UTATA KUONDOLEWA UONGOZI KATIBU HAMASA NA CHIPUKIZI WILAYA YA RORYA
>>Katibu UVCCM Siri Makanaki asema Katibu Hamasa ameondolewa madaraka kwa makosa ya utapeli, ubadhilifu
>>Asema hana pingamizi na maamuzi ya Baraza la Vijana
>>Katibu Hamasa Emmanuel Onjiro akanusha tuhuma
>> Asema Makanaki na genge lake waliunda njama kuondolewa kwake
Na Dinna Maningo, Rorya
UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) ni chombo kinachowaunganisha vijana wake wa Tanzania wanaounga mkono sera, siasa na itikadi ya chama cha Mapinduzi.
Wilayani Rorya mkoani Mara, kumeibuka mgogoro wa kiungozi baina ya Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM ) wilaya ya Rorya, Siri Makanaki na Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa wilaya hiyo, Emmanuel Paulo Onjiro jambo ambalo limesababisha kuwagawa wanajumuiya.
Katibu huyo wa UVCCM wilaya amekaimu pia ofisi ya Katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Rorya kutokana na Katibu wa CCM wilaya hiyo Loth Hilemeirut ni mgonjwa na yupo nje ya ofisi kwa matibabu .
Mwezi Januari, 08, 2024, katibu huyo wa UVCCM alimwandikia barua Emmanuel Onjiro ya Maazimio ya Baraza la Vijana wilaya ya Rorya la Desemba, 23, 2023 lililomuondoa kwenye nafasi ya Katibu wa Hamasa na Chipikizi (W).
Katika barua hiyo imeelezwa kuwa kikao hicho cha Baraza kilichoketi katika ofisi ya CCM wilaya, pamoja na mambo mengine ya uhai wa jumuiya, kikao kiliweza kupitia tabia na mienendo ya Onjiro kama kiongozi wa ngazi ya juu.
Mienendo hiyo ikiwemo ya utapeli na ubadhilifu wa mali za watu kwa nyakati tofauti ilipelekea kikao cha baraza kumuondoa kwa kura 101 kati ya kura 108 za wajumbe waliohudhulia kikao.
Katika barua hiyo Katibu UVCCM wilaya hiyo ameeleza kuwa kikao kilichomvua madaraka ndicho kilichompatia wadhifa huo na kwamba ofisi ya wilaya ya UVCCM haina kipingamizi na maamuzi hayo ya kikao cha baraza.
Kupitia barua hiyo Katibu huyo wa UVCCM amemtaka Onjiro kutotumia cheo cha Katibu Hamasa wilaya kwa manufaa yake binafsi , barua aliyoisaini na kugongwa mhuri wa chama wa jumuiya hiyo na nakala kutumwa kwa katibu CCM wilaya ya Rorya na katibu wa UVCCM mkoa wa Mara.
Hata hivyo Januari, 24, 2024, Katibu Hamasa wilaya hiyo ya Rorya Emmanuel Paulo Onjiro aliyeondolewa madaraka ya nafasi hiyo ya uongozi alikata rufaa kwenda ofisi ya umoja wa vijana mkoa wa Mara.
Pia alituma nakala ya barua kwa Katibu wa CCM wilaya ya Rorya, Katibu wa CCM mkoa wa Mara, Katibu hamasa na Chipukizi mkoa wa Mara, Katibu mkuu UVCCM Taifa na Katibu hamasa na chipukizi UVCCM Taifa.
Katika barua yake alieleza juu ya mwenendo wa tabia na utendaji kazi wa Katibu wa UVCCM wilaya ya Rorya, Siri Makanaki na tuhuma za uongo dhidi yake kwa lengo la kumuondoa kwenye nafasi yake ya Katibu hamasa.
