FCC WAPATIWA MAFUNZO YA MASOKO YA UCHUMI, BIASHARA KWA NJIA YA MTANDAO
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WATUMISHI wa Tume ya Ushindani (FCC) wamepatiwa mafunzo maalum ya kidijitali juu ya kuendesha masoko ya uchumi na biashara kwa njia ya mtandao.
Mafunzo hayo ya siku moja, yamefanyika katika ofisi ya FCC Dar es Salaam, Mei 13, 2024 yametolewa na kampuni ya Kimataifa ya masuala ya masoko na ushauri ya Novelty Analysis Consultants chini ya wataalamu wake, Rafael Mazer na Wang’ombe Kairuki ambaye pia aliwahi kuwa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya ushindani nchini Kenya yaani Competition Authority of Kenya (CAK).
Awali akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi mkuu wa FCC , William Erio amesema mafunzo hayo yanalenga kuongeza ujuzi wa wafanyakazi wake wa tume katika nyanja za majukwaa ya kidijitali na sera ya ushindani.
‘’Mpango huu wa mafunzo ni muhimu kwani yanaenda kuwajenga watumishi wetu katika mazingira ya kisasa. Teknolojia za kidijitali zimekuwa muhimu kwa maisha yetu ya kila siku, na kuleta mapinduzi katika sekta mbalimbali zikiwemo sayansi, mawasiliano, huduma za afya, fedha, na mengine mengi.
"Kupitia mafunzo haya, Wamewezesha ushirikishwaji wa kifedha, kurahisisha huduma za serikali, na kutoa njia za kupata huduma mbalimbali ndani na nje ya nchi.’’ Amesema William Erio.
Amesema Tanzania imeshuhudia kasi ya kubwa ya mabadiliko ya kidijitali ambapo amewasisitizia namna ya changamoto ya kidijitali ikiwemo masuala kama vile habari potofu na habari zisizo sahihi, ambazo mara nyingi huenezwa na watu wasio waaminifu, huwa tishio kubwa kwa watumiaji, na kusababisha hasara za kifedha na mmomonyoko wa uaminifu.
‘’Ulimwengu wa kidijitali umeanzisha aina mpya za ukiukaji wa sheria za ushindani, na hivyo kuhitaji kutathminiwa upya kwa mikakati yetu ya utekelezaji. Vile vile, mabadiliko ya kidijitali yameleta njia mpya za ukiukaji wa sheria za ushindani kama vile cartel.
"Kama FCC, iliyopewa mamlaka ya kulinda ushindani katika uchumi wa Tanzania na haki za walaji, ni muhimu kwetu kupunguza changamoto hizo na kuwawajibisha wahusika kwa matendo yao.
Hili linahitaji mbinu makini katika kugundua na kupunguza utovu wa nidhamu, na hivyo kulinda ustawi wa raia.’’ Amesema William Erio.
Mafunzo hayo yamegusa maeneo mbalimbali ikiwemo Utalii, benki, mitandao ya simu na biashara mbalimbali huku yakiangaia uelewa wa watu wa mjini na kijijini katika kuuza upatikanaji wa masoko kwa njia ya kidijitali.
Post a Comment