HEADER AD

HEADER AD

TAKUKURU KAGERA YAPOKEA MALALAMIKO 110


Alodia Dominick, Bukoba

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) mkoa wa Kagera kwa mwezi Januari hadi Machi, 2024 imepokea malalamiko 110, kati ya hayo malalamiko 96 yalikuwa hayahusu rushwa.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Kagera Pilly Mwakasege akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa leo Aprili 24, 2024 amesema kuwa, malalamiko 96 ambayo yalikuwa hayahusu rushwa walalamikaji walielimishwa na kupewa ushauri.

     Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Kagera Pilly Mwakasege akitoa taarifa ya miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi, 2024 kwa waandishi wa habari

Amesema kuwa, malalamiko 14 yalihusu rushwa na kufunguliwa majalada ya uchunguzi, kati ya majalada hayo 14 uchunguzi wa majalada 10 umekamilika na hatua mbalimbali za kisheria zinatarajiwa kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa na majalada manne uchunguzi wake bado unaendelea.

Mwakasege amezitaja idara zilizolalamikiwa katika halmashauri ni malalamiko 49, idara ya fedha 10, elimu 6, manunuzi 2, ardhi 10, Ujenzi 6, afya 7, utawala 6, kilimo na idara ya mifugo 2.

Ameeleza kuwa, taarifa nyingine 61 zilizohusu watu binafsi zilikuwa 21, TARURA tatu, Ushirika tano, polisi mbili, TFS mbili, RUWASA moja, TRA mbili, Uhamiaji tatu, sekta binafsi saba, BUWASA moja, NPS moja, Mahakama moja na Tanesco mbili.

Ameongeza kuwa, malalamiko yasiyohusu rushwa yamekuwa mengi kutokana na kuongezeka kwa malalamiko ya madai baina ya wananchi, hivyo wananchi wanaodaiana wao kwa wao walishauriwa kufuata utaratibu wa madai kwa kujibu mikataba yao ya kukopeshana.

Aidha ameeleza kuwa mashauri mapya nane yamefunguliwa mahakamani na kufanya jumla ya mashauri yanayoendelea kusikilizwa mahakama mbalimbali mkoani Kagera kuwa 27, katika kipindi hicho mashauri tisa yamefanyiwa maamuzi na Jamhuri imeshinda mashauri yote tisa.

Hata hivyo, Taasisi hiyo imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 24 yenye thamani ya shilingi bilioni 9.2 miradi hiyo ni ujenzi wa miundombinu ya maji, Zahanati, barabara, vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, bwaro na mabweni katika shule za msingi na sekondari.

No comments