MJUMBE MKUTANO MKUU TAIFA SANGO KASERA ATOA MSAADA MADAWATI 70 KATA YA BUKWE
>> Ni baada ya kuwepo uhaba wa madawati shule za msingi zilizopo Kata ya Bukwe
>>Ukosefu wa madawati wanafunzi wakaa chini, wengine walazimika kutandika kanga na jamvi
>>Lakairo akabidhi madawati hayo ofisi ya Kata
Na Dinna Maningo, Rorya
MJUMBE wa Mkutano Mkuu Taifa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoka wilaya ya Rorya, Sango Kasera Gungu ametoa msaada wa madawati 70 katika shule za msingi zilizopo Kata ya Bukwe.
Mbunge mstaafu Jimbo la Rorya Lameck Airo Machi, 15, 2024, akikabidhi madawati hayo ofisi ya Kata ya Bukwe iliyopo Kijiji cha Mika, kwaniaba ya mjumbe huyo wa mkutano mkuu, amesema Sango ametoa madawati ikiwa ni kuunga juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kupitia serikali yake imekuwa ikitoa fedha nyingi za ujenzi wa miradi ya maendeleo.
Lameck Airo akizungumza na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mika wakati alipokabidhi madawati yaliyotolewa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, Sango Kasera
" Rais Samia anafanya kazi kubwa sana kuhakikisha elimu inakuwa bora, katika kuunga juhudi zake Sango ametoa madawati 70 ili kupunguza changamoto iliyopo ya upungufu wa madawati.
"Kata hii ina shule sita kila shule itapata madawati kumi kumi isipokuwa shule ya Bukwe kutokana na uhitaji mkubwa yenyewe imeongezewa madawati mengine kumi " amesema Airo.
Baadhi ya wananchi wa Kata hiyo wamemshukuru Sango kwa kusaidia madawati na kusema madawati hayo yatapunguza changamoto japo bado hayatoshi kumaliza upungufu uliopo huku wakiomba wadau wengine kujitokeza kasaidia ili kuondoa changamoto hiyo ya madawati.
Gody Were mkazi wa Kijiji cha Mika Kitongoji cha Bukwe ambaye ni mzazi wa mwanafunzi anayesoma katika shule ya msingi Bukwe amesema wanafunzi wengi wanakaa chini.
"Madarasa hayana madawati ya kutosha kuna darasa halina dawati hata moja, wanafunzi wanakaa chini ya sakafu ambayo ina mashimo mashimo wanachakufa, wengine wanalazimika kukalia mifuko, kanga na majamvi.
"Shule ya msingi Bukwe ipo karibu na barabara ya lami, wazazi wameshindwa kununua madawati kutokana na kulemewa na michango, tumejenga nyumba ya mwalimu na ujenzi wa shule ya sekondari ya Mika kwahiyo huu msaada wa Sango utasaidia kupunguza ukubwa wa tatizo tunamshukuru sana" amesema Gody.
David Masina amesema shule ya msingi Bukwe ilianzishwa mwaka 1975, darasa la awali (chekechea) halina dawati hata moja, lina wanafunzi zaidi ya 80.
Amesema shule inahitaji kufanyiwa ukarabati wa baadhi ya madarasa baadhi ya madarasa yamechakaa ,mabati yana kutu yametoboka mvua ikinyesha inakuwa shida wanafunzi wananyeshewa.
"Tunamshukuru sana Sango Kasera kwa msaada wa madawati, Kata ya Bukwe ina vijiji 3 cha Buganjo, Mika na Nyasoro ina shule za msingi 6 na sekondari 2, Kijiji cha mika kina ujenzi wa shule ya sekondari Mika yenye kidato cha kwanza na cha pili iliyojengwa kwa nguvu za wananchi, wamejenga pia nyumba ya mwalimu.
"Kutokana na michango hiyo wananchi wameshindwa kuchangia madawati, hakuna hela hali ni ngumu serikali na wadau wengine watusaidie kama Sango alivyosaidia shule yetu kuipatia madawati 20, ameokoa baadhi ya wanafunzi hawatokaa chini "amesema David.
Mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Bukwe Sharif Baraka amesema " Mimi nasoma darasa la tano shule ya msingi Bukwe, darasa letu lina wanafunzi 70 lakini lina madawati 17 wanafunzi wengine wanakaa chini, ili ukae kwenye dawati ni kuwahiana na wakati mwingine unaweza kuwahi mwenye nguvu zake anakutoa anakaa.
Miongoni mwa shule zenye changamoto ya upungufu wa madawati ni pamoja na shule ya msingi Kotwo ina wanafunzi 550, madawati yanayohitajika ni 183, yaliyopo 103, pungufu ni 80. Darasa la tatu lina wanafunzi 68 halina dawati hata moja na madarasa mengine yana madawati machache.
Shule ya msingi Bukwe ina jumla ya wanafunzi 641, mahitaji madawati 2013 yaliyopo ni madawati 100 ,huku darasa la awali likiwa halina dawati hata moja na madarasa mengine yana madawati machache likiwemo darasa la tatu lenye na madawati 7.
Akizungumza kwa njia ya simu mjumbe huyo wa mkutano mkuu Sango Kasera amesema ametoa msaada huo kwakuwa yeye ni kiongozi hivyo amewiwa kuunga jitihada za Serikali katika kupunguza changamoto ya madawati.
"Mimi ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa nikitokea wilaya ya Rorya, ni mzaliwa wa Rorya, nina jukumu la kuchangia maendeleo kama kiongozi
Baadhi ya madawati yakiwa nje ya ofisi ya Kata ya Bukwe yaliyotolewa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa Sango Kasera
"Nilipewa taarifa kuwa kuna changamoto ya madawati hivyo nikaona na mimi nichangie chochote hata kama ni kidogo" amesema Sango.
Mwandishi wa Habari amemuuliza je ni kweli ana nia ya kusaka ubunge 2025 ndio sababu ya kugawa madawati ? nae amesema ;
" Tunajaribu kugusa hata kwa kidogo nilicho nacho, sisi kama wadau lazima tumuunge Rais wetu Dkt . Samia Suluhu hasani, Rais alileta fedha nyingi kujenga miradi zikiwemo fedha za mradi wa Boost wa kujenga madarasa.
"Kila mtu ana haki ya kugombea, muda ukifika ikaonekana nastahili kugombea basi nitagombea, ila kwa sasa natimiza wajibu wangu kama kiongozi na mzawa wa Rorya.
"Nimetoa madawati hayo baada ya kuombwa na baadhi ya watu kuwa shule zao zinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa madawati, nimewiwa kuchangia kidogo kwa nilicho" amesema Sango.
Post a Comment