JELA MIAKA 12 KWA KUJIFANYA ASKARI POLISI
Na Samwel Mwanga, Maswa
MAHAKAMA ya Wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu, imemhukumu Alex Nangale (24) mkazi wa Mtaa wa Sokoni mjini Maswa wilayani humo kwenda jela miaka 12 baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya kujifanya Askari Polisi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Hukumu hiyo imetolewa Mei, 30, 2024 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Enos Misana katika kesi ya jinai namba 45/2023 baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka mahakamani hapo na kuthibitisha makosa ambayo mshitakiwa alishitakiwa nayo.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha mashtaka kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wilaya ya Maswa, Mkaguzi wa Polisi ,Vedastus Wajanga amesema kuwa mshitakiwa huyo alikuwa akikabiliwa na makosa manane.
Ameeleza kuwa mahakama hiyo kuwa Machi 7,2023 katiika Mtaa wa Sokoni mjini Maswa,Mshitakiwa alijitambulisha kwa jina la Amos Malimi kuwa ni Askari Polisi na yupo kitengo cha Upelelezi wa makosa ya jinai na kuanzia hapo hadi Machi 31,2023 alikuwa akiomba pesa kutoka kwa Muhanga(jina linahifadhiwa)kwa kutumia utambulisho huo na kujipatia kiasi cha fedha Sh1,740,000
Mwendesha Mashitaka, Wajanga amesema kuwa kosa la kwanza la Mshitakiwa likiwa ni kujifanya askari Polisi kinyume na kifungu cha 369 (1) (2) na makosa saba yote ni kujipatia fedha kwa njia udanganyifu kinyume cha kifungu 302 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022 .
Amesema kuwa taarifa zilifika kituo cha polisi wilaya ya Maswa ambapo mshtakiwa alikamatwa na kukiri kutenda makosa hayo na baada ya upelelezi kukamilika mshtakiwa alifikishwa mahakamani na jumla ya mashahidi wanne na vielelezo vinne vilitolewa na upande wa mashtaka.
Baada ya mshitakiwa kutiwa hatiani upande wa mashtaka uliomba mshitakiwa apewe adhabu kali ili iwe funzo kwake na kwa jamii kwani makosa ya watu kujifanya askar polisi au watumishi wa serikali pamoja na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu yanaongezeka katika jamii ikizingatiwa kuwa mshtakiwa ni kijana mwenye nguvu ambae anaweza kutafuta kipato chake halali .
Pia amesema kuwa makosa kama haya huchafua taswira ya taasisi husika na jamii inakoswa imani na jeshi la Polisi kwa tabia na vitendo alivyovifanya mshtakiwa.
Mahakama baada ya kumkuta na hatia mshitakiwa aliiomba impunguzie adhabu kwani ni mkosaji wa mara ya kwanza na anafamilia inamtegemea.
Hata baada ya utetezi wake huo Mahakama hiyo ilimhukumu adhabu ya miaka mitano jela kwa kosa la kujifanya askari Polisi na miaka saba kwa makosa ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakiwa kulipa fidia ya Sh 1,740,000 kwa Muhanga.
Post a Comment