HEADER AD

HEADER AD

DKT. MPANGO AZINDUA KAMPENI 'MTU NI AFYA'


Na Gustaphu Haule, Pwani

MAKAMU wa Rais Dkt. Philip Mpango amezindua kampeni ya awamu ya pili  ya 'Mtu ni Afya'kwa kuzitaka Halmashauri zote nchini kuwatumia vizuri wahudumu wa afya wa ngazi za jamii ili hiwe rahisi kuwafikia Wananchi.

Dkt . Mpango ametoa kauli hiyo Mei, 09 mwaka huu wakati akizindua kampeni hiyo katika viwanja vya stendi ya zamani vilivyopo katika Halmashauri ya Mji Kibaha Mkoani Pwani.

Amesema kuwa kampeni ya mtu ni Afya awamu ya kwanza  ilianza mwaka 1973 na mpaka sasa imetimiza miaka 50 na kwamba awamu ya pili anayozindua itadumu mpaka mwaka 2030.

     Makamu wa Rais Dkt .Philip Mpango akizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya Mtu ni Afya awamu ya pili iliyofanyika Mei, 9 ,2024 katika viwanja vya stendi ya zamani Kibaha Mailimoja Mkoani Pwani.

Amesema kampeni ya awamu ya kwanza imefanikiwa kwa kiwango cha kuridhisha na kwamba moja ya mafanikio hayo ni kutokomeza  ugonjwa wa Ndui ambapo hata hivyo kampeni hiyo ilikuwa ikiendeshwa kwa kutumia kauli mbinu mbalimbali ikiwemo 'Nyumba ni Choo'.

Mpango ameongeza kuwa kampeni ya awamu ya pili aliyoizindua jana inalenga magonjwa yasiyoambukizwa ukiwemo ugonjwa wa kisukari shinikizo la damu  na hata magonjwa mengine.

Amesema kuwa,mwaka 1980 ugonjwa wa kisukari ulikuwa kwa kiwango cha asilimia Moja na kwasasa imefikia asilimia Tisa wakati ugonjwa wa shinikizo la damu  awali ilikuwa asilimia tano lakini kwasasa imefikia asilimia 25 kati ya watu 100.

Mpango,ameongeza kuwa katika kampeni hii ya awamu ya pili kila mtu anawajibu kushiriki hususani katika kuhakikisha nyumba zinazojengwa zinakuwa na vyoo Bora katika kaya na hata katika Shule za Msingi na Sekondari kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni .

        Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango akizindua kampeni ya Mtu ni Afya iliyofanyika Mei, 9 katika viwanja vya stendi ya zamani Mailimoja Kibaha Mkoani Pwani

Mbali na hayo lakini Dkt.Mpango amesisitiza kutibu maji ya kunywa Kwa kuchemsha,hedhi salama kwa watoto wakike kuboresha mifumo ya maji taka ,elimu ya lishe kwa watoto, usafi wa mazingira pamoja na kutoa elimu ya mabadiliko ya tabia ya nchi na athari zake kimazingira.

Aidha Makamu wa Rais amezisisitiza Wizara ya Afya na Tamisemi kuhakikisha wanaziwezesha idara za afya za Miji ,Manispaa ,Jiji na Wilaya ili ziweze kukabiliana na magonjwa ya milipuko kwa njia rahisi pamoja na kujenga uwezo wa kufanya utafiti kwa magonjwa mbalimbali ya milipuko.

Msisitizo mwingine ni kujenga uwezo wa usimamizi wa kampeni hiyo  pamoja mamlaka za Serikali za Mitaa kuimarisha mifumo ya kuondosha maji taka nyumbani pamoja kuhakikisha wanatenga maeneo maalum ya utupaji taka hizo.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kuwa kampeni awali iliongezewa nguvu katika kipindi cha mwaka 2012 /2015 na kwamba 2016 /2020 ilizinduliwa Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan ikiwa ni kampeni maalum ya masuala ya afya na usafi wa mazingira.

         Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya Mtu ni Afya iliyofanyika Mei, 9 katika viwanja vya stendi ya zamani Mailimoja Kibaha Mkoani Pwani.

Mwalimu amesema kuwa kampeni ya awamu ya  pili mpaka sasa imepata ufadhili kutoka Shirika la Afya Duniani na Shirika la  Kimataifa la Unicef na itafanyika kwa awamu mbili tofauti ikiwemo kutoka Juni  2024 mpaka Juni 2025 na kutoka Juni 2025   mpaka Juni 2030.

Katika kuhitimisha miaka 50 ya awamu ya kwanza ya kampeni hiyo Mkoa wa Iringa umeibuka mshindi wa jumla wa kupata gari mpya aina ya Land cruiser ambapo sababu za ushindi huo ni kutokana na utekelezaji wa mpango wa vyoo bora majumbani na Shuleni.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa Mkoa wa Pwani upo salama licha ya kuwepo kwa matukio ya mafuriko katika Wilaya ya Kibiti na Rufiji sambamba na nyumba 994 kuharibiwa kutokana na Kimbunga Hidaya.

   Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya Mtu ni Afya awamu ya pili iliyofanyika Mei, 9 katika viwanja vya stendi ya zamani Mailimoja Kibaha Mkoani Pwani.

Kunenge amesema kuwa Mkoa wa Pwani mpaka sasa kuna vituo vya huduma ya afya 473 huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Kunenge amesema kuwa tangu Rais Samia aingie madarakani tayari mpaka sasa Mkoa umepokea kiasi cha fedha Trilioni 1.29 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

    Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na kamati ya Ulinzi na salama ya Mkoa wa Pwani mara baada ya uzinduzi wa kampeni ya Mtu ni Afya awamu ya pili iliyofanyika Aprili 9 ,2024 katika viwanja vya stendi ya zamani Mailimoja Kibaha Mkoani.

No comments