RC MARA AWATAKA VIONGOZI WA SERIKALI KUTOA USHIRIKIANO KWA WAANDISHI WA HABARI
>> Awataka viongozi kutokuwa vikwanzo wa Waandishi wa Habari
Na Jovina Massano Musoma
VIONGOZI wa serikali mkoani Mara wametakiwa kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari pindi wanapohitaji taarifa katika ofisi zao na si kutoa vitisho.
Hayo yamesemwa hivi karibuni Mei 17,2024 na mkuu wa mkoa wa Mara, Kanali Evance Mtambi katika maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya habari yaliyofanyika katika ukumbi wa Afrilux Hotel.
Mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evance Mtambi aliyeketi mbele wa pili kushoto akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya waandishi wa habari mkoa wa Mara.
Kanali Mtambi amesema kuwa amesikia kuwa wapo viongozi wa umma ambao hawataki kutoa ushirikiano na waandishi na badala yake wamekuwa wakiwapa vitisho.
"Nimesikitishwa kusikia viongozi wa serikali wanatoa vitisho kwa waandishi wa habari na kutotoa taarifa zinazohitajika, hili ni jambo la ajabu sasa natoa agizo kwa viongozi wa mkoa huu kutokuwa vikwazo kwa waandishi", amesema Kanali Mtambi.
Amesema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt.Samia Suluhu Hassan imefanya maendeleo makubwa wananchi wanapaswa kupata taarifa.
Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Mara, Raphael Okello amemshukuru Kanali Mtambi kwa kuonyesha ushirikiano kwa Waandishi wa habari tangu alipowasili mkoani hapa na ameomba taasisi zingine kuiga mfano huo.
Mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evance Mtambi wa pili kushoto, akiwa na viongozi wa Mara Press Club, wa kwanza kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Mara Press Club Raphael Okelo, na Malima Lubasha.
Ameongeza kuwa hivi sasa mkoa una Waandishi wapatao 60 baadhi yao wanamiliki vyombo vyao vya habari vipatavyo 17 licha ya kukutana na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuhabarisha umma.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Musoma Urassa Magambo amewaomba Waandishi wa habari kuandika habari za kijamii kwani kuna changamoto mbalimbali ili ziweze kutatuliwa.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Wilaya ya Musoma Urassa Magambo
"Nawaomba Waandishi wa mkoa huu wananchi wana changamoto mbalimbali katika maeneo yao hawajui namna ya kuwapata hasa waliopo pembezoni mwa ziwa mkifika huko mtaisaidia jamii hiyo kusikiwa kilio chao,"amesema Urassa.
Urassa ameongeza kwa kusema
kuwa hivi sasa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi maji kuongezeka kumekuwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kiafya kutokana na uchafu uliopo pembezoni mwa ziwa Victoria zikitolewa taarifa kutasaidia kuzuia magonjwa kwa wananchi hao.
Post a Comment