CCM SIMIYU YAMSHUKIA MBUNGE MPINA
Na Samwel Mwanga, Itilima
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM)mkoa wa Simiyu kimemtaka mbunge wa jimbo la Kisesa katika wilaya ya Meatu mkoani humo kuacha mara moja siasa za majitaka za kuwachafua viongozi wa kitaifa wa serikali na badala yake ajikite kufanya kazi ya kuwaondolea changamoto wananchi wa jimbo lake.
Pia amewataka wabunge wa mkoa huo kujikita kufanya shughuli za kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi walioko kwenye majimbo yao waliyowachagua ili chama hicho kisipate wakati mgumu wa kuomba kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsa Mohamed ameyasema hayo Aprili 25 mwaka huu wilayani Itilima mkoani humo wakati akizungumza katika mkutano Viongozi wa chama hicho wa tarafa ya Kanadi uliofanyika katika Kata ya Langangabilili kwenye ukumbi wa shule ya sekondari Langangabilili.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsa Mohamed akizungumza na wanachama wa Chama hicho katika Kata ya Langangabilili Tarafa ya Kanadi
Akizungumza na mabalozi, viongozi wa Matawi,Kata pamoja na Madiwani amesema kuwa amefanya ziara katika jimbo la Kisesa na kusikiliza kero za wananchi lakini amekuta katika jimbo hilo kuna changamoto nyingi zikiwemo za maboma ya vyumba vya madarasa kushindwa kuezekwa kwa kipindi cha muda mrefu.
“Kabla ya kufika katika wilaya ya Itilima nilifanya ziara kama hii katika wilaya ya Meatu nimefika katika jimbo la Kisesa ambalo linaongozwa na Mbunge Luhaga Mpina lakini wananchi wana matatizo chungu mzima kuna maboma ya madarasa yametelekezwa muda mrefu na Mbunge haonekani jimboni amebaki kuwashambulia viongozi wa serikali na kuhoji kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania,Dkt John Magufuli,”.
“Mbunge Mpina badala ya kuhangaika na matatizo ya wananchi anahangaika na sababu ya kifo cha Rais Dkt Magufuli,Mungu aliyetuumba ndiye anajua lini na saa ngapi atatuchukua.
"Unawasema Mawaziri hawafai lakini akumbuke alikuwa Waziri hata salamu kwa wananchi wake alikuwa hawezi kuwasalimia,alitusaidia nini sisi Wanasimiyu alipokuwa Waziri arudi jimboni kwake akatatue matatizo ya wananchi wake katika jimbo la Kisesa,”amesema.
Amesema kuwa Tembo wamekuwa wakivamia makazi ya watu katika jimbo hilo lakini mbunge huyo amekuwa kimya huku wananchi wakitaabika na wala haonekani jimboni na kufanya wananchi kubaki na matatizo na hivyo wananchi kuichukia serikali inayoongozwa na CCM.
Sehemu ya wanachama wa CCM katika Tarafa ya Kanadi wilaya ya Itilima mkoa wa Simiyu wakiwa katika Ukumbi wa shule ya Sekondari Langangabilili
“Mbunge akapambane na Waziri wa Malia Asili na Utalii huko maana tembo wanavamia makazi ya wananchi kwenye jimbo lake wanateseka lakini yeye anakwenda kupambana na mipango ya Mwenyezi Mungu anapoamua kumchukua mtu wake hili halikubaliki,”amesema.
Amesema CCM inapoteuwa wanachama wake na wakachaguliwa kwenda Bungeni ina lengo la kutatua matatizo ya wananchi na kuhakikisha changamoto za wananchi zinatatuliwa huku akisisitiza kuwa Mbunge akishirikiana na Mwenyekiti wa CCM mkoa kupambania maendeleo ya wananchi yatawafikia haraka sana.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsa Mohamed(mwenye miwani) akisikiliza kero za wanachama wa Chama hicho katika Tarafa ya Kanadi wilaya ya Itilima
Ameeleza kuwa wananchi wa jimbo la Kisesa wanasikitika sana kuona mbunge wao akihoji vitu ambavyo hawajamtuma badala ya kujikita kwenye siasa za kujenga jimbo kwa lengo la kuwatetea wananchi.
‘’Si uhame jimbo la Kisesa uende huko ili wananchi wa Kisesa wachague mwingine wa kuwaletea maendeleo nayasema haya kwa sababu nina uchungu, ulipewa Uwaziri, kipi kizuri ulichokifanya wewe kuanzia kwenye mkoa na wilaya yako husika, ni Mbunge anayeongoza hata kwa kutoshiriki vikao vya Chama, anaongoza hata kutokwenda kusikiliza wananchi wake’’
“Kila siku yuko kwenye Magazeti na Vyombo vya habari inasikitisha sana ,unakwenda kuhoji kifo cha mtu bungeni inasikitisha sana’’.amesema.
Mwenyekiti huyo ametolea mfano wa Mbunge wa Jimbo la Itilima, Njalu Silanga ambaye ni mchapakazi na anajituma kwa maslahi ya wana Itilima na anashughulikia maendeleo ya wananchi wa jimbo hilo na kuwasisitiza waendelee kumuunga mkono.
Awali Mkuu wa wilaya ya Itilima, Ana Gidarya amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imeweza kupeleka kiasi cha Shilingi Bilioni 50 katika wilaya hiyo kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo ya Miundo mbinu ya barabara,Maji,Elimu,Afya na Umeme.
Mkuu wa wilaya Itilima,Ana Gidarya akieleza jinsi serikali ilivyopeleka fedha sh bilioni 50 katika miradi ya Maendeleo wilayani humo
Post a Comment