TANROADS MARA YAWATAKA WASAFIRISHAJI KUZINGATIA SHERIA
Na Jovina Massano Musoma
WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Mara imewashauri wasafirishaji wanaotumia magari kuanzia tani 3.5 kutozidisha uzito ili kupunguza uharibifu wa barabara.
Hayo yamesemwa Mei, 21,2024 na Meneja wa TANROADS mkoa wa Mara Mhandisi Vedastus Maribe wakati akizungumza kwa njia ya simu na Mwandishi wa DIMA Online ikiwa ni siku moja baada ya maadhimisho ya siku ya Vipimo Duniani kufanyika.
Mhandisi Vedastus amesema uzidishaji uzito una athiri haraka miundombinu ya barabara ambapo marekebisho huhitaji fedha nyingi.
Amesema kuwa wasafirishaji wanao wajibu wa kubeba mizigo yenye kiwango sahihi kama sheria inavyoelekeza lakini pia kuondokana na faini zisizo za lazima.
"Mkoa wa Mara una vituo viwili ambavyo ni Sirari wilayani Tarime na Rubana wilayani Bunda. TANROADS pia imeweka utaratibu wa kuhakiki mizani zilizopo kila baada ya miezi mitatu kwa kushirikiana na wataalam wa uhakiki mizani kutoka kwa Wakala wa Vipimo(WMA).
Ameongeza kuwa TANROADS hutoa semina kwa wasafirishaji kwa lengo la kuwaelimisha na kuwakumbusha kuzingatia sheria na kanuni zake.
"Mei, 8, 2024 TANROADS tumetoa semina kwa wasafirishaji wa Kanda ya ziwa kuhusu sheria ya uthibiti uzito wa magari ya Afrika mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 iliyofanyika jijini Mwanza yenye lengo la kukumbushana na kujifunza juu ya Sheria na kanuni hizo,"amesema Vedastus.
Dereva wa magari makubwa Haji Madege kutoka Mafinga mtaa wa Mgodi Kata ya Kinyanambo amesema uwepo wa uthibiti uzito kwa kuweka mizani ni sahihi kwani inasaidia miundombinu kutochakaa.
"Mizani ziko sawa zinasaidia kulinda barabara zetu kwani watu wangekuwa wanabeba mizigo kupita kiasi japokuwa kuna baadhi ya maeneo mizani haziko sawa zinasababisha foleni kubwa niwaombe wahusika wafatilie ", amesema Haji.
Amewapongeza wasimamizi wa mizani Kanda ya ziwa kwa kutokuwa na usumbufu kwenye vituo.
" Mara nyingi nimekuwa nikileta mzigo wa nguzo za umeme mkoani hapa sijawahi kupata kikwazo wakati wa kuhakiki uzito isipokuwa kama mwaka mmoja umepita mzani wa Rubana ulipata hitilafu taarifa zikafika kwa wahusika na Meneja wa TANROADS alifika kwa wakati na wataalam wake huduma ikaendelea .
Nae Fasil Mwinyimadi mkazi wa wilaya ya Ubungo Kata ya mabibo mtaa Kanuni dereva wa Lori ameomba kuwepo utaratibu wa utoaji elimu kwa madereva wa magari angalau mara mbili kwa mwaka wakiwemo,wamiliki na wasimamizi waliopo kwenye mizani hizo.
Post a Comment