NDEGE NYUKI KUTUMIKA UPULIZIAJI VIUADUDU ZAO LA PAMBA MASWA
Na Samwel Mwanga Maswa
WAKULIMA wa zao la pamba katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu wanatarajia kunufaika baada ya kutambulishwa kwa teknolojia ya upulizaji viuadudu kwa kutumia ndege nyuki (drones).
Hayo yameelezwa Machi 11 mwaka huu na Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge katika kijiji cha Senani na wakulima wa zao hilo mara baada ya kujionea majaribio jinsi vifaa hivyo vinavyoweza kufanya kazi kwa kumwagiliaji viuadudu katika shamba la pamba.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge akiongea na wakulima wa zao la pamba katika Kijiji Cha Senani
Amesema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Kilimo imeonyesha dhamira ya dhati ya kumkomboa mkulima kwa kumsogezea zana za kilimo ili aweze kulima kilimo cha zao la pamba kwa tija.
Dc Kaminyoge amesema ili kuipatia zawadi serikali kwa kuwawezesha wakulima wa zao la pamba katika wilaya hiyo kupata vifaa hivyo kwa ajili ya kunyunyizia dawa kwenye zao la pamba hawana budi kuzalisha zao hilo kutoka kilo 600 kwa hekari hadi Kilo 1000.
“Mimi Mkuu wa wilaya ya Maswa nimejionea mwenyewe utendaji kazi wa vifaa hivi vya kisasa kwa ajili ya upuliziaji dawa kwenye pamba yetu vinavyofanya kazi hivyo tunatoa shukrani za dhati kwa serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
“Utekelezaji wa ilani ya CCM unaonekana kwa vitendo kwa serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sijawahi kuona miujiza kama hii ya kupulizia dawa kwa kutumia ndege zisizo na rubani sisi wananchi wa wilaya ya Maswa tunamshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu kwa kutupatia vifaa hivi tunahaidi kumpatia zawadi kwa kuzalisha zaoa la pamba kwa wingi,”amesema.
Amesema kuwa ni vizuri uongozi wa serikali za vijiji kusimamia vifaa hivyo na kuweka utaratibu mzuri kwa ajili ya matumizi yake huku akionya ya kuwa kwa kiongozi yeyote ambaye ataonekana kuwatoza fedha wakulima kwa ajili ya vifaa hivyo vya kunyunyizia viuadudu katika zao la pamba atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Afisa Kilimo wa Bodi ya Pamba wilayani humo, Ally Mabrouk amesema kuwa bodi hiyo inatekeleza mradi wa Jenga kesho iliyo Bora (BBT) kupitia wizara ya kilimo.
Afisa kilimo wa bodi ya pamba Tanzania wilaya ya Maswa, Ally Mabrouk akitoa Elimu kwa wakulima za zao pamba Kijiji cha Senani juu ya matumizi ya Vifaa vya Kilimo vikiwemo ndege nyuki.
Amesema lengo ni kuongeza tija katika zao la pamba hivyo ni lazima tuhakikishe yale mambo yote ya msingi yanayoleta tija yanapatikana na kwamba bodi hiyo imekuja na program maalum kwa kata ya Senani ambayo iko chini ya mradi wa BBT.
Amesema kuwa program hiyo imeongeza nguvu kwa kuajili maafisa Ugani kwa kila kijiji ili kuhakikisha wakulima wanalima kilimo bora cha zao la pamba pia tunatoa vifaa vya kilimo kwa wakulima ili kuweza kuwarahisishia shughuli ya kilimo.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge (mwenye kofia nyeupe) akizungumza baada ya kuona boza la kumyunyizia dawa zao la pamba lilipofanyiwa majaribio.
“Lengo kubwa ni kuongeza tija katika zao la pamba na hii program tunayoitekeleza katika Kata hii ya Senani, tunakuja pia na vifaa vya kilimo kama vile matrekta,vifaa vya kupulizia dawa pamba vikiwemo ndege nyuki, mabomba ya kubeba mgongoni, jembe la kupandia, jembe la kulimia ambavyo vyote vitatumiwa na wakulima kwa kuazima
“ Na hapa tuna lengo tunataka kuifanya hii Kata ya Senani na vijiji vyake vyote kuwa kituo cha zana za kilimo ambapo mkulima atakapohitaji kifaa chochote kwa ajili ya kilimo atakipata bila ya usumbufu wa aina yoyote ili tuhakikishe zao hili la pamba linalimwa kwa tija na mkulima nakila pamba inayolimwa inavunwa ,”amesema.
Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Robert Urasa amesema kuwa moja ya changamoto kubwa iliyokuwa inawapata wakulima wa zao la pamba ni jinsi ya kudhibiti viuadudu katika zao la pamba licha ya serikali kutoa sumu lakini tatizo lilikuwa ni vifaa vinavyotumika kunyunyizia dawa hizo katika zao la pamba.
Mkuu wa Divisheni ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi wilaya ya Maswa,Robert Urassa(wa kwanza kulia),Afisa kilimo wa bodi ya pamba,Ally Mabrouk(wa pili kulia)na Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge(mwenye shati la kitenge )wakiangalia ndege isiyo na rubani (haipo pichani)wakati wa majaribio katika Kijiji cha Senani.
“Tunamshukuru Rais kwa kutupatia vifaa hivi vya kisasa kwa ukweli wakulima wetu walikuwa wanatumia bomba la mgongoni kupulizia sumu licha ya serikali kutoa sumu hizo ili kuua wadudu wanaoshambulia zao la pamba.
"Walikuwa wanatumia muda mrefu hasa wale wenye mashamba makubwa sasa kwa hizi ndege zisizo na rubani wataweza kunyunyizia na hii itatusaidia kuongeza uzalishaji katika zao letu kwa kudhibiti wadudu hao kwa wakati hivyo tutapata pamba iliyo bora,” amesema.
Post a Comment