MKUTANO WAAHIRISHWA BAADA YA KUKOSEKANA MUHTASARI WA 2019 MRADI WA MAJI NYANDUGA
CCM Tawi la Nyanduga wamwagiza Mtendaji wa Kijiji, RUWASA kuhakikisha muhtasari unapatikana
>> Yachachamaa baada ya vitongoji viwili kukosa maji licha ya Serikali kutoa Milioni 111
RUWASA yasema yaishe yapeleka mabomba vitongoji visiyo na maji
Na Dinna Maningo, Rorya
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Nyanduga, Kata ya Koryo, wilayani Rorya mkoa wa Mara, kimeshindwa kufanya mkutano wa kijiji Nyanduga baada ya kubainika kutokuwepo muhtasari wa mchakato mzima wa bajeti ya ukarabati wa mradi wa maji wa mwaka 2019/2020 kijiji cha Nyanduga.
Ni baada ya kuwepo utata wa matumizi ya fedha Tsh. Milioni 111 za mradi wa ukarabati wa maji na usambazaji wa maji zilizotolewa na serikali ambapo vitongoji viwili vya Masangura na Mirare havijasambaziwa maji huku mradi huo unaofanya kazi ukiwa bado hujakabidhiwa.
Chama hicho cha Mapinduzi kilifanya kikao na uogozi wa serikali ya Kijiji na RUWASA kwa lengo la kupata mrejesho wa ukarabati wa mradi huo wa maji kisha ufanyike mkutano wa wananchi ili serikali ya kijiji na RUWASA wawaeleze wananchi hatua zote za mradi tangu ulipoanza mwaka 2019 hadi kukamilika lakini wameshindwa kufanya mkutano kwakuwa hakuna muhtasari ambao ungewarejesha kwenye rejea ya mradi.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Tawi la Nyanduga Joshua Olala amesema " Juzi kati nimempigia simu Mtendaji wa kijiji nikamwambia tuna mkutano waandae taarifa ya maji waliyokaa na RUWASA tutakuwa na kikao cha wananchi ili wawaambie kilichofanyika kwenye mradi.
"Pia tujiridhishe yaliyohainishwa kwenye muhtasari wa awali wakati wa uanzishwaji wa mradi je ndio yametekelezwa ?. Lakini hajaja na faili wakati mafaili yote yanakaa ofisini hayahami, kwanini anashindwa kutoa muhtasari tumeahirisha mkutano wa wananchi hadi watakapotuletea muhtasari wa maji wa 2019" amesema.
Katibu wa CCM Tawi la Nyanduga , Jacob Matara amesema kuwa mradi huo umekuwa na mashaka kwani wamewahi kwenda kulalamika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Rorya mwaka 2023 kuhusu RUWASA kutosambaza maji katika kitongoji cha Masangura na Mirare lakini pia mradi kuanza hadi kukamilika bila Serikali ya kijiji na wananchi kushirikishwa katika hatua zote za mradi.
Emmanuel Ojwang mkazi wa Nyanduga amesema mradi huo tangu uanze kujengwa 2019 na kutakiwa kukalimika 2020 umekaa muda mrefu bila kukabidhiwa Serikali ya kijiji na wananchi.
"Chama kimeleta watu wa RUWASA ili kutoa ufafanuzi maana imebainika RUWASA hawakuja na muhtasari wa kikao kilichopita wakati wa utambulisho wa mradi, wakaona ni bora mkutano uhairishwe hadi watakapoleta muhtasari wa bajeti ya mradi.
" Ule muhtasari ndio dira au picha ya kuweza kutuongoza kujadili ajenda kwa upana wake, mkutano umeahirishwa maana wananchi wana maswali mengi kuhusu huo mradi hivyo muhtasari ni muhimu uletwe " amesema Emmanuel.
Mwananchi wa Nyanduga John Tagaya amesema " Mwenyekiti wa kijiji hairisha mkutano iambie ofisi yako iende itafute muhtasari, ule ndio dira kuwa awali tulipanga hivi je tuliyopanga yametekelezwa ? je mabomba yamewekwa inavyohitajika?.
" Kama bomba lilitengenezwa moja kwanini lingine halijatengenezwa wakati lilikuwa kwenye muhitasari wa awali wakati mradi unaanzishwa , tuone BOQ " amesema.
