HEADER AD

HEADER AD

PLAN INTERNATIONAL ILIVYOWAWEZESHA WASICHANA KUTOTEMBEA KWA MIGUU KWENDA SHULENI


Na Daniel Limbe, Geita

'Elimu ni ufunguo wa maisha', Msemo huu umekuwa na maana kubwa sana kwenye mafanikio ya maisha ya mwanadamu katika kukabiliana na changamoto,kutumia fursa za kimaendeleo sambamba na kubuni,kuibua na kutumia teknolojia mbalimbali kila uchao.

Hakuna ubishi kwamba mataifa makubwa duniani yamefika hapo yalipo kutokana na kuwekwa mkazo mkubwa katika suala zima elimu kwa wananchi wake.

Kutokana na ukweli huo, siyo ajabu ukisema elimu ndiyo silaha pekee inayowezesha watu kutumia vipawa vyao kuharakisha maendeleo ya jamii, katika kuvumbua, kuzalisha na kutumia teknolojia mbalimbali za kisasa, jambo linalo saidia chochea uchumi wa nchi.

Nchini Tanzania baadhi ya mikakati imekuwa ikiwekwa na mingine kutekelezwa ili kuhakikisha kunakuwa na jamii yenye uelewa na maarifa mapana yanayoendana na ushindani wa uchumi wa kidunia na hata nchi wanachama wa Afrika mashariki(EAC).

Ili kufikia malengo yaliyowekwa bado ipo haja kubwa kwa safari hiyo, kusafiri pamoja pasipo kuliacha nyuma kundi hata moja kwa kuwa manufaa yanayopatikana yanakuwa na faida kwa watu wote badala ya kubaguana.

Licha ya kwamba safari hiyo ilianza kitambo, lakini hapakuwa na usawa wa kupata elimu kwa kundi moja kutokana na mifumo mibovu ya kijamii pamoja na imani potofu zilizotokana na mila na desturi za mabibi na mababu.

Makala hii inajikita kulizungumzia zaidi kundi la wanawake, ambalo miaka ya nyuma halikupewa kipaumbele cha kupata elimu bora ukilinganisha na wanaume ambao ndiyo walionekana wanafaa kuliongoza kwa kila jambo.

Aidha kutokana na baadhi ya mataifa kuwapa fursa wanawake katika nyanja mbalimbali za kielimu, kiutamaduni na kijamii kisha kufanya vizuri, ndipo baadhi ya nchi ikiwemo Tanzania zilianza kidogo kidogo kuwaamini wanawake kuwapa fursa zinazostahili.

Mbali na fursa hizo, lakini bado hapajakuwa na usawa timilifu kutokana na kundi hilo kuendelea kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili, kiakili, kisaikolojia, kihisia, na hata kingono, huku baadhi ya watoto wa kike wakitendewa unyama ikiwemo kuzuiliwa kwenda shule kwa lengo la kuolewa na wengine kubebeshwa mimba katika umri mdogo.

Ili kukabiliana na hali hiyo, serikali kwa kushirikiana na taasisi zingine za maendeleo wamekuwa wakiweka msukumo mkubwa kwa jamii ili kuhakikisha ndoto za watoto wa kike zinatimia kwa kupata elimu stahiki na kuonyesha mchango wao katika uchumi wa taifa.

Miongoni mwa taasisi hizo ni pamoja na shirika la kimataifa la Plan International upande wa Tanzania, ambalo limekuwa likitoa elimu dhidi ya kulinda haki za watoto na kukemea ukatili kwa jamii ili kutokomeza vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikirudisha nyuma mikakati ya mtoto wa kike kujikomboa.

Mbali na jitihada za kupinga ukatili, pia limekuwa likiwawezesha vifaa mbalimbali baadhi ya watoto walioko kwenye kundi balehe wakiwemo wanafunzi wa kike wanaosoma shule za msingi na sekondari nchini.

Shirika la Plan lagawa Baiskeli

Katika kuhakikisha hatua zaidi zinapigwa ili kumwezesha mtoto wa kike kutimiza ndoto zake za kielimu,shirika la Plan International Tanzania limewagawia baiskeli 550 zenye thamani ya Tsh. Milioni 180, wanafunzi waliokuwa wakitembea umbali mrefu zaidi km 10 ili kufika shuleni.

    Mkuu wa mkoa wa Geita Marthine Shigela(aliyetega mgongo) akiwa na baadhi ya wanafunzi walionufaika na msaada wa baiskeli kutoka Shirika la kimataifa la Plan International Tanzania.

