HEADER AD

HEADER AD

WATOTO WACHANGA ZAIDI YA 120 HUPOTEZA MAISHA HOSPITALI YA RUFAA MARA


>>Sababu za vifo zatajwa

>>Mashirika yaombwa kutoa elimu kwa jamii
 
Na Dinna Maningo, Musoma

IMEELEZWA kuwa kila baada ya miezi mitatu watoto wachanga zaidi ya 30 hupoteza maisha katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Mara Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Hayo yamebainika baada ya Wanawake kutoka shirika lisilo la kiserikali la Health & Safe Delivery Baby Foundation (HSF) lenye makao makuu Nyamongo Wilayani Tarime, likiongozwa na Mkurugenzi wa shirika Emiliana Julius Range pamoja na wanawake kutoka Shirika la Power Life Health & Wealth likiongozwa na Mkurugenzi  Mariam Selemani walipotembelea wodi ya mama na mtoto.

Wanawake kutoka Shirika la HSF na Power Life wakiwa wamebeba watoto wachanga waliozaliwa katika hospitali ya Rufaa mkoa wa Mara

Wanawake hao Machi, 9, 2024 walifika katika hospitali hiyo wodi ya mama na mtoto kuwajulia hali wajawazito na wazazi waliojifungua ambapo walitoa msaada wa vitu mbalimbali Kanga, sabuni, taulo za kike na majani ya chai tiba ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya wanawake duniani.

Daktari Kiongozi Hospitali ya Rufaa mkoa wa Mara Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere , Dkt. Osmundi Dyegura ameyaomba mashirika hayo kutoa elimu kwa jamii ya umuhimu wa akina mama wanapokuwa wajawazito kuwahi kliniki kama njia ya kupunguza vifo vya watoto wachanga wanaozaliwa.

     Daktari Kiongozi Hospitali ya Rufaa  mkoa wa Mara Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere , Dkt. Osmundi Dyegura

Amesema sababu za vifo hivyo ni pamoja na uelewa mdogo wa jamii kutoanza mapema huduma ya kliniki, wajawazito wanaopewa rufaa kutoka hospitali za wilaya katika mkoa huo kufika katika hospitali ya Rufaa wakiwa wamezidiwa sana.

Pia sababu nyingine ni wanaume kutoongozana na wake zao wanapokwenda kujifungua hali inayowapa ugumu madaktari pindi kunapohitajika msaada wa mme.

Amesema vifo vinakuwa vingi kwasababu wale wanaokuwa kwenye hali mbaya kutoka hospitali za wilaya, Zahanati, Vituo vya afya wote wanapelekwa hospitali hiyo ya Rufaa, pindi inaposhindikana na hufika wakiwa wamechoka sana na kwamba vifo vingi ni vya watoto wachanga .

        Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere

Daktari huyo ameeleza "  Kwa upande wa watoto wachanga changamoto bado ni kubwa kwa robo mwaka tunaweza kupata vifo zaidi ya 30 sawa na wastani wa vifo zaidi ya 10 kwa mwezi. 

"Vifo vinachangiwa na mjamzito kuchelewa kufika hospitali kwa ajili ya kujifungua, wanakuja hali ikiwa mbaya sana wakati mwingine kuokoa maisha yake inakuwa shida.

"Watoto wanaoletwa wanakuja wakiwa na hali mbaya au mama anakaa na uchungu muda mrefu anakuja, inakuwa changamoto, wengine wanapata changamoto ya uzazi alafu wanaendelea kukaa nyumbani badala ya kuwahi hospitalini. Kuchelewa kuanza kliniki ni tatizo, tunaomba wajawazito wawahi kuanza kliniki hii inasaidia kufahamu mwenendo wa ujauzito wake.

"Tunaomba mashirika mtusaidie kutoa elimu kwa jamii wakina mama wanapokuwa wajawazito baada ya wiki ya 12 waanze kwenda kliniki hii itasaidia kujua mwenendo wa ujauzito ili kama kuna shida inatatuliwa mapema na anajifungua salama." amesema Dkt. Osmundi.

Akizungumzia vifo vinavyotokana na uzazi Daktari huyo amesema "  Vifo vinavyotokana na uzazi vimepungua sana hadi kufikia vifo vya watu 2-3 kwa miezi mitatu kwahiyo ni wastani wa kifo kimoja kwa mwezi.

" Lakini bado ni tatizo unaweza kusema ni wachache pale ambapo hujafiwa wewe, kwahiyo tunaendelea na jitihada mbalimbali kuhakikisha tunaendana na matarajio ya nchi kuhakikisha inapofika 2030 nchi kama nchi tuwe na vifo chini ya asilimia 75 kati ya vizazi 100,000" amesema.

Daktari Bingwa wa Wanawake na uzazi katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Mara, Patrick Kenguru amesema kuwa jamii bado haijapata mwamko kwamba mama mjamzito anapokwenda hospitali anatakiwa kuambatana na mmewe.

      Daktari Bingwa wa Wanawake na uzazi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara Patrick Kenguru.

"Kuna mfumo dume mama anakuja mwenyewe kujifungua baba haji wakati kuna huduma ambazo anatakiwa kuwepo kutoa msaada, sasa mpaka uanze kumtafuta inachelewesha baadhi ya mambo. Ni muda mwafaka wana Mara tuliangalie hilo anapokuja mama awepo na baba.

Dkt Patrick ameipongeza serikali kwa kutoa vifaa vya kutosha idara ya kina mama huku akiiomba serikali kuwapatia madaktari Bingwa wa kutosha kwani kwa sasa wagonjwa hawaendi kupata huduma hospitali ya Bugando wanaipata mkoani Mara.

Ameomba kutengenezwa kipande cha barabara ya mama Samia Suluhu Hassan kwani ni kero kwa wajawazito na wazazi wanaofika hospitali kwa kutumia usafiri wa pikipiki. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Health & Safe Delivery Baby Foundation (HSF) Emmyliana Julius Range amesema shirika lake litajitahidi kutoa elimu kwa jamii ili wajawazito waweze kuhudhulia kliniki kwa wakati pamoja na kufika hospitali kwa wakati.

   Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Health & Safe Delivery Baby Foundation (HSF) Emmyliana Julius Range, akimjulia hali mzazi aliyejifungua.

Ametoa wito kwa akina mama wanapojitambua ni wajawazito waanze mapema klinimi kwani wanapoanza mapema husaidia kupunguza matatizo mengi ya kiafya ya mama na mtoto.

"Tumefika Hospitali na kuona changamoto , Dkt. amesisitiza elimu tumelichukua tutalifanyia kazi. Niwaombe akina mama wenzangu tujitahidi kuanza mapema Kliniki.

"Matumbo yetu akina mama yana vitu vingi sana, unapoanza kliniki mapema inakusaidia kujua vitu vingi lakini pia itasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto.

"Tumekuwa tukiona wamama wengi wanafika kliniki au kwenda kujifungua akiwa hatua za mwisho kabisa. Mara nyingi hali hiyo inapelekea vifo vingi, ili kupunguza vifo hivi jamani sisi akina mama tuna uwezo wa kupunguza au kumaliza kabisa hivi vifo sisi wenyewe.

Mkurugenzi Shirika la Power Life Health & Wealth, Mariam Selemani
amewaomba wakinamama kufuata ushauri wa madaktari  lakini pale wanapohisi utofauti wafike kwa daktari haraka kwani itasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto.

      Mkurugenzi Shirika la Power Life Health & Wealth, Mariam Selemani.

No comments