RC PWANI : NATAMBUA MCHANGO WA WAANDISHI WA HABARI KATIKA KUCHOCHEA MAENDELEO
Na Gustafu Haule, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amesema anathamini mchango wa waandishi wa habari waliopo katika mkoa wake kwakuwa wanafanya kazi kubwa ya kuchochea maendeleo.
Kunenge ametoa kauli hiyo Mei, 23, 2024 wakati akifungua mkutano wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari uliofanyika katika ofisi za Mkoa huo ukiwajumuisha Waandishi wa habari pamoja na wadau mbalimbali.
Katika maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Klabu ya Waandishi Wa Habari mkoa wa Pwani Kunenge amesema kazi wanazofanya waandishi wa habari katika mkoa huo zinaonekana na zimekuwa zikileta matokeo chanya huku akisema lazima wathaminiwa.
Amesema kutokana na mchango mkubwa unaotolewa na waandishi hao ,yeye yupo mstari wa mbele kutoa ushirikiano katika kuhakikisha kazi ya Waandishi hao zinafanyika katika mazingira rahisi kama ambavyo Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan alivyoweka mazingira mazuri katika Sekta ya habari.
"Lazima niseme kweli Waandishi wa habari wa mkoa huu wanafanya kazi vizuri ya kutangaza mkoa wetu na niwahakikishie mimi ni kiongozi wa ushirikiano na lazima watendaji wangu nao wawe na ushirikiano ,"amesema Kunenge
Akizungumzia masuala ya uchumi kwa Waandishi wa habari Kunenge amesema kuwa kwasasa ataweka mipango mizuri na wezeshi ambayo itawasaidia Waandishi kuwa na uchumi imara huku akimuagiza Katibu Tawala mkoa wa Pwani Rashid Mchatta kukutana kwa haraka na viongozi wa Klabu hiyo ili kuanza utekelezaji wa jambo hilo.
Waandishi wa habari na wadau mbalimbali wakiwa katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yaliyofanyika Mei 23 Mjini Kibaha chini Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Pwani .Amesema kuwa mkoa wa Pwani ni Mkoa wa viwanda wenye kuzalisha bidhaa mbalimbali lakini bado waandishi hawajafanikiwa kutangaza bidhaa zinazozalishwa ambapo amewataka Waandishi hao kujikita katika kutangaza bidhaa hizo ili Mkoa hupate kufahamika zaidi kutokana na bidhaa hizo.
Kuhusu changamoto ya mazingira Kunenge amesema mkoa umepokea maagizo kutoka kwa Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango wa kutoridhishwa na janga la kukata miti na kuchoma mkaa ambapo kwasasa tayari wameweka mkakati wa utekelezaji wa jambo hilo.
Amesema miongoni mwa mambo ambayo Mkoa umeanza kuyafanyiakazi ni kupiga marufuku bodaboda zinazojulikana kwa jina la busta kubebea mkaa na badala yake zinazotakiwa kutumika ni Toyo ( pikipiki za matairi matatu).
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta amewapongeza waandishi wa habari kwa namna wanavyofanya kazi na Serikali ya mkoa huku akisema kwasasa ni lazima kuweka mikakati mizuri ya kufanyakazi.
Waandishi wa habari na wadau mbalimbali wakiwa katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yaliyofanyika Mei 23 Mjini Kibaha chini Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Pwani .Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi habari Mkoa wa Pwani Ally Hengo amesema maadhimisho hayo kidunia yalifanyika Mei 03 mwaka huu na kitaifa yalifanyika mkoani Dodoma lakini kwa mkoa wa Pwani yalisogezwa mbele kwa ajili ya kupisha shughuli za mwenge.
Hengo pamoja na mambo mengine ametumia nafasi hiyo kumshukuru Mkuu wa Mkoa kwa namna ambavyo anatoa ushirikiano kwa Waandishi wa habari ikiwa pamoja na kuendelea kukamilisha aadi yake ya kutoa kiwanja cha ofisi ya Waandishi wa habari aliyoitoa mwaka 2022.
Hata hivyo katika maadhimisho hayo mada mbalimbali zilitolewa ikiwemo mada ya mazingira iliyotolewa na afisa misitu wa mkoa wa Pwani Pierre Protas.
Kamanda wa zimamoto mkoa wa Pwani Jenifa Shirima ametoa mada ya kujiepusha na majanga ya moto pamoja na mada ya maadili iliyotolewa na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano Serikali kutoka Mkoa wa Pwani Zablon Bugingo.
Afisa misitu wa Mkoa wa Pwani Pierre Protas akitoa mada katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yaliyofanyika leo Mjini Kibaha Mkoani Pwani.
Post a Comment