KAGERA KUANZISHA MASHAMBA YA PAMOJA YA KAHAWA HEKTA 4000
Na Alodia Dominick, Bukoba
MKOA wa Kagera unatarajia kuanzisha mashamba ya pamoja ya kahawa zaidi ya hekta 4,000 lengo likiwa ni kuondoa umaskini kwa wananchi wa mkoa huo.
Hayo yamebainika katika mkutano wa wadau wa kahawa uliofanyika Mei, 29, mwaka huu katika ukumbi wa mkuu wa mkoa huo.
Akifungua mkutano huo mkuu wa mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa amesema kuwa, kuanzishwa kwa mashamba ya pamoja ya kahawa ni agizo la Wizara ya Kilimo la hivi karibuni kwa bodi ya kahawa Tanzania (TCB) kuhakikisha inatoa matrekta na Wizara kutoa miche ya mibuni zaidi ya milioni 5.
"Dhamira ya serikali ni kupanua kilimo cha kahawa, sote tunayo kumbukumbu kahawa ilivyokosa bei wakulima wengi walikata miche ya kahawa hivyo mashamba mengi yana miche michache ya kahawa na tunao uwezo wa kuzalisha mara mbili ya kahawa tuliyo nayo katika mkoa wetu wa Kagera"
"Tukifanya hivyo hata ile ya kutajwa tajwa eti sisi ni wa pili kutoka mwisho kwa umaskini itaisha tutakuwa tunashikilia namba 10 bora za uchumi Tanzania.
"Sisi kama mkoa tukishirikiana na wizara ya kilimo tumeamua kufungua mashamba ya pamoja ya kahawa kwa mwaka huu tunaenda kuanzisha hekta 4,000 wilaya za Karagwe na Muleba ili kufikia mwaka 2030 mkoa wa Kagera umaskini usiwepo tena" amesema Mwassa
Aidha amesema baada ya kuanzishwa kwa mashamba hayo watakuwa wanakata hekali mbili wanagawia wakulima na wale watakaohitaji hekali zaidi watapatiwa.
Katibu Tawala mkoa wa Kagera Steven Ndaki amesema mkoa wa Kagera ndiyo mkoa wa kwanza Tanzania kwa uzalishaji wa zao la kahawa kwa mwaka huzalisha tani 60,000 hadi tani 80,000 ingawa uzalishaji huo unakumbwa na changamoto mbalimbali.
Changamoto hizo ni pamoja na utoroshaji wa kahawa ambapo baadhi ya wananchi wanalazimika kuivuna kahawa kabla ya wakati na kusababisha ubora wa kahawa kushuka.
Ametaja lengo la kikao hicho kuwa ni kujadili fulsa, mafanikio na changamoto na mwisho watoke na mkakati utakaowezesha kudhibiti ubora, kuongeza tija na kuimarisha mfumo wa masoko wa zao hilo.
Baada ya wadau wa kahawa kujadili kwa undani wametoka na maazimio kwa kila halmashauri kuweka mikakati ya kuzuia biashara ya magendo ya kahawa bila kutumia nguvu ili kulinda mapato ya wakulima pamoja na serikali, halmashauri za Karagwe na Muleba zitenge maeneo kwa ajili ya kilimo cha kahawa.
Maazimio mengine ni kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya uvunaji wa kahawa mbichi na utoroshaji wa kahawa, msimu wa ununuzi wa kahawa ufunguliwe mapema mwezi aprili ili kuwezesha ununuzi wa kahawa aina ya arabica na kuzuia magendo, kuongeza tija na ubora wa kahawa.
Pia Amcos ziwezeshwe kuweka mikakati ya kuwakopesha wakulima mapema kabla ya kuvuna ili kudhibiti biashara ya kahawa changa ikiwa bado shambani (obutura), mikutano ya wadau wa kahawa ngazi ya mkoa ihuishwe na wajumbe wote kutoka maeneo ya uzalishaji washirikishwe.
Azimio lingine , Serikali iwekeze kikamilifu kwenye mialo, beria na mikapani kwa kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama katika kudhibiti utoroshaji wa kahawa.
Post a Comment