WATOTO ZAIDI YA 300 KUFANYIWA UPASUAJI TAASISI YA MOYO
Na Alodia Babara, Bukoba
TAASISI ya moyo ya Jakaya Kikwete hupokea watoto 30 hadi 40 kwa siku wenye matatizo ya moyo na watoto zaidi ya 300 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji katika taasisi hiyo kuanzia Januari hadi Desemba, 2024.
Takwimu hizo zimetolewa Machi, 20, 2024 na Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto Nuru Letara kutoka katika taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete katika uzinduzi wa kambi maalum ya siku tano ya madaktari bingwa waliofika hospitali ya rufaa Bukoba, ya mkoa wa Kagera kwa ajili ya kupima wagonjwa wenye matatizo ya moyo.
Dkt Nuru amesema kuwa, kutokana na ukubwa wa tatizo la moyo linalowakabili watu wazima na watoto taasisi hiyo hupokea watoto 30 hadi 40 wenye matatizo ya moyo na hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu watoto 300 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto Nuru Letara akizungumza na DimaonlineAmesema kuna magonjwa ya moyo kwa watoto ya aina mbili ambapo kuna ambayo watoto wanazaliwa nayo moyo ukiwa na matundu na kuna wale wanazaliwa mioyo ikiwa mizima lakini wanapata magonjwa ambayo yanasababisha maambukizi kwenye moyo.
Akizungumzia mtoto anayezaliwa na moyo wenye matundu amesema kuwa, inasababishwa na lishe duni kwani katika kipindi cha miezi mitatu kabla ya mama kupata ujauzito anapaswa kuwa ameanza kumeza vidonge vya vitamin (folic acid).
“Kutokutumia vidonge vya folic acid miezi mitatu kabla ya mama kubeba ujauzito ni moja ya sababu ambayo inaweza kusababisha kuzaliwa watoto wenye matatizo ya matundu ya moyo ikiwemo magonjwa ambayo anaweza kuwa nayo mama wakati wa ujauzito kama kisukari” amesema Dkt Nuru.
Ametaja visababishi vingine kuwa ni pamoja na mama mjamzito kuvuta sigara, kunywa pombe pia inaweza kusababisha mtoto kuzaliwa na matundu ya moyo.
Aidha amesema ili kuepukana na ugonjwa wa moyo wazazi wanapaswa kupanga uzazi ili waanze kutumia vidonge vya vitamin (folic acid) kwa muda muafaka, mama mjamzito kutotumia dawa bila ushauri wa daktari anaweza kujifungua mtoto mwenye matatizo ya moyo.
Kiongozi wa msafara ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka taasisi ya magonjwa ya moyo ya Jakaya Kikwete Dkt Yona Gandye amesema kuwa katika hospitali yao walianzisha tiba mkoba na tangu wameanza waliishatembelea hospitali za rufaa katika mikoa 12 na hospitali ya rufaa ya Bukoba, mkoa wa Kagera ni ya 13 tangu wameanza zoezi hilo.
Amesema kuwa kaasisi hiyo ya moyo tangu imeanza huduma ya m koba imepima watu 10, 807 katika mikoa 12 na kati ya hao 1,367 walibainika wana matatizo mbalimbali ambayo yalikuwa yanahitaji waweze kupewa rufaa kwenda kutibiwa hospitali ya Jakaya Kikwete.
Dkt Gandye amesema katika hospitali ya rufaa ya Bukoba, mkoa wa Kagera wameanza kutoa huduma Machi, 18 mwaka huu na watahitimisha Machi, 22, mwaka huu na hadi machi, 19 wamewaona wagonjwa 194 watoto 34 watu wazima 164.
Amesema kati ya hao 34 walikuwa na matatizo ambayo yako katika hatua ya juu ya tatizo lao na wameishawaanda wagonjwa hao kwa ajili ya kuwapa rufaa kwenda kutibiwa Jakaya kikwete.
“Tumebaini kwamba shinikizo la juu la damu limekuwa ni tatizo kubwa kwa wagonjwa waliokuja kituoni na katika wale wanaopewa rufaa kwenda Jakaya Kikwete
"Tumebaini walipata matatizo mbalimbali ikiwemo shinikizo la damu wamefikia mfumo wao wa utembezaji wa figo aidha uko chini au unaenda kwa kasi sana hivyo tunahitaji kwenda kutathimini kwa kina ili kuja na suruhisho kuona nini kitafanyika” amesema
Ameongeza kuwa magonjwa mengi yanayotokana na moyo ni zao la mfumo wa maisha kutofanya mazoezi au kutozingatia ni chakula gani wanakula na hivyo ametoa lai kwa viongozi kuhamasisha jamii kufanya mazoezi ya viungo ili kuwa na afya imara.
Aidha mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa amesema kuwa lengo la kuja madaktari bingwa ni kusogeza karibu huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo kwa wananchi na kuwapunguzia usumbufu wa kwenda kutafuta huduma hizo Dar es salaam au Mwanza.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa akizungumza na wananchi katika hospitali ya rufaa Bukoba, ya mkoa wa Kagera alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kambi ya madaktari bingwa wa moyo.Amesema magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo ndiyo yanaongoza kwa wagonjwa watu wazima wanaofika kutibiwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa.
Aidha ameongeza kuwa 2021 hadi 2023 ugonjwa wa shinikizo la damu ulikuwa ukiongoza kwa idadi ya wagonjwa waliokuwa wakitibiwa katika hospitali hiyo mfano shinikizo la damu peke yake wagonjwa wa nje walikuwa asilimia 7.92 na wagonjwa wa ndani walikuwa 5.58 ya wagonjwa waliokuwa wanalazwa hospitalini hapo.
Anajoyce Ngilwa mkazi wa kata ya Nshambya manispaa ya Bukoba ameishukuru serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kuleta madaktari bingwa mkoani hapa kwani wamesaidia wananchi kuwapunguzia gharama za kusafiri kwenda kutibiwa katika hospitali ya Jakaya Kikwete jijini Dar es salaam.
Post a Comment