"Nitasema ukweli daima, fitina kwangu mwisho '. Natambua kuwa upotoshaji wowote katika barua yangu unaweza kutumiwa kuniadhibu kulingana na taratibu na kanuni za chama cha Mapinduzi, hivyo nakiri kuwa malalamiko haya ni ya kweli kulingana na uelewa wangu" ilielezwa kwenye barua.
"Katibu Makanaki amekuwa na mwenendo wa utendaji usiokuwa na madili ya uongozi na unaochafua taswira ya UVCCM hali inayopelekea wanajumuiya kususia kushiriki kazi za jumuiya na chama na hivyo kudhoofisha uhai wa jumuiya na chama" imeelezwa katika barua ya Onjiro.
Mwandishi wa DIMA Online alifika nyumbani kwa Emmanuel Onjiro katika kijiji cha Wamaya, kata ya Kirogo na kuzungumza nae wakati akiwa wilayani humo akifuatilia sakata la yeye kuondolewa uongozi na mienendo ya jumuiya hiyo.
Onjiro anakanusha tuhuma zilizoelezwa katika barua ya Katibu UVCCM wilaya katika kikao cha Baraza la UVCCM wilaya hiyo kilichoketi Desemba, 23, 2023 kilichomuondoa uongozi.
Emmanuel Onjiro anasema ni kweli kikao cha Baraza la UVCCM wilaya hiyo kiliketi ambapo mgeni rasmi katika kikao hicho alikuwa Katibu wa Hamasa na Chipukizi mkoa wa Mara, Leonard Otuoma na kwamba katika ajenda za kikao hicho hakukuwa na ajenda yoyote iliyohusu katibu hamasa wa wilaya.
" Sijawahi kuitwa kwenye kikao chochote rasmi kuhusu malalamiko ya mtu yeyote kwenye chama dhidi yangu kwamba mimi nimetapeli mali za watu. Kamati ya utekelezaji ambayo ndio kikao kinachojadili ajenda zote kabla ya baraza kukaa haikuwahi kujadili swala langu wala kuniita kunionya kwa kosa lolote lililotajwa kwenye barua ya Katibu.
" Siku ya kikao cha Baraza baada ya mgeni rasmi kuondoka katibu na genge lake waliibua madai hayo ya uongo na katibu akasimamia zoezi la kupiga kura kuniondoa kwenye nafasi yangu bila hata kutaka kunisikiliza, nilinyimwa haki yangu ya msingi ya kusikilizwa wala kujitetea" anasema.
Onjiro anasema " Ndani ya kikao walikuwepo watu wasiokuwa wajumbe halali wa kikao wapatao 13 ambao ni vijana 8 wa itifaki, katibu wa CCM Kata ya Kyangasaga, na wajumbe wengine wanne walioorodheshwa kwenye mahudhurio ya siku hiyo" anasema Onjiro.
Anasema kuwa kura anazodai Katibu kuwa ziliridhia kuondolewa kwake katika nafasi yake hazikutangazwa mbele ya wajumbe kwani Katibu wa CCM wilaya ya Rorya Loth alimuelekeza katibu wazazi wilaya, Furaha Bwire amuamuru Katibu Makanaki asitishe zoezi hilo kwakuwa ni batili.
Anasema Baraza hilo lilikuwa ni batili kwakuwa lilikuwa na vurugu juu ya kuondolewa kwake na katibu Makanaki mwenyewe alisema mbele ya wajumbe kuwa atawataarifu juu ya muafaka wa hilo jambo kwani vikao bado vinaendelea.
" Cha kushangaza ni kuwa siku ya Januari, 22, 2024 nilipokwenda ofisini katibu Makanaki aliniita na kunikabidhi barua ya kuondolewa kwenye nafasi yangu, barua iliyoandikwa Januari, 08, 2024. Barua ambayo kimsingi haisemi wazi kuwa makosa hayo ya utapeli nilimfanyia nani na wala haitaji watu wanaonilalamikia" anasema Onjiro.