Baiskeli hizo ni miongoni mwa 2,200 zinazotarajiwa kutolewa kwa wanafunzi wengine ambao baadhi yao wamekuwa wakikwepa masomo kutokana na kutembea umbali mrefu ili kufika shuleni.

Hatua hiyo ni jitihada kubwa katika ukombozi wa elimu kwa mtoto wa kike, kutokana na wingi wa vikwazo anavyokumbana navyo akiwa nyumbani, mtaani, na hata shuleni.

Mkurugenzi wa miradi wa taasisi hiyo, Nicodemas Gachu, anasema msaada huo ni miongoni mwa vipaumbele vya taasisi hiyo katika kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu bora na kuwaepusha na vikwazo wanavyokutana navyo njiani wakati wa kwenda shule na kurejea nyumbani.

Anasema mpango huo unalenga kuwafikia wanafunzi wa kike wanaotoka katika mazingira magumu katika mkoa wa Geita na Kigoma ili kusaidia jitihada za serikali za kumwinua mtoto wa kike dhidi ya unyanyasaji aliokuwa akiupata siku za nyuma.

"Tumekuwa na miradi inayohusiana na afya, tumejenga vituo vya afya, tumejenga ufahamu juu ya mambo mbalimbali yanayohusiana na vijana walio katika kundi balehe pamoja na vijana wengine.

"Hata hivyo tunashirikiana na serikali kuhakikisha kwamba mtoto na haki zake zinalindwa, na kwamba tutaendelea kushirikiana katika kubuni na kuendeleza miradi mbalimbali kwa lengo la kuisaidia jamii"anasema Gachu.

Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na Mwandishi wa Habari wa chombo hiki  (majina tunayahifadhi) wamepongeza jitihada za mashirika na serikali kuhakikisha wanawawezesha kusoma pasipo vikwazo na kwamba hatua hiyo itakuza usawa wa kijinsia katika jamii.

Kadhalika wanasema baiskeli hizo zitaongeza chachu ya usomaji ukilinganisha na awali ambapo baadhi yao walikuwa wakifika shuleni na kukuta baadhi ya vipindi vimeshafundishwa hivyo kukosa haki ya kujifunza kikamilifu.

"Tunawapongeza sana hawa wahisani kwa msaada wa baiskeli hizi,tunaamini zitatusaidia kuwahi shuleni na pia kutuepusha na vishawishi vya kuomba rifti kwa mabodaboda na wenye magari ambao baadhi yao huturubuni ili kufanya nao vitendo vya ngono".

" Ni kweli kufanya ngono katika umri mdogo ni kosa kisheria lakini baadhi ya wanafunzi tunashindwa kujizuia kutokana na mazingira ya familia zetu kuwa maskini,unataka usome lakini nyumbani hupewi nauli wala pesa ya kula shule na bado unatembea umbali mrefu,kinachofuata ni kukubali vishawishi na hivyo kujikuta tunashindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya mimba" amesema mmoja wa wanufaika wa msaada huo.

Hellena Mathias,mkazi wa Nyankumbu, anasema elimu kwa mtoto wa kike ni muhimu sana hasa katika dunia ya sasa, lakini wasiwasi wake ni kwamba bado hayajawekwa mazingira mazuri ya kumnusurua mtoto wa kike na ukatili wa njiani na shuleni.

"Ujue vishawishi ni vingi sana kwa watoto wa kike, akitoka nyumbani salama huko mtaani vijana na watu wazima wanamuwinda, akinusurika mtaani shuleni nako siyo salama sasa hapo usawa utapatikana haraka kweli ?" anahoji Hellena.

Siwema John mkazi wa mkoani, anaona nyota inayong'aa kwa mtoto wa kike na kwamba ni muda wa kupambana ili kuufikia usawa ukilinganisha na wanaume kwa madai hakuna kisichowezekana iwapo mwanamke ataaminiwa na kupewa fursa.

"Zamani ilionekana mwanamke ni mtu wa kukaa nyumbani na kusubiri kuolewa, tulinyimwa elimu wakawa wanapewa wavulana pekee, lakini sasa tumeshaamka lazima tuufikie usawa wa kijinsia wa aslimia 50 kwa 50".

