JOKATE ALIVYOTUMIA USIKU WA MWANAMKE NYAMONGO KUWAPA SOMO WANAWAKE
>>Awataka Wanawake kuacha kuoneana vivu, fitna, umbea, kubaguana
>>Meneja NSSF Tarime asisitiza wanawake kupendana
>>Wakurugenzi Shirika la HSF, Power Life waeleza mafanikio
Na Dinna Maningo, Tarime
KWA mara ya Kwanza katika mji wa Nyamongo ,wilaya ya Tarime mkoani Mara kufanyika usiku wa mwanamke, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha mwezi wa wanawake duniani ambapo kila tarehe 8, ya kila mwaka Dunia uadhimisha siku ya wanawake.
Hivi Karibuni Machi, 13, 2024, Shirika la Health & Safe Delivery Baby Foundation (HSF) lililloanzishwa na Mwanamke Emmyliana Julius Range mkazi wa Nyamongo kwa kushirikiana na Mkurugenzi mwanzilishi wa shirika la Power Life Health & Wealth, Mariam Seleman lenye makao yake mjini Musoma walimwalika Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania wa Chama cha Mapinduzi CCM, Jokate Mwegelo kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya wiki ya wanawake yaliyofanyika Nyamongo.
Jokate Mwegelo akikagua mabanda ya maonesho ya wajasiliamali wakati wa maadhimisho siku ya wanawake duniani
Jokate Mwegelo akawasili Nyamongo ambapo aliweza kukagua mabanda ya maonesho ya bidhaa mbalimbali na kuzungumza na wananchi.
Jokate akashiriki usiku wa mwanamke. Katika usiku huo wanawake wakiwa wamevalia mavazi mazuri na wengine sare za batiki wanaonekana wenye furaha huku ukumbi ukiwa umefurika wanawake kibao, ama kweli endapo Jokate asingewasili Nyamongo mioyo ya wanawake ingejawa huzuni.
Katika usiku huo wanawake wakajadili mada mbalimbali, kubwa zaidi wanawake wanasisitizwa kupendana, kuacha wivu, chuki ,fitna, kubaguana na badala yake washirikiane na kuchapa kazi ili kujiinua kiuchumi.
Kauli mbiu ya mwaka huu inasema " Wekeza kwa Mwanamke kuharakisha Maendekeo ya Taifa na Ustawi kwa Jamii".
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mara, Nansy Msafiri anasema ili mwanamke awe kiongozi bora anapaswa kuwa mnyeyekevu.
Mwenyekiti UWT mkoa wa Mara Nansi Msafiri (wapili kulia) akizungumza na wajasiliamali wakati Katibu mkuu UWT (wa nne) kulia alipokuwa akikagua mabanda ya maonesho Nyamongo wakati wa kusherekea siku ya wanawake duniani
" Mwanamke kiongozi bora lazima awe mnyenyekevu au mbunifu asiyekuwa na hofu katika mageuzi yoyote tunawekeza kwasababu mwanamke mjasiliamali ndiyo mtafutaji, tunawekeza tuna uhakika jamii itastawi, itanawili.
"Tupate viongozi wanawake ambao ni waadilifu ,wanyenyekevu, waaminifu, viongozi wanaoenda na kasi ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu" anasema Nansy.
Meneja wa mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Wilaya ya Tarime Adolfrida Mulokozi anawasisitiza wanawake kupendana wasibaguane wala kudharauliana na badala yake wawekeze kwa wanawake ili kuharakisha maendeleo ya Taifa na ustawi wa jamii.
Meneja wa mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Wilaya ya Tarime Adolfrida Mulokozi akizungumza na wanawake
"Wanawake tunatakiwa kupendana tushirikiane. Usitake kujua huyu anatoka wapi, mwanamke ni mwanamke wa Tanzania lazima umkubali, wanawake tupendane bila kujua huyu ni nani, ukishaona mwanamke mwenzio amevaa gauni au sketi mkubali kuna kitu utakichukua kwake.
"Tukishapendana kuna kitu utakichukua kwangu na mimi nitakichukua kwako kwa ushirikiano huo tutapata maendeleo. Acha kubaguana, usimwangushe mwenzako kwamba hafai muinue yawezekana wewe umepata neema mwenzio hajapata, sio lazima wote tuende darasani" anasema Adolfrida.
Mossy Magere mzaliwa wa Nyamongo anasema " Tunapozungumzia wanawake tunazungumzia asilimia 51 ya binadamu wa Tanzania ni wanawake, hivyo ni muhimu kuwekeza kwa mwanawake kwa asilimia 51 kwa mujibu wa sensa.
"Ili tuweze kufikia kwenye usawa ni vyema tuwekeze kwa watoto wetu. Akina mama mtambue vipaji vya watoto tujitahidi kuisaidia serikali tuweze kuwa na watoto wenye vipaji" anasema Mossy.