Mjumbe wa Serikali ya kijiji cha Nyanduga Musa Okoko amesema kuwa Serikali ya kijiji walikubaliana na RUWASA kuwa fedha zitakapoingia kwenye akaunti na ujenzi kuanza watoe mrejesho kila hatua lakini haikufanyika hivyo na kamati ya ujenzi haikushirikishwa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyanduga Andere oyier amesema lengo la kikao hicho kati ya Chama, Serikali na RUWASA kilikuwa ni kubaini mapungufu ambayo yapo kwenye utekelezaji wa mradi wa RUWASA kuhusu maji katika kijiji cha Nyanduga.
" Mradi huu ulianza kujengwa 2019-2020 lakini mradi ulikuwa haujakamilika. Wananchi wamekuwa wakilalamika sana kutokamilika kwa mradi na wakalalamika kutoshirikishwa kwenye hatua zote za utekelezaji wa mradi wa maji.
" Pia wanalalamika kupanda kwa gharama za uniti za maji toka sh. 1800 hadi 2000 kwa uniti moja ya maji. Wananchi wanataka maji yapatikane kwa wakati na yapatikane maeneo yote. RUWASA walete mabomba wasambaze maji kitongoji cha Mirare na Masangura walivyoviacha" amesema Mwenyekiti.
Alipoulizwa kuhusu muhtasari amesema " Mimi siyo mtunzaji wa nyaraka mimi ni msimamizi wa vikao ukiniuliza muhitasari mimi sina masijala" amesema.
Mtendaji wa kijiji cha Nyanduga Mkami Wambura amesema kuwa hakupewa taarifa mapema ya kuwasilisha muhtasari wa 2019 hivyo angepewa muda mapema angeutafuta na kuuwasilisha.
"Faili lipo ila sikujua kikao kitahitaji muhtasari wa tarehe ngapi, ningejua kuwa kinahitajika muhtasari wa kikao fulani ningepekua kwenye mafaili, toka 2019 hadi leo ni muda mrefu na mafaili yalishafungwa yapo pembeni mmenishtukiza " amesema Mtendaji.
Meneja RUWASA Azungumza
Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) wilaya ya Rorya , James Kishinhi amesema chagamoto iliyopo katika kijiji hicho wananchi walitaka washirikishwe kwenye hatua zote za ununuzi na hatua ya kumpata mzabuni.
"Tumekubaliana kwamba tuanzie kwenye ajenda ya awali tuwe na muhtasari ule wa wakati wa utambulishaji wa mradi na kazi zilizofanyika hadi sasa kudadavua hadi hapa tulipofika japo maji yapo. Wanataka kujua mchakato mzima wa ukarabati wa mradi wa maji Nyanduga wa Milioni 111.
" Na sisi tumekubali tutaleta muhtasari kwasababu tuliitwa tu kwenye kikao hatukuwa tumeandaa muhtasari, tulikuja tu na taarifa za kazi zilizofanyika. Tulikuwa tunafanya ukarabati wa mradi, kuna vitongoji vya Masangura naMirare ambavyo vilikuwa havipo vilizaliwa baada ya kugawanywa vijiji toka mradi ulipojengwa miaka ya 1980 havikuwepo kwa kipindi hicho.
Amesema wananchi wanahitaji maji kwenye vitongoji hivyo ambavyo kwasasa vina watu na kwamba wamepokea ombi RUWASA itapeleka maji kitongoji cha Masangura na Mirare.
" Tayari tumechukua bomba za ziada tulizokuwa nazo nakuzipeleka kwenye vitongoji hivyo ili waweze kupata maji. Huu Mradi ulipangiwa Milioni 111 kwa ajili ya ukarabati wa mradi, tumekarabati kuanzia chanzo cha maji ambapo tulifunga pampu na kupelea umeme.
" Awali tulikuwa tunatumia jenereta kwa kutumia nishati ya dizeli, tulifanya ukarabati wa bomba kuu na kuondoa bomba zilizofungwa miaka ya 1980 na kuweka bomba zingine , ukarabati wa tenki na vituo vya kuchota maji kwa sasa mradi umekamilika na vituo vyote vinatoa maji.
" Jamii ilitaka ishirikishwe kwenye hatua za manunuzi ambapo awali tulitumia mfumo ambao manunuzi yalinunuliwa kitaifa yakaletwa mkoani, jamii ilitaka ishiriki katika ununuzi wa mabomba" amesema.
Post a Comment