"Sisi wanawake ni jeshi kubwa na ukimwelimisha mwanamke umeelimisha jamii, sisi tumeshatoka kwenye unyonge sasa tunaweza ndiyo maana unaona hata rais wetu wa Tanzania ni mwanamke,Mama Samia Suluhu Hassan"anasema Siwema.

Anakazia kuwa mwanamke akipewa elimu ni rahisi zaidi kuyafikia maendeleo ya familia na jamii kwa ujumla kutokana na kwamba siyo mtu mwenye kupenda kujilimbikizia mali isipokuwa hupenda jamii yote ifaidike kupitia yeye.

"Tazama hata ripoti mbalimbali zinazotolewa nchini kuhusiana na ufisadi, ni wanawake wangapi wametajwa kujilimbikizia mali ukilinganisha na wanaume,ndiyo maana serikali ya awamu ya sita imeamua kuwaamini wanawake na kuwapa fursa mbalimbali za kiungozi"anasema Siwema.

Petro Nyanzenze,mkazi wa Katoro, anashauri jamii kuendelea kuwapa elimu wasichana bila kuwasahau wavulana kwa madai makundi yote hayo yanategemeana katika kuinua uchumi wa familia na Taifa kwa ujumla.

"Sifurahishwi sana na tabia ya wazazi kuwanyima haki ya elimu watoto wa kike kwa lengo la kuwaozesha ili kupata fedha za mahali au vinginevyo,elimu ni miongoni mwa haki za binadamu kwa hiyo kila mmoja anapaswa kupewa elimu tena iliyo bora" anasema Nyanzenze.

Mkuu wa mkoa wa Geita,Marthine Shigela anasema jamii inapaswa kuacha kumsumbua mtoto wa kike ili apate elimu,huku akitumia fursa hii kuwaonya baadhi ya wazazi na walezi wanaozuia elimu kwa watoto.
      Mkuu wa mkoa wa Geita,Marthine Shigela,akiwaasa wazazi na walezi walioshiriki katika hafra fupi ya kugawa baiskeli kwa watoto wanaotoka mazingira magumu mkoani humo

Anasema mikakati ya mkoa huo ni kukomesha mimba za utotoni kupitia Mamlaka mbalimbali za kiserikali na kijamii na kuhakikisha mtoto wa kike anasoma katika mazingira salama.

Shigela,anasema serikali haikubaliani hata kidogo kuona mtoto wa kike anashindwa kuendelea na masomo kutokana na vikwazo,ndiyo maana hata waliopata ujauzito na kujifungua bado wamepewa fursa ya kuendelea na masomo.

Anawapongeza sana wadau wa maendeleo mkoani humo zikiwemo taasisi za kimataifa ambazo zimekuwa bega kwa bega na serikali kuhakikisha malengo yanayokusudiwa yanafikiwa kwa kiwango cha hali ya juu.

Hata hivyo,anasema msaada wa baiskeli hizo kwa wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu, ulenge kuwanufaisha watoto wenyewe badala ya wazazi kuzitumia kwaajili ya kwenda kunywea pombe na kushindwa kuzifanyia matengenezo.

        Baadhi ya wanafunzi(wanufaika wa msaada) wakiendelea kupokea maelekezo mbalimbali kutoka kwa viongozi.

 Waziri wa Elimu

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, anasema Tanzania inajivunia kutekeleza kwa vitendo hatua za kuhakikisha mtoto wa kike anapata haki katika ngazi zote za elimu.

Akizungumza katika siku ya kimataifa ya mtoto wa kike Oktoba, 11, 2023 iliyofanyika Dodoma,
anataja baadhi ya mafanikio ambayo yamepatikana kwenye elimu kuwa ni pamoja na mpango wa kuwarejesha shule wanafunzi waliokatisha masomo wakiwemo wasichana.

Anasema kupitia mpango huo jumla ya wanafunzi wa kike 7,995 wamerejea shule kupitia mfumo rasmi na usio rasmi kwa lengo la kutimiza ndoto zao.

"Juhudi mbalimbali zilizofanyika Tanzania ni pamoja na kupitia Sera, Sheria na Nyaraka mbalimbali ili kuhakikisha watoto wote wakiwemo wa kike wanapata fursa sawa ya elimu"anasema Prof. Mkenda.

Anasema baadhi ya juhudi hizo ni kutungwa kwa sheria ya Haki ya mtoto ya mwaka 2009 na kutoa waraka wa Elimu namba 3 wa mwaka 2021 kuhusu urejeshwaji wa wanafunzi waliokatisha masomo katika elimu ya sekondari na msingi.