Afisa Maendeleo Halmashauri ya wilaya ya Tarime Nyamjungu Emmanuel anasema " Akina mama hawa wakiwa sehemu ya Tarime Vijijini wameamua kukualika na wanakukaribisha kufurahi nao. Halmashauri ya wilaya imeweza kuvijengea uwezo vikundi 120 katika huduma ndogo ndogo za kifedha.
Katibu mkuu wa UWT Taifa Jokate Mwengelo ( wa pili kulia) akiwapongeza kwa maandalizi mazuri ya tukio la usiku wa mwanamke. Mkurugenzi shirika la HSF Emmyliana Julius Range (wa kwanza kulia), wa tatu kulia ni Mkurugenzi shirika la Power Life na kushoto ni afisa Maendeleo Halmashauri ya wilaya ya Tarime Nyamjungu Emmanuel.
"Halmashauri imepanga kuendelea kuwezesha akina mama kiuchumi ambapo milioni 400 zipo kwaajili ya mkopo wa asilimia 10 wa Wanawake, vijana na wenye ulemavu" anasema.
Mkurugenzi wa shirika la HSF Emmyliana Range akisoma risala ya shirika anasema shirika hilo limesajiliwa linafanya kazi ndani ya Tanzania ambapo linashughulika na utatuzi wa changamoto za afya ya uzazi zinazowakabili mama na mtoto.
"HSF inajitahidi kuunga juhudi za serikali kuboresha afya na usalama wa mama na mtoto wakati wa kujifungua, tunatambua umuhimu wa kupata huduma bora za afya wakati wa ujauzito yaani uzazi salama na mtoto mwenye afya njema.
"HSF ni shirika linaloshirikisha wanawake kwa njia mbalimbali linatoa elimu na mafunzo kwa wanawake katika maswala ya afya ili waweze kujitambua na kujali afya zao.
Emmyliana anasema shirika limefanikiwa kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa wanawake 500 na matunzo bora kwa watoto wachanga wanaozaliwa na kuwafikia wajawazito 500 ambapo limeweza kutoa misaada mbalimbali ikiwemo kutembelea wodi ya mama na mtoto hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara Kumbukumbu ya mwalimu Nyerere.
Pia Taasisi hiyo imeweza kufanya harambee ya kuchangia ujenzi wa jengo la mama na mtoto kituo cha afya Nyangoto, pesa keshi na ahadi jumla Milioni 600 pamoja na baadhi ya vifaa vya ujenzi, ambapo hadi kukamilika kwa jengo hilo litagharimu Bilioni 2.
Mkurugenzi wa Power Life Mariam Seleman anasema shirika lake limesajiliwa kisheria na lilianzishwa kwa malengo ya kuwajengea uwezo wanawake wa kike na wa kiume ili kujikuza kiuchumi.
Mkurugenzi wa Power Life Mariam Seleman (kulia) na Mkurugenzi wa HSF Emmyliana Range (kushoto) wakimpatia zawadi ya dhahabu yenye thamaniya Tsh. Milioni moja Katibu wa UWT Taifa, Jokate Mwegelo.
"Tunapiga vita vya ukatili vinavyomnyima haki mwanamke, kuimarisha mahusiano mazuri kwa jamii. Shirika limedhamilia kuyafikia maeneo mbalimbali yasiyofikika kutoa elimu ya kijamii na kiuchumi.
"Kuwajengea uwezo wajasiliamali ili kuweza kuuza bidhaa zao, ushauri wa tiba kwa wagonjwa mbalimbali na kushirikiana na HSF kwa lengo la kumkomboa mwanamke katika maswala ya afya.
Anasema shirika linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo maeneo ya kufanyia mafunzo ya vitendo kwa wajasiliamali na baadhi ya watu kukwamisha juhudi za maendeleo ya shirika.
Jokate awaasa wanawake
Jokate Mwegelo anayapongeza mashirika hayo kwa kuandaa hafla hiyo ya kusherekea siku ya wanawake duniani huku akiwataka wanawake kuacha kuoneana wivu na badala yake washirikiane kuleta maendeleo.
"Hawa watu wa Nyamongo wamefanya makubwa na ni wa hapahapa Mara, kila mtu ana kitu chake na hawa wanawake wamekubaliana kuungana. Niwaombe wanawake tuache kuoneana wivu.
" Unaona eti usipomuunga mkono mwenzako wewe utapungukiwa, kila mtu anacho kitu ambacho Mungu amemuumba nacho ndiyo maana anatujua, Mungu ana sababu ya wewe ndio maana tumezaliwa tukaja duniani.
Anaongeza kusema" kinachotukwamisha sisi tofauti na mwanaume, wanaume wao wanapenda sapoti, mwenzake akikosa utasikia chukua Milioni 10, Milioni 50, sisi tunapeana maneno tu.