"Barua iliyoandikwa na katibu Makanaki ni utashi wake yeye na genge lake akiwemo Katibu wa Senet, Alloyce Ayuka waliokuwa wakinituhumu kwa makosa ya kutunga na wala sio maamuzi ya baraza" anasema Onjiro.
Onjiro anasema sababu nyingine ya kuondolewa nafasi ni baada ya kuwatetea vijana wa kike ambao Katibu Makanaki aliwataka kimapenzi na wakakataa na wengine kuwatishia kuwaondoa kwenye nafasi za uongozi.
Anasema matendo ya katibu wa UVCCM wilaya ya kuwataka vijana wa kike mapenzi na vitisho vya kuwaachisha nafasi zao yamepelekea baadhi ya vijana kuacha kushiriki shughuli za jumuiya.
Katika barua ya Onjiro aliyokata rufaa kupinga kuondolewa amewataja baadhi ya vijana wa kike ambao katibu wa UVCCM aliwataka kimapenzi na wengine kuwatishia kuwaachisha nafasi zao za uongozi.
Vijana wa kike waliotajwa katika barua yake, ni Zainab Oketch kutoka kata ya Kirogo, Jemima Juma wa kata ya Kigunga na vijana wa kike waliotajwa kwa jina moja la Roina wa kata ya Baraki na Magreth wa kata ya Koryo pamoja na mwanafunzi anayedaiwa kuwa na mahusiano na katibu Makanaki.
Katibu UVCCM Rorya azungumza
Mwandishi wa DIMA Online amefika ofisi ya CCM wilayani Rorya na kuzungumza na Katibu wa UVCCM wa wilaya hiyo, Siri Makanaki kutaka kufahamu sakata hilo na ni watu gani waliotapeliwa fedha na Onjiro.
Pia kufahamu ubadhilifu wa mali uliotendwa na kijana huyo aliyeondolewa ukatibu kama alivyoeleza kwenye barua yake, kwani barua iliyoandikwa na Makanaki hayakutajwa majina na mali ambazo Onjiro ametapeli na kufanya ubadhilifu wa mali.
Makanaki anasema ni kweli kikao hakikuwa cha kumjadili Onjiro bali hoja iliibuliwa miongoni mwa wajumbe kwenye kikao hicho na kwamba waliohudhulia wote walikuwa ni wajumbe halali isipokuwa katibu wa kata ya Kyangasaga alimwalika kwa ajili ya kuandika mhitasari.
"Mimi ni katibu ambaye ni mtendaji mkuu nina uwezo wa kumwalika mtu yeyote akaandika kile tu kinachozungumzwa na siyo kujenga hoja wala kupindisha neno. Mtu yeyote ambaye tunajua ni mwandishi makini tunaweza kumualika hata kama ni wewe.
"Hoja yake iliibuliwa kwenye ajenda ya mengineyo wajumbe wakanyoosha mkono akiwemo wa kutoka kwenye kata ambayo Onjiro alienda kutapeli.
" Wakaomba iongezwe kwenye mengineyo ya mwenendo wake kuwa sio mwadilifu. Kura zikahesabiwa na katibu wa senet mkoa wa Mara na mimi nikazitangaza kura 101 zilizokubali aondolewe kati ya kura 108 zilizopigwa.
Anasema kosa alilolifanya Onjiro ni kujipatia mali kwa kutumia jina la jumuiya kinyume cha utaratibu na kumtapeli fedha Samson Mkurunzi maarufu Nyasembo mkazi wa Kata ya Ikoma pamoja na kumuuzia mwanae kadi ya Chipukizi sh. 50,000 licha ya kwamba kadi hizo hutolewa bure.
"Alikwenda kwa Samson maarufu Nyasembo mfanyabiashara alikuwa anataka kwenda kununua ng'ombe za kupeleka mahari Kenya, huyo Onjiro alimwambia ampatie hiyo Milioni moja akamnunulie ng'ombe kwa bei rahisi, akampatia lakini hakununua akatokomea na fedha. Alimtapeli Tsh.500,000 kuwa amepata kazi shirika la AMREF eti bila kuwapa hawatampatia kazi.
