo yaliyofanywa na wanawake hapa Tanzania, tujiunge tena katika kukuza usawa wa kijinsia, kusherehekea tofauti na kusimama kwa ajili ya haki za wanawake wote.
"Kwa pamoja tunaweza kujenga jamii yenye kujumuisha na yenye usawa ambapo kila mwanamke ana fursa ya kufanikiwa na kuleta mabadiliko.’’ Amesema.
Katika Bonanza hilo Club ya Waandishi DCPC iliweza kuibuka mshindi kwa kunyakua kombe hilo kwa mara ya kwanza kwa kuwafunga Polisi Jamii.
DCPC ilinyakuwa ubingwa huo baada ya kuwafunga Polisi Jamii kwa mikwaju ya penalti 4-3, katika mchezo wa fainali uliokuwa wa vute nikuvute kutokana na timu zote kuoneshana umwamba ndani ya dakika 90 na kutoka suluhu bila ya kufungana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi Temeke ACP. Kungu Malulu amewataka waandishi wa habari pamoja na Polisi wawe na mahusiano mazuri yenye kuleta tija katika kazi zao.
Nae Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), Samson Kamalamo ameipongeza timu ya DCPC FC kwa kuiheshimisha taaluma ya uandishi wa habari kupitia michezo.
Pia amelipongeza jeshi la Polisi kwa ushirikiano mzuri katika kuandaa bonaza hilo ambalo limeleta tija kubwa katika kada hizo mbili ambazo mara nyingi zimekuwa zikishirikiana katika utendaji wa kazi.
Ameongeza kuwa lengo la bonanza hilo ni kujenga mahusiano mazuri baina ya waandishi wa habari na jeshi la Polisi nchini
Post a Comment