"Na mimi nimekuja hapa kwa heshima yao hawa wanawake wenye mashirika na kwa heshima ya hiki ambacho wamekifanya, mimi mwenyewe ndio mara ya kwanza namuona dada Emmyliana simjui ndio mara ya kwanza kumuona " anasema Jokate.
Jokate anasema kuwa hajutii kufika Nyamongo na ameridhika na maandalizi yaliyofanywa katika usiku wa mwanamke Nyamongo.
Wananchi Nyamongo wakiupokea msafara wa Katibu wa UWT Taifa Jokate mwegelo pindi ulipowasili nyamongo
"Naomba niseme sijutii kufika Nyamongo sijutii hata kidogo na nimeridhika na maandalizi, yaani nimefurahi mmeandaa vizuri kwelikweli, event (tukio) mmeiandaa vizuri kwelikweli, nyie wenyewe mmependeza mnajipenda sana.
"Nataka niwatie moyo mmeanza vizuri mwendelee yaani mmefanya vizuri kwelikweli. Akina mama wenzangu msiwaangushe hawa wanawake kwenye mipango yao endeleeni kushikamana na hawa akina mama waweze kutimiza ndoto zao" anasema Jokate.
Jokate anawataka wanawake kuendelea kupendana huku akimwomba mwenyezi Mungu amuongoze kama sehemu ya huduma asiwe ilimradi tu kiongozi.
" Ukiona umeinuka muinue na mwenzako, nalisema hilo kwasababu wengine tunaogopa kusaidia wenzetu kwasababu tuna kawivu sana ambako hakana afya.
" Namuomba Mungu aniongoze kutoka moyoni kama sehemu ya huduma, niongoze kama sehemu ya kubadili maisha ya watu na niweze kuvusha watu na kuwasaidia watu.
"Nisiwe tu kiongozi ilimradi tu kiongozi maana bila hivyo sitatimiza sababu za Mungu za kuniumba na kunipa kipaji cha uongozi. Kuna kitu ambacho Mungu amekupa ukifanye kwa ajili ya watu wengine , pengine wewe umeumbwa kuinua jeshi la akina mama wainuke kiuchumi kupitia wewe kama uwe daraja la wao kuvuka.
Jokate anawatia moyo wanawake kupambana bila kuchoka huku akitolea mfano kuwa Rais Samia aliichukua nchi katika wakati mgumu lakini amesimama imara na mambo yanaenda vyema.
Anaongeza " Tulivyonavyo sio vyetu, vingekuwa vyetu ukifa basi ungeondoka navyo, Mungu katupa uwezo kuyafanikisha haya ili kuwasaidia na wenzetu. Tuna fursa nzuri kupitia uongozi wa Rais wetu Dkt. Samia pamoja na changamoto hazimzuii yeye kutosimama imara.
"Tunakumbuka aliichukua nchi katika wakati mgumu, sasa kama yeye amefanikiwa sisi ni akina nani tusifanikiwe?. Hii iwe chaku kuwa na sisi tunaweza kusimama kwenye mambo tunayoyaamini, tunaweza na Mungu hatoweza kutuacha atatupa nguvu ya kusonga mbele" anasema Jokate.
Jokate anawashauri wanawake kutumia vyema pesa walizonazo na kwamba wasipozitumia vilivyo hawatanufaika na badala yake watapata msongo wa mawazo.
" Utaishi maisha mazuri ndio, lakini je alama ulioiacha duniani ni ipi?. Leo hii wote wamekuja hapa kwa sababu ya watatu hawa wenye kampuni zao, wametueleza mambo yao tutakuja kuyakumbuka haya waliyoyafanya.
"Je sisi tunapenda kukumbukwa kwa lipi ? au tunapenda kukumbukwa kwa kusifika kwa umbea, uchonganishi, Fitina, kurudisha watu nyuma? kukatisha watu tamaa, kutukana na migogoro? uamuzi ni wako kuamua.
" Mimi nawaombea mkumbukwe kwa wema, mkumbukwe kwa mazuri, muwainue wenzenu na kuwasema wenzenu kwa wema hapo utakuwa umetenda haki kuliko kukumbukwa kwa umbea na uchonganishi. Wema ni hazina na kizazi cha baadae hivyo" anasema Jokate.
Katika usiku huo wa wanawake, baadhi ya wanawake walipewa tuzo kama wanawake wapambanaji katika maendeleo na wengine kupewa kiasi cha fedha baada ya kuibuka na ushindi katika michezo.
Mgeni rasmi Jokate akapewa dhahabu yenye thamani ya Tsh. Milioni moja kwa ajili ya kumpatia mwanae aliyemruhusu kujumuika na wanawake wa Nyamongo.
Wakurugenzi wa Taasisi ya HSF na Power Life wakamshukuru Jokate kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na kumkaribisha tena Nyamongo.
Post a Comment