" Alimtapeli pia huyo Nyasembo Tsh. Milioni 1.8 kuwa ana shamba hivyo ampatie fedha akamlimie, akampatia kuwa alime ekari 8 kati ya hizo tano za Nyasembo na tatu zake lakini hakufanya kama walivyokubaliana, akalima ekari chache, Nyasembo anamdai Onjiro jumla ya fedha zote Tsh. Milioni 2.9.
Anaongeza kusema " Nilimwambia aungane na vijana wengine kwenda kuzima mwenge mkoani Manyara akatumia nafasi hiyo kumtapeli Nyasembo laki mbili kuwa kateuliwa na kamati ya siasa kwenda kuzima mwenge Manyara. Aliharibu na kuiba betrii ya pikipiki ya UWT, alafu anasema nilimuomba elfu 30,000 eti alivyoninyima nikamjengea bifu, mimi na yeye nani wa kumpa mwingine pesa ".
Kiongozi huyo anasema kuwa Onjiro alipewa nafasi ya kujitetea lakini alipingwa na wajumbe na hivyo kumuondoa na kwamba alishapewa barua za onyo lakini bado amekuwa akiendelea na utapeli.
" Alafu barua za onyo inategemea, yapo maamuzi ya papo kwa papo, tulichokifanya ni kumtoa nje akae pembeni, tangu tumuondoe jumuiya ipo vizuri imetulia. Mwaka 2019 akiwa ananisaidia ofisini kwangu aliwahi kukataliwa na kamati ya utekelezaji ya mpito baada ya kuiba viti viwili, betri ya pikipiki ya UWT" anasema Makanaki.
Katibu huyo wa UVCCM anaongeza kusema " Samson Nyasembo alikuja kushtaki ofisini na tulishamuonya Onjiro kwa barua lakini habadiliki. Nafasi ya ukatibu hamasa haikatiwi rufaa ndiyo maana haijashughulikiwa na uongozi wa mkoa na hata taifa maana walisema rufaa yake haina kitu.
"Nilimwita nikamwambia hii rufaa yako umechemka unanilalamikia kuwa sina adabu kuwa natembea na wanawake wa UVCCM, haya walete hao wanawake uliowataja kwenye rufaa.
"Istoshe rufaa wanaiangalia ina mantiki ipi, yeye alipaswa kukata rufaa ya kuondolewa kwenye nafasi ya uhamasishaji sasa yeye ananikatia rufaa mimi" anasema Makanaki.
Anaongeza kusema " Anasema eti natembea na wanawake wa UVCCM kwani yeye amekuwa inchaji wa kujua wanawake ninaotembea nao ?, mi nilifikiri anasema natembea na watoto wa shule labda nimewapa mimba, yeye anawasema wanawake ambao wana waume na watoto ambao wana akili zao timamu.
" Mara eti natembea na mwanafunzi yaani Mwandishi ukimwona huyo wanaesema natembea nae ni kitoto kidogo nihangaike nae wa nini wakati kuna mabinti watu wazima. Kubwa lililomuondoa ni hili la kuuza kadi ya chipukizi sh 50,000" anasema Makanaki.
Katibu Hamasa UVCCM akanusha
Emmanuel Onjiro anakanusha tuhuma hizo na kusema kuwa Samson Nyasembo ni rafiki yake na hajawahi kumdhulumu na kwamba hakuuza kadi Tsh.50,000 bali fedha hiyo aliomba kwa ajili ya uchapaji fomu na nauli kwenda Musoma.
