HEADER AD

HEADER AD

MTOTO MWENYE ULEMAVU WA NGOZI AIBWA



Na Alodia Babara, Muleba

Noela Asimwe Novath mtoto mwenye umri wa miaka miwili na nusu mwenye ulemavu wa ngozi (albinism) katika kijiji cha Bulamula, Kata ya Kamachumu wilaya ya Mureba mkoani Kagera ameibwa katika mikono ya mama yake.

Imeelezwa kuwa mtu mmoja asiyejulikana alibisha hodi nyumbani kwao na kuomba msaada wa chumvi akidai amenga’twa na nyoka.

Mama mzazi wa mtoto huyo Judith Richard amesema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 30, mwaka huu saa 7:30 jioni wakati mama huyo akiwa amekaa ndani na mtoto wake ndipo mtu alipiga hodi bila kutaja jina lake na kusema kuwa, amenga’twa na nyoka hivyo  anaomba msaada wa chunvi.

Judith amesema kuwa alifungua mlango na kumuona mtu ambaye alikuwa akitembea kwa kuchechemea bila kujua, kumbe alikuwepo mtu mwingine amejibanza ukutani.

Anasema ghafla aliyekuwa amejibanza ukutani alimkaba koo na aliyekuwa anachechemea aliingia ndani na kutokomea na mtoto kusikojulikana.

 “Kuna mtu alipiga hodi akaniita mama Asimwe naomba unisaidie chumvi  nikamuuliza wewe nani akajibu mie Kelvin wa wapi wa humu humu kitongojini Mbare, awali roho ikasita baadaye nikawaza siwezi kujua atakayenisaidia nikafungua mlango nikiwa nimewasha tochi ya simu yangu.

" Nilimuona mtu amaejibanza ukutani muda huo huo alikuja haraka akanikaba shingo dakika kama nne amenikaba na aliyekuwa anajifanya anachechemea aliingia ndani na kutokomea na mtoto wangu” amesema Judith.

Amesema baada ya mtu huyo kumwachia alianza kupiga kelele za kuomba msaada ndipo mke wa shemeji yake alitoka na yeye kuanza kumsaidia kupiga kelele za kuomba msaada wanakijiji walikusanyika.

Mkuu wa wilaya ya Muleba Dkt Abel Nyamahanga amesema kuwa, jeshi la polisi limeshaweka mtego kila sehemu kwa ajili ya kuwakamata watu waliofanya kitendo vya wizi wa mtoto huyo.

Dkt Nyamahanga ameitaka jamii ya wakazi wa Muleba kuendelea kuonyesha mshikamano katika kumtafuta mtoto huyo kama ambavyo walifanya toka tukio lilivyotokea.

“Sisi kama serikali kwa kushirikiana na jeshi la polisi tunaendelea kupambana na mitego yote tuliyoitega tulitoa taarifa kila kona ili kuwanasa waharifu.

" Maelekezo yetu kama serikali ukiona matukio haya yameanza, wameanza kutikisa kiberti kijiji chochote ndani ya wilaya ya Muleba wenye binadamu mwenye ualibino kupitia kwa maafisa ustawi wa jamii waripoti kila siku juu ya usalama wa watu hawa”

“Na nyie wanawake msiwaache watoto wenu bila mtu yeyote mkaenda kuchota maji umbali wa mita kadhaa tuwalinde kwa kila namna na kwa gharama yoyote kwa sababu ni binadamu wenzetu” amesema Dkt Nyamuhanga.

Kaimu Kamanda mkuu wa jeshi la Polisi mkoa Kagera Yusuph Daniel amesema wanaendelea na msako wa kutafuta waalifu waliohusika kupora mtoto huyo na wamefanikiwa kuwakamata watu watatu washukiwa wa tukio hilo.

Kamanda Daniel amesema katika uchuguzi wanaoendelea nao bado ni mapema kusema tukio hilo la kupora mtoto mwenye Ualbino limehusisha  imani za kishirikina na bado hakuna mwananchi yeyote ambaye amethibitisha hilo.

Jeshi la polisi mkoa Kagera linatoa wito kwa wananchi  kushirikiana na polisi kata kufanya msako  kwa ajili ya kumpata mtoto huyo na kutoa taarifa za uharifu unaotokea kwenye maeneo yao.

No comments