WAANDISHI WA HABARI WAHIMIZWA KUEPUKA KURIPOTI TAARIFA ZA DAWA ZINAZOIBUA TAHARUKI
Na Andrew Chale, Iringa
MKUU wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba amewataka Waandishi wa Habari nchini kuripoti habari sahihi ilikuepuka taharuki ikiwemo suala la kuripoti habari za dawa na vifaa tiba ambalo lipo chini ya Mamlaka ya dawa na vifaa tiba nchini (TMDA)
Akifungua kikao kazi hiko, Mei 16, 2024 kilichowakutanisha Wahariri na Waandishi wa Habari kutoka Dodoma, Singida, Iringa na Dar es Salaam, Serukamba amesema kuwa TMDA haiwezi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi bila ushirikiano wa Waandishi wa Habari kupitia Vyombo vyao mbalimbali hapa nchini .
‘’Ni imani yangu kuwa kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na kushirikisha wananchi, mtaweza kuelewa matatizo yaliyopo katika jamii yanayohusiana na usalama na ubora wa bidhaa zinazodhibitiwa na TMDA, na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha kwamba sheria ya dawa na vifaa tiba sura 219 inatekelezwa na wadau wote kwa ufanisi.’’ Amesema Serukamba.
Mkuu huyo wa mkoa akimnukuu Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu. Julius Nyerere, kuhusu kuripoti habari sahihi amesema;
‘’Raia wanahitaji taarifa sahihi na zenye kuaminika katika wakati sahihi.
Vivyohivyo kwa wafanyabiashara kwenye masoko hata na Serikali.
"leo mmealikwa katika kikao kazi hiki ili mkasaidie kupunguza taharuki, kwa kuhakikisha kwamba mnazingatia kupata taarifa sahihi kutoka katika vyanzo sahihi.
Wakati huohuo, Mkuu huyo wa mkoa ameipongeza TMDA kwa mambo makubwa inayokabiliana nayo hususani uwepo wa dawa duni na dawa bandia.
Baadhi ya Waandishi wa habari na Wahariri kutoka Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa katika picha ya pamoja na mkuu wa mkoa Iringa, Peter Serukamba na watendaji wa TMDA
‘’Ni matumaini yangu mtaweka mikakati ya pamoja juu ya kuimarisha udhibiti wake pamoja na udhibiti wa matangazo ya bidhaa husika ili wananchi wapate taarifa sahihi na kuweza kufanya uchaguzi wa bidhaa zenye usalama na ubora wa afya zao.’’ amesema Serukamba.
Serukamba ameviomba vyombo vya habari kuelimisha umma kuachana na matumizi ya dawa duni na bandia ambazo zimekuwa zikiripotiwa uwepo wake hapa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo amesema kuwa Mamlaka hiyo inafahamu umuhimu wa sekta ya habari nchini hivyo wataendelea kushirikiana na Vyombo vya habari.
Amesema TMDA imefanikiwa kuweka mifumo mizuri ya udhibiti wa dawa ambayo imehakikiwa na shirika la Afya Duniani (WHO) na kwamba wanafanya kazi kubwa na kwa ufanisi kwa kufuata mifumo iliyopo.
‘’Nisema tu, tunafahamu sekta ya habari ni muhimu. Na kazi yetu kulinda afya za jamii ni kuifikia jamii katika kuipasha habari kupitia vyombo vya habari ambavyo huwafikia wananchi wengi.
Dkt. Fimbo amesema TMDA imekuwa ikizunguka kila Kanda kukutana katika vikao kazi hivyo na wahariri na waandishi kwa kutoa mada mbalimbali za watalaama, lakini pia kutoa tuzo kwa Waandishi wa Habari wanaoripoti habari za Mamlaka hiyo.
‘’Tumefanya hivyo Mbeya, Dar es Salaam, na sasa tupo hapa Iringa.’’ amemalizia Dkt. Fimbo.
Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma, Gaudensia Simwanza, akielezea jambo wakati wa kikao kazi na Waandishi na wahariri kilichofanyika tarehe 16 Mei,2024.
Post a Comment