HEADER AD

HEADER AD

CCM SIMIYU : VIONGOZI WA MASHINA NI WATU MUHIMU NDANI YA CCM WAHESHIMIWE

Na Samwel Mwanga, Bariadi

DHAMIRA ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kinachoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye ni rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Mabalozi wanakuwa mstari wa mbele katika kukiinua Chama.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM)mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed wakati akizungumza mwezi Mei, 2 mwaka huu na Viongozi wa CCM ngazi mbalimbali.

     Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsa Mohamed akizungumza na Viongozi wa chama hicho wa Tarafa ya Ntuzu wilaya ya Bariadi kwenye ukumbi wa Shule ya sekondari Alliance mjini Bariadi

Viongozi hao kuanzia ngazi ya mashina hadi Kata katika Tarafa ya Ntuzu wilaya ya Bariadi kwenye mkutano wa ndani uliofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Baraidi Alliance ambapo amesema kuwa anatambua ukubwa wa nafasi ya Balozi na Shina ndani ya chama hicho.

Amesema kuwa mabalozi wanapaswa kuheshimiwa ndiyo wenye wanachama huko kwenye maeneo yao hivyo hawapaswi kidharauliwa na ndiyo wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi katika nafasi zote za kuchaguliwa kwa kuwashawishi wapiga kura kuchagua wagombea wa CCM.

"Mie ni Mwenyekiti wa CCM mkoa lakini nimeweka heshima kubwa kwa mabalozi sababu najua mabalozi ndio msingi wa shina la CCM na ndio maana tumeelekeza nguvu kubwa kuhakikisha viongozi wote wa CCM wanatambua hakuna viongozi wakubwa zaidi ya mabalozi.

"Na kwa mantiki hiyo chama kinarudi kwa wanachama na sisi viongozi  tunaochaguliwa wanachama hawa ndiyo maboss wetu na ndiyo maana mnamuona hapa mbele ya meza kuu yupo balozi, "amesema.

Amesema kuwa mabalozi ni viongozi muhimu katika kukijenga chama hicho na amewasihi kuendelea kukitumia kwa moyo wote huku akiwapongeza kwa kufanya kazi yao vizuri ya kukisimamia na kushiriki kikamilifu katika shughuli za chama.

      Sehemu ya Viongozi wa CCM katika Tarafa ya Ntuzu wilaya ya Bariadi wakiwa kwenye ukumbi wa Shule ya sekondari Alliance mjini Bariadi kumsikiliza Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsa Mohamed   

Amesema katika mikutano yake ya kusikiliza kero anawapatia kipaumbele mabalozi hao ambao ndiyo wenye wanachama kuanzia ngazi ya shina.

Pia amewataka viongozi hao wa CCM kufanya vikao vya kamati ya siasa katika maeneo yao na pia kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho ili waweze kuwaeleza wananchi fedha ambazo zimeletwa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan.

“Mwenyekiti wa tawi ana nguvu sawa na Mwenyekiti wa CCM mkoa na anatakiwa kufanya kazi za utekelezaji wa Ilani kama wanavyofanya viongozi wa wilaya na mkoa kuisimamia serikali kwenye maeneo yao maana miradi mingi ya maendeleo inatekelezwa huko na fedha nyingi zinapelekwa huko kazisimamie,”amesema.

Pia amewataka viongozi hao kujiandaa na kuhakikisha wanashinda chaguzi zinazokuja za Serikali za Mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025 kwa nafasi za Wenyeviti wa Vitongoji, Mitaa na Vijiji kwa serikali za mitaa na Madiwani,Wabunge na Rais katika Uchaguzi Mkuu.

“Tutahakikisha kuwa tutasimamisha wagombea wanaokubalika katika jamii ili CCM iweze kushinda katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu na kuendelea kushika dola na kuwaletea maendeleo wananchi,”amesema.

Naye Balozi Jacobo Suki wa Shina la Somanda, tawi la Butiama mjini Bariadi amesema kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu amewaheshimisha mabalozi wa chama hicho na ndiyo maana leo ameteuliwa kuongoza kikoa hicho.


Amesema kuwa kwa sasa ni vizuri mabalozi wakatembea kifua mbele kwani wanatambuliwa na kuthaminiwa na kiongozi wa juu wa chama hicho katika mkoa huo na amehaidi kwa niaba ya wenzake kufanya kazi za kuimarisha chama hicho.

“Kwa niaba ya mabalozi wote mlioko katika mkutano huu jisikieni nyote mko jukwaa kuu kwa heshima hii niliyopewa na Mwenyekiti wa CCM kuwa huku inaonyesha wazi kuwa anatuthamini na mimi nikuhaidi na mabalozi wenzangu tutafanya kazi kwa moyo ili kukijenga chama chetu,”amesema.

Mkutano huo uliojumuisha Viongozi mbalimbali wa Chama , Serikali, Dini na Wazee katika tarafa ya Ntuzu ikiwa ni mwendelezo wa Ziara ya mwenyekiti huyo kutembelea Tarafa zote za mkoa huo na kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

      Balozi wa CCM,Jacobo Suki wa Shina la Somanda,tawi la Butiama mjini Bariadi mkoani Simiyu akifungua Mkutano wa Viongozi wa Tarafa ya Ntuzu  uliohitishwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa huo,Shemsa Mohamed

No comments