"Ukiangalia tuhuma hizo zinamhusisha mtu mmoja tena maswala binafsi, mimi sijamtapeli Nyasembo. Unawezaje kumtapeli mtu bado aendelee kukupa pesa kama sio tuhuma za kupika!. Istoshe ni rafiki yangu hata sasa akiwa na jambo lake katika shughuli zake ananishirikisha na hakuna barua yoyote iliyoandikwa na Nyasembo kuwa nimemtapeli.
" Nilimuomba elfu 50, 000 nitolee fumu za kugawia vijana kwa ajili ya kuomba nafasi ya uongozi katika uchaguzi akiwemo mtoto wa Samson aliyegombea nafasi ya chipukizi.
" Nilizitumia kuchapa na kudurufu fomu nikazipeleka mkoani kwa usafiri wa pikipiki kwenda na kurudi Utegi. Anasema nimeiba viti viwili vya ofisi si kweli nilimuomba akanipa mbona yeye alichukua viti saba akapeleka kwake Bunda!, sijaiba betri ya pikipiki.
Anaeleza "Nilipofikisha zile fomu Katibu wa mkoa alisema watu wamezidi umri nirudi nirudie zoezi, nikarudi kisha nikazipeleka wakati huo katibu alinipa nauli 10,000, mkuu wa mafunzo alinipa Tsh. 18,000, zijumlishe fedha hizo na gharama za usafiri kwenda mkoani na kurudi zaidi ya mara moja bado hujala, alafu ananiongopea kuwa niliuza kadi" anasema.
" Hiyo Tsh. 50,000 niliyopewa Katibu Makanaki aliniomba nimpatie Tsh. 30,000 baada ya kufahamu kuwa Nyasembo kanipatia fedha, nilivyokataa alianzisha chuki na kunigawa kwa wanauvccm na hapo ndipo vita ilizidi kuniandama" anasema.
Anaongeza " Sababu nyingine ni baada ya mzazi wa mwanafunzi wa kidato cha tatu ambaye ni kijana wa hamasa kufika kwangu tarehe 15, 11,2023 akimlalamikia katibu UVCCM kutembea na binti yake.
" Nikamjulisha Katibu Makanaki cha kushangaza akanilaumu kuwa mimi namtangaza kwa katibu wa Chama wilaya huku akinitishia kuniondoa kwenye madaraka kwamba yeye ana ushawishi mkubwa kwa wajumbe wa Baraza" anasema Onjiro.
Chombo hiki cha habari kikamtafuta Samson Nyasembo kufahamu yaliyoelezwa na Katibu UVCCM wilaya vikiwemo vitendo vya utapeli wa fedha na mali lakini pia kama amewahi kuandika barua ya malalamiko kwenye chama chicho au kushtaki ofisi za serikali ama Polisi.
Alitafutwa kupitia simu lakini simu yake haikupatikana, ambapo ilielezwa kuwa yupo nje ya nchi nchini Kenya. Hata alipotafutwa kupitia WhatsApp kwa namba yake ya nchini Kenya simu iliita bila kupokelewa wala kujibu ujumbe wa maneno (SMS) .
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Rorya, Furaha Bwire alipotafutwa ili kufahamu madai ya katibu Hamasa juu ya katibu wa chama hicho wilaya kumwamuru yeye amzuie katibu Makanaki kustisha zoezi hilo la kumwondoa madaraka kwani ni batili, alipokea simu kisha kuomba kulizungumzia jambo hilo baadae lakini alipotafutwa tena ili kuzungumza hakupokea simu.
Onjiro anaiomba ofisi ya UVCCM mkoa wa Mara kufuatilia swala hilo na kuchukua hatua zinazostahiki kwa haraka ikiwemo ya kupatiwa haki yake ya kusikilizwa na kubatilisha maamuzi binafsi ya katibu wa UVCCM dhidi yake.
Anasema yupo tayari kutoa ushahidi katika kikao chochote kama akihitajika yeye au wahusika aliowataja kwenye barua.
..........Itaendelea
Post a Comment