AGREY MWANRI AELEZA SABABU YA UZALISHAJI MDOGO ZAO LA PAMBA
Na Samwel Mwanga, Maswa
BALOZI wa Pamba Tanzania, Agrey Mwanri amesema kuwa uzalishaji mdogo wa zao la pamba kwa hekari unasababishwa na baadhi ya viongozi ambao hawatimizi wajibu wao katika kusimamia wakulima wa zao hilo kulima kwa kufuata sheria na kanuni zinazoongoza kilimo cha zao hilo.
Mwanri amesema hayo Mei, 13 mwaka huu wilayani Maswa mkoani Simiyu katika kikao kazi maalum cha kujengeana uwezo kilichowakutanisha Maafisa watendaji wa Kata, Maafisa watendaji wa Vijiji, Maafisa Ugani, Viongozi wa Vyama vya Msingi wa Ushirika(AMCOS)na baadhi ya watumishi wa serikali ngazi ya halmashauri ya wilaya hiyo.
Balozi wa Pamba Tanzania,Agrey Mwanri akizungumza na watendaji wa Kata,Vijiji,Maafisa Ugani,Viongozi wa AMCOS na viongozi wa wilaya ya Maswa katika Ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo mji Maswa juu ya kilimo bora cha zao la pamba.
Amesema kutowajibika kwa baadhi ya viongozi ndiko kunasababisha wakulima wa zao la pamba kulima kiholela bila kufuata kanuni zinazoongoza zao hilo na hivyo kusababisha uzalishaji kuwa mdogo kwa hekari ukilinganisha na nchi nyingine duniania zinazolima zao hilo.
“Wakati mwingine kutowajibika kwenu vizuri kunapelekea wakulima kulima kiholela, zao la pamba lipo kwa mjibu wa sheria za nchi na sio kienyeji sheria Na. 2 ya mwaka 2001 na ile ya 2011 zilitungwa kanuni 10.
" Moja wapo ya kanuni inamtaka kila mkulima kung’oa na kuchoma maotea yote ya msimu uliopita ili kuua wadudu waharibifu kuhamia kwenye msimu uliopo , kupanda kwa msitari pamoja na kupulizia dawa ya kuuwa wadudu,” amesema.
Ameongeza kuwa katika mkoa wa Simiyu ikiwemo wilaya hiyo bado kunauelewa mdogo juu ya kulima kilimo chenye tija jambo lililopelekea waanzishe kuwepo mkulima mwezeshaji ambae atakuwa ni chambo kwa wakulima wengine, kutoa elimu ya kutosha huku akiwaasa viongozi wawe mfano katika zao hilo kwa kwa kufanya hivyo kutainua na kuongeza pato la mtu mmoja na taifa ikilinganishwa na musimu uliopita.
Baadhi ya Maafisa watendaji wa Kata,Vijiji,viongozi wa Amcos na viongozi wa wilkaya ya Maswa wakiwa kwenye kikao cha Balozi wa pamba Tanzania,Agrey Mwanri kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo.
“Tatizo lililopo katika halmashauri zetu zinazolima pamba la kwanza ni uelewa mdogo wa wananchi wetu kuhusu nini wanachokabiliana nacho sasa uzalishaji wetu ni kiduchu hapa naomba Mkuu na wanasemina mnisikilize vizuri.
" Bukinafaso wanapata kilo 2500, Benin wanapata kilo 2500, Misri wanapata kilo 2500 kwa hekari moja na wako kwenye project ile ya Brazil ambayo imetusaidia ya 60 kwa 30.
“ Lakini nenda kaulize mkulima wa kwetu hapa Simiyu, nenda Bariadi na hasa kule wilaya ya Meatu ambayo inaongoza kwa uzalishaji wa zao la pamba hapa nchini, lakini anayeongoza kwa uzalishaji ni kilo 200 kwa hekari moja ni aibu anayefuata kilo 150, anayefuata kilo 100 na anayefuata kilo 50 sasa nenda kamuulize huyu wa kilo 50 atakwambia amelima hekari tano tuseme polepole tusije tukachekwa,”amesema.