Kwa mujibu wa utafiti wa hali ya Afya ya Uzazi na Mtoto na viashiria vya malaria nchini ya mwaka 2022 umebainisha kuwa, mifarakano na migogoro katika familia imesababisha malezi duni na uangalizi hafifu wa watoto hususani watoto wa kike, hali iliyosababisha kuanza ngono katika umri mdogo na wengine kupata mimba za utotoni.

Utafiti huo unaonyesha aslimia 22 ya watoto wenye umri wa miaka 15 hadi 19 walipata ujauzito ikilinganishwa na aslimia 27 ya watoto wa umri huo kwa mwaka 2015/16 na kwamba kiwango cha mimba za utotoni vijijini ni kikubwa kwa zaidi ya aslimia 25 ukilinganisha na aslimia 16 mijini.

Kutokana na hali hiyo,Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na makundi maalumu, Dkt.Dorothy Gwajima anasema licha ya kwamba kiwango hicho ni kidogo lakini bado jitihada zinahitajika zaidi ili kuondoa kabisa tatizo la mimba za umri mdogo.

Aidha takwimu za Jeshi la polisi za mwaka 2021 zinaonyesha jumla ya matukio ya ukatili kwa watoto yaliyotolewa taarifa katika vituo vya polisi nchini ni 11,499, huku mikoa iliyoongoza ikiwa ni Arusha (808), Tanga (691), Shinyanga (505), Mwanza(500) na Ilala (489) na kwamba makosa yaliyoongoza kwa idadi ni matukio ya ubakaji (5,899), Mimba (1,677), Ulawiti (1,114), Kukatisha masomo (790) na Shambulio la mwili (390).

Aidha Takwimu za Elimu (BEST 2020) zinaonyesha kuwa jumla ya wanafunzi wa shule za msingi 1,135 na Sekondari 5,340 waliacha masomo kwa sababu ya ujauzito, Mikoa yenye namba za juu kwa mimba za utotoni kwenye shule za msingi ni Mwanza(98),Tanga(97), Ruvuma(84), Geita(78) na Morogoro(71) wakati kwenye shule za Sekondari ni Mwanza(491), Morogoro(389), Dodoma(381), Mara(369) na Ruvuma(327).

Hata hivyo Takwimu za Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2022 nchini, zinaonyesha kubwa idadi ya watoto walio chini ya umri wa 0-4 ni 9,484,170 huku watoto walio kati ya miaka 5-9 wakiwa ni 8,918,580 sawa na aslimia 42.76 ya watoto wote.

 Sheria ya Mtoto

Kwa mujibu wa sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009 kifungu cha 13(1) Mtu hatamsababishia mtoto mateso au aina nyingine ya ukatili, kumpa adhabu zisizo za kibinadamu au kumdhalilisha mtoto ikijumuisha mila na desturi zozote zenye madhara kwa mtoto kimwili au kiakili.

Ibara ya 12 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kifungu (1) Binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa, (2) Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.

Pia Ibara ya 13(1) Watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki, bila ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.
 
 Mkataba wa Kimataifa

Mkataba wa Kimataifa wa Haki ya Mtoto (UNCRC) unazitambua haki za watoto kwa marefu na mapana yake katika nyanja mbalimbali ambazo ni muhimu katika maisha ya binadamu.

Haki zote za mtoto zimewekwa kwenye makundi muhimu matatu (3) ambayo ni kundi la haki ya kulindwa, haki ya kupatiwa mahitaji na haki ya kushirikishwa ambapo ndani ya makundi haya matatu ndimo haki zote zimazowahusu watoto zimejumuishwa.

Mkataba huu umejikita katika misingi mikuu minne (4) ambayo ni kuyaweka mbele maslahi ya mtoto, kukomesha ubaguzi, kuzingatia maoni ya mtoto katika kufanya maamuzi dhidi ya mambo yanayomhusu pamoja na kukua,kuishi na kuendelezwa.

Kudumishwa kwa haki za mtoto ni kujenga jamii na taifa lenye raia wenye kuheshimiana, wenye uzalendo, fikra chanya, uendelevu, umoja na mshikamano.

Mkataba huo unaeleza kwamba, watoto wa kike wakithaminiwa, kuheshimiwa na kuendelezwa kingali wadogo, hukua na ustawi mwema hali inayowawezesha kuifurahia dunia na kuona ni mahali salama pa kuishi.

No comments