WANAUME ZAIDI YA 1000 DAR ES SALAAM WAPASULIWA MABUSHA
Na Andrew Chale, Dar es Salaam
WANAUME zaidi ya 1000 Mkoa wa Dar es Salaam, wamefanyiwa upasuaji wa ugonjwa wa mabusha (Ngilimaji) kwenye kambi maalum iliyoendeshwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau, mwishoni mwa mwaka 2023.
Hayo yameelezwa na Mganga mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Dkt. Mohammed Mang’una wakati wa taarifa kwa umma iliyokuwa ikitolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu juu ya matokeo ya tathimini ya hali ya kutokomeza ugonjwa wa matende na mabusha nchini hususani mkoani Dar es Salaam.
Dkt. Mohamed Mang’una amesema mkoa wa Dar es Salaam, watu wamekuwa wakipata ugonjwa huo wa matende na mabusha kutokana na hali ya kimaisha ikiwemo kuhamahama, kutokakuwa na elimu sahihi na hali ya kimazingira.
"Takwimu za waliofanyiwa upasuaji wa ugonjwa wa mabusha ama ngilimaji mwishoni mwa mwaka jana katika kambi tulivuka lengo kwa kuwafanyia upasuaji wanaume zaidi ya 1000.
Upasuaji huu ni mkubwa kwani ulivuka lego lile tulilojiwekea, Lakini pia tunaendelea na zoezi la kutoa elimu ilikuweza kuwafikia watu wote Dar es Salaam." Amesema Dkt . Mohamed Mang'una.
Awali Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ametoa taarifa kwa umma na kueleza kuwa, watu zaidi Milioni 3.7 wameweza kuwaepusha na hatari ya kupata maambukizi ya vimelea vya ugonjwa huo wa matende na mabusha.
"Katika tathimini hizo, ni faraja kwetu kuona kuwa tumefanikiwa kuwanusuru wananchi zaidi ya Milioni 3.7 kuepuka na ugonjwa huu matende na mabusha mkoa wa Dar es Salaam.
"Nipende kumshukuru sana Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuunga mkono jitihada za kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.
"Mwaka jana aliahidi kutoa kiasi cha Dola za kimarekani milioni tatu, katika kipindi cha 2024 ilikufanikisha juhudi za kutokomeza magonjwa hayo.’’ Amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Wataalamu wanasema kuwa chanzo kikubwa cha matende na mabusha ni vimelea vya minyoo midogomidogo jamii ya Filaria, mtu akipata minyoo hiyo inaenda kwenye damu na inaweza kusababisha madhara sehemu za haja ndogo na baadae inaweza kusababisha maji kujikusanya kwenye sehemu za korodani.
Maji yakizidi sehemu hizo za siri huvimba na baadaye hadi ngozi inaweza kuaathiri na kuweka ugumu wakati inapotakiwa kupatiwa matibabu.
Pia sababu nyingine ya magonjwa hayo ni mbu ambao ndio wanaeneza hiyo minyoo na ipo sehemu zote nchini lakini zaidi inapatikana sehemu za Pwani kutokana na hali ya kimazingira.
Imeelezwa kuwa wakati tafiti zinaanza waligundua mbu aina ya Culex, aliyegunduliwa na wataalam wanaoangalia tabia za mbu na wadudu lakini baadaye ikabainika kuwa ni mbu wa aina zote wanaweza kusambaza vimelea vya minyoo midogomidogo.
Vimelea hivyo vinavyosababisha matende na mabusha na kwamba hata mbu anayeeneza Malaria anaweza kusambaza vimelea hivyo vya matende na Mabusha.
Hata hivyo Jamii imeshauriwa kufanya bidii kuzuia mbu kama vile kusafisha mazingira yanayomzunguka, kufukia madimbwi ya maji.
Pia kutumia vyandarua kwakuwa unapojikinga na mbu hujikingi na Malaria peke yake, bali unajikinga dhidi ya homa ya Denge, Matende na Mabusha na vingine vingi.
Post a Comment