Amesema kuwa katika musimu wa kilimo unaokuja wa mwaka 2024/2025 wameanza mapema kuhakikisha kilimo cha zao hilo kinalimwa kwa tija hivyo kupitia bodi ya pamba wameweza kununua matrekta 200.
Baadhi ya viongozi wa AMCOS wilaya ya Maswa waliohudhuria kikao cha Balozi wa Pamba Tanzania,Agrey Mwanri katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo.
Matrekta hayo ni kwaajili ya kuweza kuwasaidia wakulima katika kilimo pamoja na kuleta vifaa vya kupulizia dawa zikiwemo ndege nyuki hivyo amewaomba viongozi hao kuhakikisha wanalisimia zao la pamba kwa nguvu zote kwenye maeneo yao.
Amesema kuwa serikali ilianzisha Program ya Ijenga Kesho iliyo Bora (BBT)na kwa sasa vijana hao wako katika maeneo mbalimbali hapa nchini ambapo pia kwa musimu ujao wa kilimo watasaidia katika kuhakikisha zao la pamba linalimwa kwa kufuata kanuni bora za zao hilo na kuomba wapewe ushirikiano huko kwenye maeneo yao ambayo watayafanyai kazi.
Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge amesema kuwa zao la pamba ni muhimu kwa wilaya ya Maswa kwani katika musimu uliopita Halmashauri ya wilaya hiyo imekusanya zaidi ya Tsh. Bilioni moja kwa ajili ya ushuru wa zao hilo hivyo asilimia 75 ya makusanyo ya halmashauri hiyo inategemea zao hilo.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge akizungumza katika mkutano wa Balozi wa pamba Tanzania,Agrey Mwanri katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo uliopo mjini Maswa.
Amesema kuwa kwa msingi huo sasa ni wakati kwa viongozi wa wilaya hiyo kuanzia ngazi ya kijiji hadi wilaya kuhakikisha wanalisimamia zao hilo kwa akili zao, uwezo wao na nguvu zao kwa kutoa elimu kwa wakulima ili waweze kuzalisha pamba kwa wingi kwa hekari moja kwani wana uwezo wa kufikisha kilo 2500 kwa hekari moja.
“Halmashauri imepokea zaidi ya T.Sh Bilioni moja nukta sifuri kutokana na ushuru wa zao la pamba, inamana ndiyo kusema asilimia 75 ya makusanyo ya mapato ya halmashauri yanatokana na kilimo cha pamba!.
" Kama sisi ni watumishi wa halmashauri wa serikali tunahitaji kutumia akili zetu zote na nguvu zetu kuhakikisha uzalishaji wa pamba unapanda kama ambavyo anasisitiza Balozi wa pamba na anapoondoka kazi yetu ni kutoa elimu kwa wakulima wa zao la pamba inaendelea,” amesema.
Awali Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wilaya ya Maswa, Robert Urasa akisoma taarifa ya utekelezaji wa zao la pamba kwa msimu wa mwaka 2023/2024, amesema kuwa wilaya hiyo ilitenga kulima hekta 60,438 ya zao hilo hadi kufikia Aprili 30 mwaka huu waliweza kulima hekta 48,986.8 sawa na asilimia 81.05 na kufanikiwa kuvuna tani 22,044.06 lakini malengo yao yalikuwa tani 60,438.
Mkuu wa Divisheni ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi wilaya ya Maswa,Robert Urasa akitoa taarifa kwa Balozi wa Pamba Tanzania,Agrey Mwanri(hayuko pichani)juu ya utekelezaji wa zao la pamba katika wilaya hiyo kwa musimu wa mwaka 203/2024
Amesema kuwa walishindwa kufikia malengo yao kutokana na kuwepo kwa changamoto mbalimbali zikiwemo uwepo wa mvua nyingi, kutostawi vizuri kwa zao la pamba na uwepo wa mlipuko wa wadudu waliovamia zao hilo likiwa shambani.
Post a Comment